JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA FEDHA
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA,
MHESHIMIWA DKT. WILLIAM A. MGIMWA (MB.),
AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2012/13
14 JUNI, 2012
DODOMA
I UTANGULIZI:
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liweze
kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa
mwaka wa fedha 2012/2013. Pamoja na hotuba hii, nimewasilisha vitabu
vinne vya Bajeti vinavyoelezea takwimu mbalimbali za Bajeti. Kitabu cha
Kwanza kinaelezea makisio ya mapato. Kitabu cha Pili kinaelezea makisio
ya matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea; Taasisi na
Wakala wa Serikali; cha Tatu kinahusu makisio ya matumizi ya kawaida
kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na cha Nne kinaelezea
makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea,
Taasisi na Wakala za Serikali; Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2012 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nitumie fursa hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa
aliyonayo kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Naahidi kutekeleza
majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa na
Mheshimiwa Rais kuwa mawaziri kama ifuatavyo: Mhe. Prof. Sospeter
Mwijarubi Muhongo (Mb); Mhe. Mhandisi Christopher Kajoro Chiza (Mb);
Mhe. Dkt. Harrison George Mwakyembe (Mb); Mhe. Dkt. Fenella Ephraim
Mukangara (Mb); Mhe. Balozi Khamis Sued Kagasheki (Mb); Mhe. Dkt.
Abdallah Omari Kigoda (Mb). Aidha, napenda kuwapongeza wafuatao kwa
kuteuliwa kuwa naibu mawaziri katika Wizara mbalimbali, Mhe. Janet
Zebedayo Mbene (Mb); Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb); Mhe. Dkt. Seif
Suleiman Rashid (Mb.); Mhe. George Boniface Simbachawene (Mb.); Mhe.
January Yusuf Makamba (Mb.); Mhe. Dkt. Charles John Tizeba (Mb.); Mhe.
Amos Gabriel Makalla (Mb.); Mhe. Angela Jasmine Kairuki (Mb.); Mhe.
Stephen Julius Maselle (Mb.); na Mhe. Mhandisi Dkt. Binilith Satano
Mahenge (Mb). Kadhalika, nampongeza Mhe. James Mbatia (Mb) kwa
kuteuliwa na Mhe. Rais kuwa Mbunge.
4. Mheshimiwa Spika, nawapongeza pia, Mhe. Alhaji Adam Kimbisa (Mb.);
Mhe. Shy Rose Banji (Mb.); Mhe. Abdulah Alli Hassan Mwinyi (Mb); Mhe.
Charles Makongoro Nyerere (Mb); Mhe. Dkt Twaha Issa Taslima (Mb); Mhe.
Nderkindo Perpetua Kessy (Mb); Mhe. Bernard Musomi Murunyana (Mb); Mhe.
Anjela Charles Kizigha (Mb.); Mhe. Maryam Ussi Yahaya (Mb.), ambao
wamechaguliwa kutuwakilisha kwenye Bunge la Afrika Mashariki. Ni
matumaini yangu watatuwakilisha vyema kwa maslahi na manufaa ya Taifa
letu.
5. Mheshimiwa Spika, maandalizi ya Bajeti hii yamehusisha wadau na
Taasisi mbalimbali. Napenda kuwashukuru walioshiriki kwa namna moja au
nyingine kufanikisha matayarisho yake. Kwa namna ya pekee, ninaishukuru
Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi chini ya uenyekiti wa Mhe. Mtemi
Andrew John Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi, pamoja na kamati
nyingine za kisekta kwa ushauri mzuri waliotoa wakati wakichambua
mapendekezo ya Bajeti hii. Aidha, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge
wote kwa ushauri na mapendekezo yao ambayo yamezingatiwa katika Bajeti
hii.
6. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mhe. Stephen Masatu Wasira
(Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kwa
ushirikiano alionipatia wakati wa maandalizi ya Bajeti. Aidha,
nawashukuru Naibu Mawaziri wa Fedha, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb) na
Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb). Namshukuru Katibu Mkuu Ndugu Ramadhani M.
Khijjah; Naibu Katibu Wakuu, Ndugu Laston T. Msongole; Dkt. Servacius
B. Likwelile; na Ndugu Elizabeth Nyambibo kwa mchango wao mkubwa katika
matayarisho ya Bajeti. Vilevile, nawashukuru Prof. Benno Ndulu Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania; Dkt. Phillip Mpango, Katibu Mtendaji Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango; Ndugu Harry Kitilya, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania; na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya
Takwimu ya Taifa. Nawashukuru wote kwa mchango wao katika maandalizi ya
bajeti hii. Naishukuru pia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa
kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 na
nyaraka mbalimbali za sheria ambazo ni sehemu ya Bajeti hii.
7. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Wakuu wa Idara, Wakuu wa
Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na wafanyakazi wote wa Wizara
ya Fedha kwa ushirikiano wao. Aidha, namshukuru Mpigachapa Mkuu wa
Serikali kwa kuchapisha Hotuba hii kwa wakati. Nawashukuru pia
wataalamu na wale wote waliotoa mapendekezo kuhusu sera, mikakati na
masuala mbalimbali ya kodi ambayo yamezingatiwa katika kuandaa Bajeti
hii.
8. Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa mwenyeji wa Mikutano ya Bodi ya
Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa Mwaka 2012 iliyofanyika
kuanzia tarehe 28 Mei hadi tarehe 2 Juni 2012 na kufunguliwa rasmi na
Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Mikutano hii ilifanyika kwa ufanisi mkubwa katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Arusha na kuhudhuriwa na washiriki 2,350
kutoka ndani na nje ya Tanzania. Hii imekuwa ni nafasi ya kipekee kwa
Tanzania kutangaza fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini. Aidha,
washiriki wa ndani kutoka sekta binafsi walipata nafasi ya kufahamu
fursa za mikopo zilizopo katika Benki ya Maendeleo ya Afrika. Napenda
kutoa wito kwa sekta binafsi kutumia fursa hizo kikamilifu.
9. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2012/13 imelenga kukabiliana na
changamoto zinazokabili uchumi ikiwa ni pamoja na; kuongeza fursa za
kukuza uchumi, kushughulikia uhaba wa chakula nchini, kupambana na
mfumuko wa bei, kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kusimamia
matumizi, kushughulikia suala la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana,
kuwekeza katika miundombinu ya nishati ya umeme hususan ujenzi wa bomba
la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, barabara, bandari na reli ya
kati ili kupunguza gharama za kufanya biashara na kuongeza tija katika
uzalishaji; pamoja na kulipa madeni ya ndani na nje.
II. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA SERA ZA BAJETI YA
MWAKA 2011/12
10. Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba sasa kutoa
taarifa kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/12. Mfumo wa Bajeti
ya mwaka 2011/12 uliendeleza juhudi za Serikali za kufikia malengo ya
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Aidha, bajeti ilizingatia utekelezaji
wa vipaumbele vya Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano
(2011/12 – 2015/16); Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015;
Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA); Ilani ya Uchaguzi ya
CCM ya mwaka 2010; Mkakati wa Taifa wa Madeni; pamoja na kuimarisha
usimamizi wa kodi na matumizi ya fedha za Umma.
11. Mheshimiwa Spika, misingi na shabaha za bajeti ya mwaka 2011/12,
pamoja na mambo mengine, ililenga kukamilisha malengo ya Serikali ya
kukabiliana na changamoto za kupunguza makali ya maisha kwa wananchi;
kuendelea kuboresha mfumo wa makusanyo ya mapato ya ndani; kuboresha
mazingira ya uwekezaji wa ndani na nje; kuendeleza sekta binafsi ili
kupanua wigo wa kodi; kukamilisha maandalizi ya Mradi wa Vitambulisho
vya Taifa; na kutenga rasilimali na kutekeleza miradi katika maeneo ya
kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
12. Mheshimiwa Spika, maeneo mengine yaliyozingatiwa katika misingi na
shabaha ya bajeti hiyo yalikuwa ni: kutekeleza mipango na mikakati
maalum ya kuharakisha ukuaji wa uchumi; kutafuta mikopo ya masharti
nafuu na ya kibiashara; kuharakisha utekelezaji wa Sheria ya Ubia kati
ya Sekta ya Umma na ya Binafsi ili kupanua fursa za utekelezaji wa
miradi ya maendeleo; Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012; kuhakikisha
kwamba maduhuli ya Serikali yanakusanywa ipasavyo na kuwasilishwa
katika Mfuko Mkuu wa Serikali; pamoja na kulinda na kudumisha mafanikio
yaliyopatikana katika Sekta za huduma za jamii, hususan elimu na afya
ambazo zimekuwa na upanuzi mkubwa wa huduma.
