Friday, February 17, 2012

ASKOFU ACHANGIA VYOMBO VYA MUZIKI


ASKOFU wa Jimbo la Mashariki (TAG), Mchungaji Lawrence Kametta ametoa mchango wa vyombo vya muziki kwa Kanisa la TAG Kitunda Kati jijini Dar es Salaam ili kuendeleza vipaji vya muziki wa injili.

Askofu Kametta alitoa mchango huo juzi wakati akizindua rasmi jengo hilo la ibada, na kuomba kushirikishwa katika hatua zote za ununuzi wa vifaa hivyo.

Alisema kuwa badala ya watu kufurahia kwenda mpirani ama katika nyumba za anasa, ni vyema wakafurahia kuingia katika nyumba za mungu kwa kuwa sehemu hiyo ndiyo pekee ya tiba mbadala kwa matatizo yote.

"Vijana sugu, majambazi, wanaotumia dawa za kulevya matatizo yao hayawezi kumalizwa na viongozi, bali nyumba za mungu za pekee, ndio maana tujitolee kwa mioyo yetu yote kuzijenga nyumba hizi.
 
"Mtapata dhambi za bure kumlaumu Kikwete au kiongozi mwingine yeyote, kwa kuwa hakuna mwenye uwezo wa kubadilisha maisha ya wanadamu, tiba ya matatizo sugu ipo katika nyumba ya mungu, na nyumba hizi zikitumika sawasawa zitabadili maisha ya watu kimwili na kiroho,"alisema Askofu huyo.

Aliongeza kuwa, nyumba ya mungu ni karakana ya kiroho, hivyo ina uwezo wa kutengeneza mwili wa binadamu na ukarudi kuwa mpya na kuongeza kuwa ni tiba ya matatizo yote sugu.

"Wakati madaktari wakigoma, watumishi wa mungu hawana mgomo, wakati watoa huduma nyingine kwenye jamii wakigoma kwa kudai maslahi bora, watumishi wa mungu wapo wakitoa huduma bila kujali maslahi, wapo siku zote kwa tiba ya uponyaji. Hivyo ni vyema jamii ikazitiilia maanani nyumba za mungu kama mkombozi wa maisha yao duniani na mbinguni,"aliongeza Askafu Kametta.

Hata hivyo, aliwataka wananchi waelewe kuwa utakatifu wa mtu si mavazi, wala muonekano mzuri bali ni hali inayotoka ndani ya moyo ikiwa ni sambamba na kujitolea kufanya kazi za mungu kwa ibada na hata nyimbo.

Sambamba na kuchangia katika vyomvo vya muziki, Askofu huyo aliahidi kutoa mchango wake kwa kanisa hilo ambalo limejengwa kwa nguvu ya wananchi.

mwisho