Hatua za Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/12
Kupunguza Makali ya Maisha
13. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/12,
Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto
zinazowakabili wananchi kwa lengo la kupunguza makali ya maisha
kunakotokana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma. Hatua
zilizochukuliwa ni pamoja na: kurekebisha namna ya kukokotoa gharama za
mafuta na kutangaza bei elekezi kila mwezi na kuanzisha utaratibu wa
uagizaji mafuta kwa pamoja (bulk procurement). Hatua hizi zimesaidia
kupunguza kasi ya upandaji wa bei ya mafuta hapa nchini.
14. Mheshimiwa Spika, Serikali imetumia shilingi bilioni 296 kutekeleza
mpango wa dharura wa kukabiliana na tatizo la upungufu wa nishati ya
umeme kwa kutumia mitambo ya kukodi. Utekelezaji wa jitihada hizi
umeongeza megawati 324 kwenye Gridi ya Taifa. Kadhalika, Serikali
ilitumia Dola za Marekani milioni 183 kugharamia ujenzi wa mitambo ya
kufua umeme wa megawati 100 kwa mkoa wa Dar es Salaam mradi ambao
umekamilika na uko kwenye hatua za majaribio na Megawati 60 kwa mkoa wa
Mwanza ambao bado ujenzi unaendelea.
15. Mheshimiwa Spika, Serikali imetumia shilingi bilioni 27 kugharamia
ununuzi na usambazaji wa tani 120,000 za mahindi katika masoko kwa
lengo la kukabiliana na uhaba wa chakula kwa baadhi ya maeneo. Aidha,
Serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari bila kutoza ushuru wa forodha
kiasi cha tani 200,000 ili kukabiliana na uhaba na kupanda kwa bei ya
sukari. Kadhalika, Serikali ilipandisha kiwango cha riba inayotozwa na
Benki Kuu kwa Taasisi za Fedha kutoka asilimia 7.58 hadi asilimia
12.58. Vilevile, Serikali ilipandisha kiwango cha amana ambacho benki
za biashara zinapaswa kuhifadhi Benki Kuu kutoka asilimia 20 hadi
asilimia 30. Hatua hizi zimesaidia kupunguza kasi ya kupanda kwa bei.
Kuwezesha Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira
16. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na tatizo la ajira, Serikali
imechukua hatua mbalimbali za kuongeza fursa za ajira. Hatua hizo ni
pamoja na: kuboresha mazingira ya kisera na kisheria kuwezesha sekta
binafsi kukua; kupanua huduma za fedha ikiwa ni pamoja na kuongeza
mitaji katika Benki ya Rasilimali, Benki ya Wanawake, Benki ya Posta na
Twiga Bancorp, na kufanikisha uanzishwaji wa kampuni ya kutoa mikopo ya
muda mrefu ya ujenzi wa nyumba na makazi. Hatua nyingine
zilizochukuliwa na kuchangia ongezeko la ajira ni pamoja na kujenga
miundombinu ya barabara, umeme, kilimo, mawasiliano na kuwezesha
wananchi kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji. Aidha, kuna Taasisi
mbalimbali ambazo zimechangia kutoa ajira kama vile, TASAF, SELF, VETA,
Shirika la Viwanda Vidogovidogo (SIDO), Taasisi ndogondogo za Fedha,
VICOBA, Benki za Kijamii na Mifuko ya Udhamini ya mikopo inayosimamiwa
na Benki Kuu. Katika mwaka 2011/12, Serikali iliajiri Walimu wa Shule
za Sekondari na Msingi 25,000, Maafisa Ugani wa Kilimo na Mifugo 4,499
na Watumishi wa Kada ya Afya 6,916.
Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Sekta Binafsi
17. Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza utekelezaji wa Mpango wa
Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji mwaka 2011 kufuatia kuidhinishwa kwake
mwaka 2010. Kupitia Mpango huu, taratibu na kanuni za mawasilisho na
malipo ya kodi na ushuru yanafanyika kwa njia ya mtandao. Utaratibu huu
umeongeza ufanisi kwa kuondoa usumbufu na upotevu wa muda katika
ulipaji wa kodi. Hadi sasa, zaidi ya asilimia 75 ya walipa kodi wakubwa
na walipa kodi wengine 2,795 wanafanya mawasilisho yao kwa njia ya
mtandao. Aidha, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianzisha
mfumo unaounganisha usimamizi wa kodi (Asycuda, ITAX) na benki za
biashara ili kurahisisha ulipaji wa kodi. Mfumo huu umeunganisha jumla
ya benki 25. Kadhalika, Mamlaka inatumia huduma za M-Pesa (Vodacom) na
“NMB mobile” kwa ajili ya kulipia kodi ya majengo na kodi ya mapato.
18. Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea na jitihada za kupunguza
urasimu katika utoaji wa mizigo bandarini kwa kuanzisha utaratibu wa
kuwasilisha nyaraka kwa njia ya mtandao kabla ya mizigo kuwasili.
Utaratibu huu umelenga kupunguza tatizo la mrundikano na upotevu wa
nyaraka na kupelekea kupungua kwa muda na gharama za uagizaji na
usafirishaji mizigo nje ya nchi. Serikali imepunguza vizuizi vya
usafirishaji mizigo ndani ya nchi kutoka 50 vilivyokuwepo kufikia 15,
isipokuwa vituo vya mizani na forodha. Lengo la hatua hii ni kupunguza
gharama za kufanya biashara na usumbufu wanaopata wafanyabiashara.
Sera za Mapato
19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali iliendelea
kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani yanayotokana na kodi
na yasiyo ya kodi kwa kuchukua hatua za kiutawala, kisera pamoja na
marekebisho ya viwango vya kodi na sheria.
20. Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya marekebisho katika Sheria ya
Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 ili kuboresha uzalishaji katika
sekta za Kilimo, Mifugo, Viwanda, Biashara na Utalii. Marekebisho hayo
ni pamoja na kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vipuri vya
zana za kilimo; chakula cha kukuzia kuku; nyuzi za kutengenezea nyavu
za kuvulia samaki; pamoja na kuanzisha utaratibu wa kuwarejeshea kodi
wageni kwa bidhaa walizonunua nchini wakati wanaondoka.
21. Mheshimiwa Spika, Serikali ilifuta msamaha wa Kodi ya Ongezeko la
Thamani kwenye kuuza na kupangisha majengo ya nyumba za kuishi za
Shirika la Nyumba la Taifa - NHC; kuondoa unafuu wa Kodi ya Ongezeko la
Thamani kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali isipokuwa kwenye vifaa vya
misaada kwa vituo vya kulelea watoto yatima na shule.
22. Mheshimiwa Spika, Serikali pia ilifanya marekebisho ya Sheria ya
Kodi ya Mapato, SURA 332 kwa kufuta kodi ya Zuio kwa usafirishaji wa
samaki nje ya nchi ili kuongeza utoaji wa huduma za usafirishaji wa
mazao ya samaki kutokea hapa nchini badala ya kupitia nchi za jirani.
Aidha, marekebisho yalifanyika katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA
147 kwa kupunguza ushuru wa bidhaa kwenye mafuta mazito ya kuendeshea
mitambo ili kupunguza gharama za uzalishaji.
23. Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ushuru wa Mafuta ya Petroli, SURA 220
ilifanyiwa marekebisho kwa kutoa msamaha wa ushuru unaotozwa kwenye
mafuta yanayotumika katika kuendesha meli, na vifaa vingine
vinavyotumika katika utafiti wa mafuta na gesi ili kupunguza gharama.
Aidha, marekebisho yalifanyika kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki, ya mwaka 2004 kufuatia kuridhia kwa Mawaziri wa Fedha
wa Nchi Wanachama kufanya marekebisho mbalimbali katika kukuza Sekta za
Viwanda, Usafirishaji, Mifugo, Biashara na Utalii. Vilevile,
marekebisho yalilenga katika kuboresha afya ya jamii na kuimarisha
ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
24. Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na
kuhamasisha na kuhakikisha mashine za kielectroniki – EFD zinatumika
ipasavyo; kuimarisha mfumo wa kusimamia vitalu vya kodi; kuongeza vituo
vya kutoa huduma kwa wateja na vya kukusanyia mapato; kuimarisha mifumo
ya malipo ya kodi; na kuboresha mfumo wa uthaminishaji kwa kuimarisha
ukaguzi wa hesabu za walipa kodi.
Mwenendo wa Ukusanyaji Mapato
25. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Serikali ilipanga
kukusanya mapato ya jumla ya shilingi bilioni 13,525.9 kutoka katika
vyanzo mbalimbali na kutumia kiasi hicho kwa matumizi ya kawaida na
maendeleo. Vyanzo vya mapato vilikuwa kama ifuatavyo: mapato ya ndani
yalikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 6,775.9; mapato kutoka
Serikali za mitaa yalikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni
350.5; misaada na mikopo ya kibajeti ilikadiriwa kufikia kiasi cha
shilingi bilioni 869.4; misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na ya
kisekta ilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 3,054.1; mikopo
ya ndani na nje yenye masharti ya kibiashara ilikadiriwa kufikia kiasi
cha shilingi bilioni 1,664.9; na mikopo ya kulipia dhamana na
hatifungani zinazoiva zilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni
810.9.
26. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mapato ya ndani ikijumuisha mapato
ya Halmashauri, hadi Aprili 2012 makusanyo yamefikia jumla shilingi
bilioni 5,684.5. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 80 ya makadirio ya
kukusanya shilingi bilioni 7,126.4 kwa mwaka 2011/12.
27. Mheshimiwa Spika, makusanyo ya kodi yalifikia shilingi bilioni
5,227.5 ambayo ni sawa na asilimia 84 ya makadirio ya kukusanya
shilingi bilioni 6,228.8. Kulingana na mwenendo wa makusanyo ya mapato
ya kodi kwa kipindi cha miezi kumi ya mwaka 2011/12, hadi kufikia
mwishoni mwa mwaka wa fedha 2011/12 Serikali inatarajia kukusanya jumla
ya shilingi bilioni 6,307.8 na hivyo kuweza kufikia lengo tulilojiwekea.
28. Mheshimiwa Spika, mapato yasiyotokana na kodi yamefikia shilingi
bilioni 451.6 ikiwa ni asilimia 83 ya lengo la kukusanya shilingi
bilioni 547.1 kwa mwaka. Kutokana na mwenendo huo, Serikali inatarajia
hadi Juni 2012 kufikia lengo.
29. Mheshimiwa Spika, mapato ya Serikali za Mitaa yalifikia kiasi cha
shilingi bilioni 143, sawa na asilimia 40.8 ya lengo la kukusanya
shilingi bilioni 350.5 kwa mwaka. Hadi Juni 2012, Serikali inatarajia
kukusanya jumla ya shilingi bilioni 200 kutokana na chanzo hiki ikiwa
ni asilimia 57 ya lengo la mwaka. Kutokufikia malengo ya ukusanyaji wa
mapato haya kumechangiwa na kuchelewa kuanza kutekeleza utozaji wa ada
za leseni.
Misaada na Mikopo ya Masharti Nafuu Kutoka Nje
30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali ilikadiria kupata
kiasi cha shilingi bilioni 869.4 kama misaada na mikopo ya kibajeti
ambapo hadi sasa Serikali imepokea shilingi bilioni 916.3, ikiwa zaidi
kwa shilingi bilioni 46.9. Ongezeko hili limetokana na baadhi ya
wafadhili kutoa fedha zaidi ya kiwango walichoahidi. Kwa upande wa
misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha mifuko ya kisekta,
hadi kufikia Aprili 2012 ilifikia shilingi bilioni 1,450.4 sawa na
asilimia 47 ya makadirio ya bajeti ya mwaka ya shilingi bilioni
3,054.1. Upungufu huu umesababishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa
baadhi ya miradi na kuchelewa kupokea taarifa ya fedha hizi kutoka kwa
washirika wa maendeleo na Wizara na Taasisi zinazotekeleza miradi
husika.
Mikopo ya Ndani
31. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012,
Serikali imekopa kiasi cha shilingi bilioni 526 kwa ajili ya kulipia
dhamana za Serikali zilizoiva ikiwa ni asilimia 64 ya lengo la mwaka la
shilingi bilioni 819.1. Aidha, Serikali ilipanga kukopa shilingi
bilioni 393.4 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa kwa ajili ya
kugharamia matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia Aprili 2012, Serikali
ilikuwa imekopa shilingi bilioni 232.6 sawa na asilimia 59 ya makadirio
ya mwaka.
Mikopo ya Nje yenye Masharti ya Kibiashara
32. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12 Serikali ilikadiria kukopa kiasi
cha Dola za Marekani milioni 822, sawa na shilingi bilioni 1,271.6 kama
mikopo ya kibiashara. Katika kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012,
Serikali ilisaini Mkataba wa mkopo wa kiasi cha Dola za Marekani
milioni 310 na Benki ya Standard ya Afrika Kusini. Hadi kufikia Aprili
2012, jumla ya Dola za Marekani milioni 229 ambazo zilitumika kulipia
madeni ya barabara ya mwaka 2010/11. Aidha, Serikali ilisaini Mkataba
wa mkopo wa Euro milioni 61 na Benki ya HSBC. Mkopo huu umeelekezwa
kugharamia ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa megawati 60 Nyakato
Mwanza. Serikali pia imesaini mkataba wa mkopo wa Dola za Marekani
milioni 350 kutoka Benki ya Credit Suisse ya Uingereza ambapo Dola za
Marekani milioni 200 zimepokelewa mwanzoni mwa Mwezi Juni 2012. Kiasi
kilichobaki cha Dola za Marekani milioni 150 kitapatikana na kutumika
mwaka 2012/13.
33. Mheshimiwa Spika, Serikali imepata Mshauri Mwelekezi ambaye
ataishauri Serikali katika zoezi la kujiandaa kufanyiwa tathmini ya
uwezo wa kukopa na kulipa madeni (Sovereign Credit Rating). Maandalizi
haya yataiwezesha nchi kufanyiwa tathmini yanatarajiwa kukamilika
mwanzoni mwa mwaka 2013. Kukamilika kwa zoezi hilo kutawapatia
wakopeshaji imani na hivyo kuiwezesha Serikali kupata mikopo yenye
masharti nafuu ya kibiashara kwa wakati.
Sera za Matumizi
34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali iliendelea
kutekeleza sera za matumizi kulingana na upatikanaji wa mapato ya
ndani, misaada pamoja na mikopo ya ndani na nje. Aidha, Serikali
iliendelea kuboresha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za
umma, ikijumuisha udhibiti wa ulipaji wa mishahara, matumizi katika
miradi ya maendeleo, ruzuku ya pembejeo, ununuzi wa umma na kuendelea
kudhibiti malimbikizo ya madeni. Serikali imeandaa mkakati wa kulipa na
kudhibiti madeni yatokanayo na malimbikizo ya madai ya watumishi;
wakandarasi; wazabuni; na madeni mengineyo. Madeni hayo yatalipwa baada
ya kuhakikiwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani.
Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma
35. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuimarisha usimamizi wa fedha
za umma, Serikali iliendelea kutekeleza programu ya maboresho ya
usimamizi wa fedha za umma katika Serikali Kuu na Serikali za mitaa.
Katika utekelezaji wa programu hiyo Serikali imeweka mtandao wa IFMS
katika Halmashauri 133. Aidha, Serikali imetoa mafunzo ya ulipaji kwa
mfumo wa malipo ya kibenki - TISS kwa watumishi wa kada ya Uhasibu
katika mikoa 20, Hazina ndogo zote, Ofisi ya Bunge, TAMISEMI na Ofisi
ya Mrajisi wa vyama vya Ushirika. Vilevile, Serikali imetoa mafunzo kwa
Wahasibu wa Wizara, Idara, Mikoa na Balozi zetu 32 katika kuandaa
Hesabu za Serikali kwa viwango vya Kimataifa (IPSAS – Accruals basis).
36. Mheshimiwa Spika, kutokana na maboresho hayo, usimamizi wa fedha
katika Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa
unaendelea kuimarika. Hali hii inajidhiirisha katika taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2010/11 ambapo
Hati safi za ukaguzi kwa Wizara, Idara na Sekretarieti za Mikoa
zimeongezeka kutoka asilimia 71 hadi asilimia 85. Wakati Hati zenye
shaka zimepungua kutoka asilimia 26 mwaka wa fedha 2009/10 hadi
asilimia 15 kwa mwaka wa fedha 2010/11 na hapakuwepo na Hati
zisizoridhisha ikilinganishwa na mwaka 2009/10 ambapo Hati hizo
zilitolewa kwa Taasisi mbili.
37. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Balozi zetu Hati safi zimeongezeka
kutoka asilimia 71 mwaka 2009/10 na kufikia asilimia 85 mwaka 2010/11
na hapakuwepo na Hati zisizoridhisha katika mwaka 2010/11. Aidha,
kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa Hati safi zimeongezeka kutoka
asilimia 49 mwaka wa fedha 2009/10 hadi asilimia 54 mwaka 2010/11 na
Hati zenye shaka zimepungua kutoka asilimia 64 mwaka 2009/10 na kufikia
asilimia 56 mwaka 2010/11.
38. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali imefungua akaunti
sita kwa kila Halmashauri kwa ajili ya uendeshaji wa majukumu yao.
Akaunti hizo ni za Mapato; Amana; Matumizi ya kawaida; Mishahara;
Maendeleo; na Mfuko wa Barabara. Lengo la hatua hii ni kupunguza
gharama za uendeshaji, urasimu wa matumizi, ugumu wa kutoa taarifa za
matumizi, ulimbikizaji wa fedha kwenye akaunti bila kutumika kwa muda
mrefu na kudhibiti fedha zisitumike katika shughuli ambazo
hazikuidhinishwa.
Mwenendo wa Matumizi
39. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, Serikali ilikadiria
kutumia kiasi cha shilingi bilioni 13,525.9 katika mwaka wa fedha wa
2011/12. Mgawanyo wa matumizi ya Serikali katika kipindi hiki ulikuwa
kama ifuatavyo; kiasi cha shilingi bilioni 8,600.3 zilitengwa kwa ajili
ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 4,925.6 zilikadiriwa
kutumika kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Matumizi ya kawaida
40. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012
matumizi ya kawaida yamefikia shilingi bilioni 7,349.8 sawa na asilimia
85.5 ya makadirio ya mwaka kama ilivyo katika ridhaa ya matumizi. Kati
ya kiasi hicho, malipo ya mishahara ya watumishi wa Serikali,
Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Taasisi na
Mashirika ya Umma yalikuwa shilingi bilioni 2,760.5 sawa na asilimia
84.4 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 3,270.3. Malipo ya riba kwa
mikopo ya ndani na nje yalikuwa shilingi bilioni 316.1 sawa na asilimia
102.4 ya makadirio ya shilingi bilioni 308.7 kwa mwaka. Malipo ya
mikopo ya nje yalikuwa shilingi bilioni 57.3 sawa na asilimia 85.7 ya
makadirio kwa mwaka. Serikali ilitumia shilingi bilioni 526 kwa ajili
ya kulipia dhamana za Serikali za muda mfupi na Hatifungani za Serikali
zilizoiva. Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika kulipa madeni
kwa wakati ili kuepuka malimbikizo ya riba.
41. Mheshimiwa Spika, matumizi mengineyo katika Wizara, Idara, Taasisi
za Serikali, Mikoa na Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 2,384.9
ikiwa ni asilimia 72.8 ya makadirio ya shilingi bilioni 3,275.1 kwa
mwaka. Kati ya matumizi mengineyo, kiasi cha shilingi bilioni 284.1
zilitumika kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ikiwa ni
asilimia 89 ya bajeti ya mwaka ya shilingi bilioni 317.4, na hivyo
kunufaisha jumla ya wanafunzi 93,176. Kadhalika, Serikali ililipa kiasi
cha shilingi bilioni 44.0 za madai ya walimu wa shule za msingi na
sekondari yaliyohakikiwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani.
Matumizi ya Maendeleo
42. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Matumizi ya Maendeleo kiasi cha
shilingi bilioni 2,657.2 ziligharamia miradi ya maendeleo
ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya kutumia shilingi bilioni
4,924.6. Fedha za ndani zilikuwa shilingi bilioni 1,201.6
ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 1,871.5 sawa
na asilimia 64.2. Upungufu huu umetokana na kuchelewa kupatikana kwa
wakati kwa mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara. Jumla ya
shilingi bilioni 663.8 ziligharamia miradi ya miundombinu, kati ya hizo
shilingi bilioni 296 zilitumika kwenye miradi ya umeme na shilingi
bilioni 367.8 kwenye miradi ya barabara. Matumizi ya maendeleo
yaliyogharamiwa kwa fedha za nje yalikuwa shilingi bilioni 1,450.4
ikilinganishwa na makadirio ya shilingi bilioni 3,054.1 sawa na
asilimia 47.
Vitambulisho vya Taifa na Anwani za Makazi
43. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na azma yake ya kutekeleza
mradi wa Vitambulisho vya Taifa ambavyo vitasaidia, pamoja na mambo
mengine, kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja
na huduma za kifedha. Mradi huu unaenda sambamba na uanzishwaji wa
anwani za makazi. Vitambulisho hivyo vitaanza kutolewa katika robo ya
kwanza ya mwaka 2012/13 kwa Zanzibar na Mkoa wa Dar es Salaam.
Sensa ya Watu na Makazi na Utafiti Kuhusu Hali ya Umaskini
44. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi
Serikali imeendelea kugharamia maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi,
ambapo utekelezaji umefikia asilimia 95. Hadi sasa Serikali imetumia
shilingi bilioni 23.6 kugharamia maandalizi ya zoezi la Sensa. Sensa
hiyo imepangwa kufanyika tarehe 26 Agosti 2012. Aidha, Serikali
iliendelea kugharamia utafiti wa mapato na matumizi katika kaya.
Utafiti huu ulianza mwezi Oktoba 2011, na unatarajiwa kukamilika mwezi
Septemba 2012 na matokeo yanatarajiwa kutoka mwezi Julai 2013. Utafiti
huu utatoa picha halisi ya hali ya umaskini, hususan wa kipato tangu
mwaka 2007 hadi mwaka 2012. Hii itasaidia kutambua mwenendo wa umaskini
wa kipato na sababu zilizopelekea mwenendo huo.
Utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II)
45. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/12, serikali
iliendelea kutekeleza MKUKUTA awamu ya pili unaojielekeza katika maeneo
ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato, kuboresha maisha na
ustawi wa jamii, na utawala bora na uwajibikaji sambamba na Melengo ya
Maendeleo ya Milenia. Ili kufikia matokeo tarajiwa katika kila eneo,
sekta kadhaa huchangia katika utekelezaji kupitia sera, mikakati na
mipango ya kisekta. Kwa mantiki hiyo, utekelezaji wa MKUKUTA II
unahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali za uchumi katika hatua ya
upangaji na utekelezaji.
46. Mheshimiwa Spika, MKUKUTA ni mkakati unaoziweka pamoja juhudi za
Serikali na wadau mbalimbali katika kupambana na umaskini. Aidha,
umaskini ni suala pana linalojumuisha umaskini wa kipato na usio wa
kipato. Ni kweli kuwa umaskini wa kipato umekuwa ukipungua kwa kasi
ndogo. Hata hivyo, Serikali inachukua hatua mbalimbali za kupunguza
umaskini kwa kujenga mazingira bora ili wananchi washiriki kikamilifu
katika shughuli za uchumi, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika elimu,
afya, miundombinu na sekta ya fedha.
47. Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto zilizojitokeza, hususan
mtikisiko wa uchumi duniani, uchumi uliendelea kukua kwa kiwango cha
kuridhisha. Kiwango cha ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2011, kilikuwa
asilimia 6.4 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2010. Aidha, pato la
wastani la Mtanzania limeongezeka kutoka shilingi 770,464 kwa mwaka
2010 hadi shilingi 869,436 kwa mwaka 2011. Kwa wastani, ongezeko hili
limeongeza uwezo wa wananchi kupata huduma bora ikiwa ni pamoja na
nyumba bora, simu za mkononi, pikipiki na usafiri wa baiskeli.
48. Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutekeleza programu
mbalimbali za huduma ya jamii kwa lengo la kuboresha maisha na ustawi
wa jamii. Matokeo ya utekelezaji wa programu hizo zinaonesha mabadiliko
chanya. Katika sekta ya elimu, viwango vya uandikishaji na kumaliza
katika ngazi zote za elimu vinaridhisha. Mfano, kiwango cha
uandikishwaji katika elimu ya msingi, kilikuwa asilimia 94 na katika
elimu ya sekondari ni asilimia 35 kwa mwaka 2011. Huduma za afya kwa
mtoto na mama zinaendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa mpango
wa afya ya mtoto na mama. Aidha, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji
safi na salama imeendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa programu
ya sekta ya maji iliyoanza mwaka 2007.
49. Mheshimiwa Spika, katika kudumisha utawala bora na uwajibikaji,
Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na:
kuimarisha sekta ya sheria kwa kuongeza idadi ya mahakimu wa Mahakama
za mwanzo; kuimarisha mfumo wa sheria na haki za binadamu; kuhamasisha
umma kuhusu haki za binadamu na wajibu wa jamii; na kushiriki katika
mpango wa nchi za Afrika kujitathmini zenyewe katika masuala ya utawala
bora. Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa
fedha za umma, kwa kuimarisha ofisi za ukaguzi katika wizara, mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Sekta ya Fedha
50. Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya mageuzi mbalimbali katika sekta
ya fedha ili kuhakikisha kwamba inachangia kikamilifu katika shughuli
za kiuchumi na kukuza Pato la Taifa. Mageuzi haya yameleta mafanikio
makubwa.Hadi kufika mwezi Aprili mwaka 2012 idadi ya benki imeongezeka
na kufikia 49 kutoka benki 43 Aprili mwaka 2011. Kadi za simu za
mkononi zinazotumika kutoa huduma za kifedha zimefikia 21,184,808 mwaka
2011 kutoka 10,663,623 mwaka 2010. Aidha, idadi ya Taasisi ndogo ndogo
za kifedha zimefikia 150 mwaka 2011.
51. Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutoa Mikopo ya kilimo
kupitia dirisha la Kilimo lililopo katika Benki ya Rasilimali Tanzania.
Hadi kufikia Machi, 2012 jumla ya mikopo 81 yenye thamani ya shilingi
bilioni 22.9 ilitolewa, kati ya mikopo hiyo, 42 ni ya SACCOS, 32 ni kwa
ajili ya makampuni na 7 kwa Taasisi ndogondogo za fedha (MFIs). Mikopo
iliyotolewa kwa MFIs na SACCOS ilitumika kukopesha miradi mingi ya
wakulima wadogo wadogo vijijini. Aidha, Serikali imetoa shilingi
bilioni 30 kwa ajili ya mtaji wa Benki ya Kilimo.
52. Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea na utekelezaji wa programu ya
mageuzi na maboresho ya Ushirika nchini ili kuimarisha vyama vikuu vya
ushirika na kuviwezesha kutoa huduma za kifedha kwa wananchi wengi
zaidi hususan waliopo vijijini. Mwaka 2011, idadi ya Vyama vya Ushirika
wa Akiba na Mikopo (SACCOS) iliongezeka na kufikia 5,346 kutoka vyama
5,314 mwaka 2010. Vile vile, idadi ya wanachama iliongezeka kwa
asilimia 5.7 na kufikia wanachama 970,655 kutoka wanachama 917,889
mwaka 2010. Aidha, Hisa, Akiba na Amana za wanachama ziliongezeka
kutoka shilingi bilioni 236.8 mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 399.0
mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 68.5. Mikopo iliyotolewa kwa
wanachama iliongezeka kutoka shilingi bilioni 539.2 mwaka 2010 hadi
shilingi bilioni 627.2 mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 16.3.
53. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi 2012, mikopo kwa sekta binafsi
iliongezeka kwa asilimia 21.9 ikilinganishwa na asilimia 23.3 Machi
2011. Ongezeko hili linaenda sambamba na kuongezeka kwa rasilimali za
fedha za ndani kwenye benki pamoja na kupungua kwa ukuaji wa rasilimali
za fedha za kigeni kwenye benki. Sehemu kubwa ya mikopo hii ilielekezwa
katika shughuli binafsi asilimia 21.9; biashara asilimia 19.9;
uzalishaji bidhaa viwandani asilimia 11.9; kilimo asilimia 11.8; na
usafiri na mawasiliano asilimia 7.9.
54. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza upatikanaji wa mikopo, Serikali
imepata Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya kuanzisha taasisi ya kuratibu
taarifa za wakopaji (Credit Rerefence Bureau) na mfumo wa kuhifadhi
taarifa za wakopaji (Credit Reference Databank). Mshauri mwelekezi
ameanza zoezi la kuweka mitambo na kutoa mafunzo kwa watumiaji. Aidha,
Serikali imeboresha mazingira ya upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu na
kati kwa ajili ya nyumba, Kilimo na uwekezaji ambapo kanuni za taasisi
za fedha za maendeleo ziliandaliwa na kuchapishwa katika Gazeti la
Serikali la Machi 2012.
55. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali imeendelea kufanya
maboresho katika sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa kufanya tathmini ya
uwekezaji wa mifuko, uhai wa mifuko, pamoja na kuandaa mwongozo za
uwekezaji wa mifuko hiyo. Aidha, Serikali imefanya marekebisho ya
Sheria za Mifuko yote pamoja na Mamlaka ya Usimamiaji wa Shughuli za
Mifuko (SSRA) ili kuboresha usimamizi wa mifuko hiyo.
Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi
56. Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu lilipitisha sheria mpya ya Ubia
kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ya mwaka 2010 ili kutoa fursa
kwa sekta binafsi kushiriki katika ujenzi wa miundombinu na kuiendesha
kwa lengo la kutoa huduma bora za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.
Katika mwaka 2011/12, Serikali imefanya maandalizi ya utekelezaji wa
Sera ya Ubia ikiwa ni pamoja na kuanzisha madawati ya PPP kwa kila
Wizara na kuandaa miongozo itakayotumika kuchambua na kuidhinisha
miradi ya Ubia kwa mujibu wa sheria. Aidha, Serikali imeanza hatua za
awali kubaini miradi inayoweza kutekelezwa kwa utaratibu wa Ubia kwa
mujibu wa sheria.
57. Mheshimiwa Spika, dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta
Binafsi inatekelezwa kwa kutumia sheria mbili – Sheria ya Ubia ya mwaka
2010 na Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 iliyorekebishwa mwaka
2011. Sababu za kurekebisha Sheria ya Ununuzi wa Umma pamoja na mambo
mengine ni kuingiza vifungu vinavyowezesha Taasisi za Serikali kupata
Wabia makini wa uwekezaji katika miradi ya Umma kwa njia zilizo wazi.
Aidha, katika mwaka 2012/13, Serikali itakamilisha Kanuni za Sheria ya
Ununuzi wa Umma ambazo zinazingatia mazingira ya kipekee ya Sheria ya
Ubia ambayo inawezesha kupata Wabia walio tayari kuwekeza katika miradi
husika. Serikali itahakikisha kanuni na taratibu zote za kuidhinisha na
kusimamia miradi ya ubia zinazingatiwa.
58. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Serikali itatoa
mafunzo ya uelewa wa dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta
binafsi kwa watumishi wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi za
Serikali, na Halmashauri zote. Aidha, Serikali itachagua miradi
michache ya kuanza nayo ili kupata uzoefu wa uendeshaji wa miradi hiyo.
Maeneo tunayotarajia kuanza nayo ni barabara, reli, bandari, viwanja
vya ndege, maji pamoja na ujenzi wa ofisi.
59. Mheshimiwa Spika, Napenda kutumia fursa hii kuziomba Wizara, Idara
zinazojitegemea, Mashirika ya Umma, na Mamlaka ya Serikali za Mitaa
kuhamasisha Sekta Binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi
mbalimbali kwa kuzingatia taratibu na kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa
Sheria.
Usimamizi wa Deni la Taifa
60. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma yake ya kuboresha
miundombinu ya kimkakati, Serikali imeendelea kukopa kutoka nje na
ndani ya nchi ili kugharamia miradi mbali mbali ya maendeleo. Hadi
mwishoni mwa Machi 2012, deni la taifa lilikuwa shilingi bilioni
20,276.6 ikilinganishwa na deni la shilingi bilioni 17,578.9 Machi 2011
ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 15.4. Kati ya hizo, shilingi
bilioni 15.306.9 zilikuwa ni deni la nje na shilingi bilioni 4,969.7 ni
deni la ndani. Kati ya kiasi cha deni la nje, shilingi bilioni 12,342.5
zilikuwa ni deni la umma na kiasi kilichobaki cha shilingi bilioni
2,964.4 ni deni la sekta binafsi. Aidha, hadi kufikia Machi 2012, deni
la ndani la Serikali lilifikia shilingi bilioni 4,969.7 ikilinganishwa
na shilingi bilioni 4,496.5 mwezi Machi, 2011, sawa na ongezeko la
asilimia 10.5. Sababu kubwa ya kuongezeka kwa deni la taifa ni mikopo
mipya kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo na utumiaji wa
dhamana za muda mfupi za Serikali kwa ajili ya kudhibiti mfumuko wa bei
katika uchumi na kushuka kwa thamani ya shilingi kuliongeza deni la nje.
61. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Deni la Taifa
linasimamiwa vizuri, mwezi Februari, 2012, Serikali ilifanya tathmini
ya uhimilivu wa deni (Debt Sustainability Analysis) likijumuisha
dhamana zinazotolewa na Serikali kwa Wizara, Mashirika na Taasisi za
Umma ambapo matokeo ya tathmini hiyo yanaonesha kuwa Deni la Taifa
linahimilika.
Usimamizi wa Mashirika ya Umma
62. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Taasisi, Wakala na Mashirika
ya umma yanatekeleza majukumu yao, Serikali imetoa Waraka Na.1 wa mwaka
2012 unaoelekeza Wizara mama na Bodi za Wakurugenzi kuingia katika
mikataba ya utendaji, Waraka huo umeanza kutumika Januari, 2012. Aidha,
ukaguzi wa kiutendaji (Management Audit) katika Taasisi za Serikali
umefanyika kwa baadhi ya Taasisi na Mashirika ya umma kwa kuangalia
uzingatiaji wa kanuni, Sheria na miongozo mbalimbali inayotolewa na
Serikali ikiwa ni pamoja na uwajibikaji na utawala bora, matumizi ya
fedha na taratibu za ajira. Zoezi hili ni endelevu na linalenga
kuboresha uendeshaji wa Mashirika na Taasisi za Serikali. Kadhalika,
Serikali imefanya uhakiki wa mashirika 170 yaliyobinafsishwa. Kati ya
hayo, mashirika 41 yalikutwa yanajiendesha kwa faida, mashirika 66
yanajiendesha kwa hasara na mashirika 63 yalikuwa muflisi. Kwa yale
ambayo yanaendeshwa kwa hasara yatawekwa chini ya mfilisi kwa lengo la
kuyachambua na kupendekeza hatua za kuchuliwa. Aidha, kwa yale
yaliyokuwa muflisi hatua za kuyafilisi zinaendelea.
III. BAJETI YA MWAKA 2012/13
63. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2012/13 itazingatia vipaumbele
vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13; Awamu ya
Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II);
Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka
2010 na program za maboresho katika sekta ya umma. Lengo likiwa ni
kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
64. Mheshimiwa Spika, pamoja na miongozo hiyo, Bajeti hii inazingatia
pia changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka
2011/12. Changamoto hizo ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika;
kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la Dunia; uhaba wa chakula katika
baadhi ya maeneo; kupanda kwa bei za bidhaa na huduma; kutopatikana kwa
wakati fedha za kugharamia miradi ya maendeleo kulikosababishwa na
masharti magumu na urasimu kwa mikopo ya kibiashara; na kuongezeka kwa
malimbikizo ya madeni ya ndani, hususan ya wazabuni, wakandarasi na
watumishi. Mambo mengine yaliyozingatiwa ni pamoja na mwenendo wa
uchumi wa dunia na makubaliano ya kikanda na kimataifa. Serikali
imepanga hatua mbalimbali za kuchukua kukabiliana na changamoto hizo
kama nitakavyoeleza hapo baadae.
Shabaha na Malengo ya Bajeti ya mwaka 2012/13
65. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2012/13, imejielekeza katika kufikia Shabaha na malengo yafuatayo:
i. Kukuza Pato halisi la Taifa kwa asilimia 6.8 mwaka 2012 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.4 mwaka 2011;
ii. Kuimarisha miundombinu ya uchumi, ikijumuisha umeme, barabara, reli na bandari;
iii. Kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha;
iv. Kuongezeka kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano na Pato la
Taifa wa asilimia 18 kwa mwaka 2012/13 kulinganisha na mwelekeo wa
asilimia 16.9 mwaka 2011/12;
v. Kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei ili urudi kwenye viwango vya tarakimu moja;
vi. Kuwa na kiwango tengemavu cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha;
vii. Kukua kwa mikopo kwa sekta binafsi kwa kiwango cha asilimia 20 ya
Pato la Taifa mwishoni mwa Juni 2013 sambamba na jitihada za kudhibiti
mfumuko wa bei;
viii. Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji
ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua
miezi minne na nusu;
ix. Kuimarisha utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP)
ili kupanua fursa za kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo;
x. Kuboresha mazingira ya wafanya biashara wadogo na wakati;
xi. Kulinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika Sekta za huduma za jamii;
xii. Kuimarisha utawala bora na uwajibikaji; na
xiii. Kujenga uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi na
kifedha pamoja na kushiriki kwa ufanisi katika ushirikiano kikanda na
kimataifa.
Misingi ya Bajeti ya Serikali kwa Kipindi cha mwaka 2012/13
66. Mheshimiwa Spika; ili kufikia malengo yaliyoainishwa hapo juu,
misingi ya Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2012/13 ni hii
ifuatayo:
i. Kuendelea kuimarika kwa utengamavu wa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii;
ii. Kuwepo kwa nishati ya umeme wa uhakika na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia;
iii. Kuimarika kwa utekelezaji wa Sera za Fedha na Bajeti;
iv. Kuendelea kuimarika kwa mahusiano na Washirika wa Maendeleo;
v. Kuendelea kutekeleza sera ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi;
vi. Kuendelea kutekeleza maboresho katika sekta ya umma ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma;na
vii. Kuendelea kuboresha mazingira ya biashara pamoja na kuongezeka kwa tija na fursa za uwekezaji.
Sera za Mapato
67. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na azma yake ya kuimarisha
ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali katika
maeneo ya mapato yatokanayo na kodi na yasiyotokana na kodi; na kupanua
wigo wa makusanyo. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha taratibu za
kukusanya mapato pamoja na kupunguza misamaha ya kodi ili kuweza
kugharamia kwa kiwango kikubwa matumizi ya kawaida kwa kutumia mapato
ya ndani. Sera za mapato zitakazozingatiwa kwenye Bajeti ya mwaka
2012/13 ni pamoja na;
i. kuboresha mifumo ya ukusanyaji na usimamiaji wa mapato yasiyo ya
kodi kwa kupitia upya mfumo wa utoaji stakabadhi na leseni, pamoja na
kuboresha viwango vya kubakiza maduhuli kwa Wizara, Idara na Taasisi za
Serikali;
ii. kupanua wigo wa kodi kwa kuendelea kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iingie kwenye mfumo wa kodi;
iii. kuendelea kufanya mapitio ya sheria za Wakala/Taasisi za Umma
zinazokusanya maduhuli ili ziweze kuchangia zaidi kwenye Mfuko Mkuu wa
Serikali;
iv. kuendelea kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazotoa misamaha
ya kodi kwa lengo la kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo;
v. Kupitia upya mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya majengo katika majiji,
manispaa, miji, wilaya na miji midogo ili kuuboresha zaidi;
vi. kufanya mapitio ya vyanzo vya mapato na mfumo wa ukusanyaji katika Serikali za Mitaa ili kuongeza mapato; na
vii. Kujenga uwezo wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini,
Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania,
Wakala wa Ukaguzi wa Madini ili kusimamia ukusanyaji wa mapato katika
maeneo ya madini, gesi na petroli.
Hatua za Kuboresha Uzalishaji na Huduma
68. Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea mapendekezo kutoka kwa wadau
mbalimbali wakiwemo waheshimiwa wabunge kuhusu haja ya kuboresha
mazingira ya uzalishaji katika sekta za Uvuvi, Viwanda, Kilimo, Mifugo
na Utalii. Hatua ambazo Serikali imepanga kuchukuwa ni pamoja na:
i. Kupitia upya vivutio kwa sekta ya viwanda vya ndani vinavyotumia
malighafi za ndani vikiwemo viwanda vya nguo na mafuta ya kula;
ii. Kutafuta utaratibu mzuri wa kubainisha vipuri vya mashine na
mitambo inayosamehewa kodi ili kuondoa usumbufu wanaoupata waagizaji;
iii. Kupitia upya viwango vya kodi katika sekta ya Kilimo na Uvuvi kwa lengo la kuviwianisha na kupunguzwa;
iv. Kupitia upya maudhui na viwango vya Tozo ya Kuendeleza Stadi
(Skills Development Levy) na Leseni ya Magari (Motor Vehicle Licence).
Kwa kufanya hivyo, Serikali inalenga katika kupanua wigo wa kodi,
kuwapunguzia mzigo waajiri na kupanua ajira hapa nchini. Aidha, mapitio
ya Leseni za Magari yatazingatia kurejea madhumuni ya kuanzishwa kwa
leseni hiyo; na
v. Kufanya mapitio ya Sheria ya VAT kwa lengo la kuibadili kwa kuzingatia uzoefu wa kimataifa “Best Practice”.
69. Mheshimiwa Spika, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinahimizwa kuongeza
ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuzingatia fursa zilizopo. Aidha, OWM
– TAMISEMI kwa kushirikiana na Shirika la Misaada na Utaalamu la
Ujerumani – GIZ watakamilisha na kusambaza kwenye Halmashauri mfumo wa
kompyuta wa utunzaji kumbukumbu za mali na majengo (Integrated Property
Rating Information Management System - IPRIMS) ili kuboresha ukusanyaji
wa mapato hususan kodi ya majengo. Natoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge
wote pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali kuweka msukumo
utakaowezesha Halmashauri kukusanya kikamilifu kodi ya majengo pamoja
na mapato mengine ili kuziongezea uwezo wa kuhudumia wananchi na
kuwaletea maendeleo endelevu.
70. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za mapato zilizoainishwa hapo
juu, Serikali inalenga kukusanya mapato ya ndani (bila kujumuisha
Halmashauri) shilingi bilioni 8,714.7 sawa na asilimia 18 ya Pato la
Taifa. Kati ya kiwango hicho, mapato ya kodi shilingi bilioni 7,080.1
na mapato yasiyo ya kodi shilingi bilioni 644.6. Mapato yanayotokana na
vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 362.2 sawa na asilimia 0.7 ya
Pato la Taifa.
Mikopo ya Ndani
71. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na utaratibu wake wa kukopa
katika soko la ndani la fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya
maendeleo na kulipia hatifungani za Serikali na dhamana za Serikali za
muda mfupi zinazoiva. Katika mwaka 2012/13, Serikali inakusudia kukopa
kiasi cha shilingi bilioni 1,632 kutoka soko la fedha la ndani. Kati ya
kiasi hicho, shilingi bilioni 483.9 sawa na asilimia moja ya Pato la
Taifa ni kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo na kiasi cha
shilingi bilioni 1,148.1 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani za
Serikali na dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva. Kiwango hiki
kimezingatia viashiria vya kiuchumi pamoja na kuhakikisha kuwa Taasisi
za Fedha zinaendelea kutoa mikopo kwa Sekta binafsi ili kuchochea
ukuaji wa uchumi.
Misaada na Mikopo Mipya yenye Masharti Nafuu
72. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na Washirika wa
Maendeleo ili kuhakikisha Misaada na mikopo inapatikana kwa wakati na
kuchangia katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali. Katika bajeti ya
mwaka 2012/13 serikali inatarajia kupata kiasi cha shilingi bilioni
3,156.7 kutokana na misaada na mikopo yenye masharti nafuu. Kati ya
fedha hizo, Misaada na mikopo ya kibajeti ni shilingi bilioni 842, sawa
na Dola za Marekani milioni 495. Misaada na mikopo kwa ajili ya miradi
ya maendeleo ikijumuisha mifuko ya kisekta inatarajiwa kuwa shilingi
bilioni 2,314.2.
73. Mheshimiwa Spika, pamoja na misukosuko ya kiuchumi na majanga ya
kiasili iliyozikumba nchi Wahisani, bado zimeendelea kutoa misaada na
mikopo kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Napenda kuwatambua
washirika wetu wa maendeleo ambao ni: Uingereza, Norway, Canada,
Marekani, Uholanzi, Ubelgiji, China, Finland, Ufaransa, Ujerumani,
Ireland, Japani, Korea ya Kusini, Denmark, Hispania, Sweden, Uswisi,
India, Italia, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Umoja wa
Ulaya, Global Funds, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), BADEA, Kuwait
Fund, Nordic Fund, Opec Fund, Saudi Fund, na Mashirika ya Umoja wa
Mataifa. Tunawashukuru Sana.
Mikopo ya nje yenye Masharti ya Kibiashara
74. Mheshimiwa Spika, sera ya Serikali ni kutafuta mikopo nafuu kutoka
mashirika na nchi wahisani kwa ajili ya kugharamia Bajeti yake ya
maendeleo. Hata hivyo, kwa kuzingaita mahitaji makubwa ya kuendeleza
miradi ya miundombinu kwa mwaka 2012/13, Serikali inatarajia kupata
kutoka nje mikopo yenye masharti ya kibiashara kiasi cha shilingi
bilioni 1,254.1 sawa na Dola za Marekani milioni 749. Fedha hizi
zitatumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama
ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13 ikijumuisha
mchango wa Serikali (counterpart fund) katika ujenzi wa bomba la gesi
kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, mradi wa maji wa Ruvu chini na ujenzi
wa barabara. Uamuzi wa kuendelea kukopa kwa masharti nafuu na ya
kibiashara unazingatia uhimilivu wa Deni la Taifa uliopo.
Sera za Matumizi
75. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, sera za matumizi zitazingatia yafuatayo:
i. Matumizi yataendelea kuzingatia mapato halisi yanayopatikana;
ii. Nakisi ya bajeti haitazidi asilimia 5.5 ya Pato la Taifa, ikijumuisha ruzuku;
iii. Mafungu yataendea kuzingatia viwango vya matumizi vitakavyoidhinishwa na Bunge;
iv. Maafisa Masuuli wataendelea kuzingatia Sheria ya Fedha na ya Ununuzi wa Umma; na
v. Serikali inaendelea kukusanya madeni yote kwa lengo la kuyahakiki na kuyapangia utaratibu wa kuyalipa.
Matumizi ya Kawaida
76. Mheshimiwa Spika, Sera za matumizi ya kawaida kwa mwaka 2012/13
zinalenga pamoja na mambo mengine katika kugharamia mishahara; madeni
ya mikopo ya ndani na nje; uboreshaji wa huduma za kiuchumi na
maendeleo ya jamii; mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; mitihani ya
shule za msingi na sekondari; ununuzi na usambazaji wa dawa; mahitaji
ya Tume ya Kuratibu Mabadiliko ya Katiba; matengenezo ya mali ya
Serikali; ununuzi wa chakula cha hifadhi; mahitaji ya kawaida kwenye
miradi iliyokamilika; pamoja na kuendelea kulipa madai mbalimbali ya
watumishi na wazabuni.
77. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa
mikopo ya muda mrefu, kilimo kisichokuwa na tija na ukosefu wa ajira,
Serikali imetenga fedha katika maeneo yafuatayo: Shilingi bilioni 30
kwa ajili ya Benki ya Rasilimali; shilingi bilioni 40 kwa Benki ya
Maendeleo ya Kilimo na hivyo kufikisha mtaji wa shilingi bilioni 100.
Aidha, shilingi bilioni 7.5 zimetengwa kwa ajili ya kurejesha mafunzo
ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, ambapo katika awamu ya
kwanza vijana 5,000 wanatarajiwa kujiunga. Vilevile, Serikali imetenga
jumla ya shilingi bilioni 70.7 katika maeneo mapya ikiwa ni Mikoa,
Wilaya na Halmashauri kugharamia matumizi ya kawaida na maendeleo.
Matumizi ya Maendeleo
78. Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2011 na
Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/13, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Mahusiano na Uratibu Mhe. Stephen Masatu Wasira, aliainisha
miradi ya kitaifa ya kimkakati pamoja na miradi katika maeneo muhimu ya
ukuaji wa uchumi. Bajeti hii itazingatia vipaumbele hivyo:
a) Miundombinu
i. umeme - mkazo utawekwa katika upatikanaji wa umeme wa kuhakika kwa
kuongeza uzalishaji, usafirishaji na usambazaji ambapo jumla shilingi
bilioni 498.9 zimetengwa kwa ajili hiyo. Aidha, Serikali itatekeleza
mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa
mkopo kutoka Benki ya Exim ya China wenye thamani ya Dola za Marekani
milioni 1,225.3 utakaosimamiwa na TPDC.
ii. usafirishaji na uchukuzi – uimarishaji wa reli ya kati ikijumuisha
ukarabati wa injini na mabehewa ya treni. Kwa upande wa barabara,
miradi inayopewa kipaumbele ni pamoja na barabara zenye kufungua fursa
za kiuchumi. Katika usafiri wa anga na majini, miradi itakayotekelezwa
ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege na uendelezaji wa
gati ya Ziwa Tanganyika. Jumla ya shilingi bilioni 1,382.9 zimetengwa
katika eneo hili.
iii maji safi na salama - kuongeza upatikanaji wa
maji safi na salama mijini na vijijini. Kiasi cha shilingi bilioni 568.8 kimetengwa.
iv Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
– kuimarisha mawasiliano kwa kutumia TEHAMA ili kuboresha upatikanaji
wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa taarifa za
masoko ya ndani na nje ya nchi; ukusanyaji wa mapato; huduma za afya;
elimu; huduma za kifedha; n.k. Jumla ya shilingi bilioni 4 zimetengwa
katika eneo hili.
b) Kilimo, Uvuvi na Ufugaji
79. Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na sekta binafsi, Serikali
itawekeza katika kilimo cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya
Wami, Ruvu, Kilombero na Malagarasi pamoja na kuongeza tija na thamani,
kubadilisha mfumo wa kilimo na kukuza kilimo cha misitu. Hii ni pamoja
na kuendeleza shughuli za ufugaji na uvuvi ili ziwe na tija kwa
kuboresha mazingira ya uwekezaji; kwa kufanya hivyo kutapunguza
umaskini wa kipato.
80. Mheshimiwa Spika, katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula
pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula, Serikali itaimarisha
utekelezaji wa dhana ya Kilimo Kwanza kwa kuhakikisha kwamba nguzo zake
zote zinaendelea kuzingatiwa; kuhakikisha kwamba walengwa wanapata
pembejeo kwa wakati; Maafisa ugani kutakiwa kuwa na mashamba yao ya
mfano (mashamba darasa) ili kuwaelimisha wakulima kilimo cha kisasa;
kuongeza msukumo kwenye kilimo cha umwagiliaji ili wakulima waweze
kufanya shughuli zao za kilimo katika misimu yote badala ya kutegemea
mvua;Kuimarisha masoko ya mazao kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko
ambayo imeshaanza shughuli zake; na Mikoa kutakiwa kuendelea kutenga
ardhi na vijiji kutakiwa kupima na kurasimisha ardhi kwa ajili ya
wawekezaji wa ndani na wa nje. Kiasi cha shilingi bilioni 192.2
kimetengwa katika eneo hili.
c) Maendeleo ya Viwanda
81. Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kuendeleza viwanda
vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini; viwanda vinavyoongeza
thamani ya madini; viwanda vikubwa vya saruji; na viwanda vya
eletroniki na TEHAMA pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na
kutenga maeneo maalum ya uwekezaji mijini na vijijini na kukuza ubia
kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. Hatua hii inaenda sambamba na
kuboresha na kuimarisha viwanda vidogo vidogo nchini. Jumla ya shilingi
bilioni 128.4 zimetengwa katika eneo hili.
d) Maendeleo ya Rasilimali Watu na Huduma za Jamii
82. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Serikali imepanga
kuboresha viwango vya elimu katika ngazi zote hususan katika maeneo ya
utafiti, ufundi stadi, afya; sayansi na ujuzi maalum kuhusu madini,
gesi, urani, chuma na mafuta; hatua hii inajumuisha ukarabati wa
maabara na upatikanaji wa vifaa vya maabara. Shilingi bilioni 84.1
zimetengwa katika eneo hili.
e) Utalii
83. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha huduma zitolewazo
katika eneo hili ikiwa ni pamoja na kutangaza utalii na kuboresha
mazingira ya kitalii na kutoa mafunzo ya utalii, kuainisha maeneo mapya
ya utalii na kuboresha vyuo vya utalii.
Huduma za Fedha
84. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za kifedha
hususan mifumo ya kuweka akiba na kukopa kama vile SACCOS, VICOBA na
benki za kijamii ili kuwawezesha wananchi kupata mitaji kwa ajili ya
biashara na uzalishaji. Kiasi cha shilingi bilioni 2.6 zimetengwa kwa
ajili ya kuimarisha mtaji wa Benki ya Wanawake, Mradi wa SELF na Mfuko
wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Aidha, Wizara ya Fedha itaendelea
kusimamia maendeleo ya Taasisi za fedha zinazojihusisha na utoaji wa
mikopo kwa wajasiriamali. Ili kufanikisha hili kitengo kilichopo cha
maendeleo ya sekta ya fedha kitahuishwa na kuwa idara kamili.
Usimamizi wa Fedha za Umma
85. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza awamu ya nne ya
Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma na kuhakikisha
kwamba Sheria ya Fedha za Umma na Sheria ya Ununuzi wa Umma zinafuatwa
kikamilifu ili kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za Umma.
Maeneo yanayozingatiwa kwenye programu hiyo ni pamoja na: kuendelea
kuboresha Mtandao wa malipo (IFMS) ili kuimarisha udhibiti wa matumizi
ya fedha za Umma kwa Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
utoaji wa mafunzo ya ulipaji kwa mfumo wa malipo wa kibenki kwa
watumishi wa Ofisi za Bunge, Sekretarieti za Mikoa, Idara ya Ushirika,
Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI na Ofisi za Hazina ndogo Mikoa yote.
Aidha, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya kuandaa hesabu kwa kutumia
viwango vya uhasibu vya kimataifa ili kuongeza uwazi katika matumizi ya
fedha za Umma; kuijengea uwezo Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa
Serikali katika kuhakikisha kanuni na taratibu za matumizi ya fedha za
umma zinazingatiwa ipasavyo; na kujenga uwezo wa Serikali Kuu, Mikoa na
Halmashauri katika eneo la uandaaji wa mipango na bajeti, ukusanyaji wa
mapato, usimamizi wa raslimali, uboreshaji wa mawasiliano na utoaji wa
taarifa za utekelezaji wa bajeti.
86. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha utaratibu wa
kupeleka fedha kwenye Halmashauri na kutoa taarifa mapema kuhusu
matumizi ya fedha zilizopelekwa. Aidha, fedha zote zitakazovuka mwaka
bila kutumika zitatolewa taarifa kwenye vikao vya Kamati za Kudumu na
Baraza la Madiwani ili kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa umma.
87. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Serikali itaendelea na
zoezi la uhakiki wa watumishi kwenye Wizara, Idara, Sekretarieti za
Mikoa na Halmashauri zote ili kuondoa watumishi wasiostahili kwenye
orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa Serikali. Aidha, mamlaka
za ajira na maafisa masuuli wanaelekezwa kusitisha malipo kwa watumishi
walioacha au kuachishwa kazi, kustaafu, kufariki au likizo bila malipo
ili kuzuia upotevu wa fedha za umma.
88. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutilia mkazo wa ukaguzi wa
mapato na matumizi ya fedha za umma katika Wizara, Taasisi, Wakala,
Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuthibitisha endapo fedha
zinazopangwa kukusanywa zinapatikana na pia fedha zinazotumwa kutoka
Hazina zinafika na kutekeleza shughuli zilizoidhinishwa. Serikali
itaboresha mifumo ya udhibiti na usimamizi wa fedha za umma
zinazokusanywa au kupelekwa kwenye Mikoa na Halmashauri nchini.
Usimamizi wa Mashirika ya Umma
89. Mheshimiwa Spika, katika kukabliana na changamoto za usimamizi wa
Mashirika ya Umma, Serikali inaendelea kuimarisha Ofisi ya Msajili wa
Hazina kwa kufanya mapitio ya Sheria za Msajili wa Hazina ambazo ni
“Treasury Registrar Ordinance” ya mwaka 1958 na “Treasury Registrar
Powers and Functions” SURA 370 ya mwaka 2000 kama ilivyorekebishwa
mwaka 2010 ili kuwa na Sheria moja. Lengo la hatua hiyo ni kuimarisha
ofisi kwa kuipa nguvu zaidi za kisheria kuweza kusimamia ipasavyo
utendaji wa Mashirika ya Umma pamoja na Taasisi ili kuongeza tija.
Kukabiliana na Mfumuko wa Bei
90. Mheshimiwa Spika, uchumi wetu unakabiliana na changamoto nyingi
ikiwemo mfumuko wa bei ambao kwa wastani umeshuka kutoka asilimia 19.8
mwezi Desemba 2011 hadi asilimia 18.7 mwezi Aprili 2012. Kichocheo
kikubwa cha mfumuko wa bei ni kupanda kwa bei za umeme, mafuta na
vyakula hususan mchele na sukari. Kwa mfano kwa mwezi Aprili 2012,
chakula kimechangia asilimia 24.7 wakati umeme na mafuta vimechangia
kwa asilimia 24.9. Mfumuko wa bei ambao haujumuishi chakula na nishati
bado uko kwenye tarakimu moja ambayo ni asilimia 8.8. Hivyo, jitihada
za Serikali zitaelekezwa katika kukabiliana na kupanda kwa bei ya
bidhaa hizo.
91. Mheshimiwa Spika, hatua za haraka ambazo Serikali itachukua ni
pamoja na kutoa vibali vya uagizaji wa sukari na mchele kutoka nje na
kuendelea kuimarisha Hifadhi ya Chakula ya Taifa. Aidha, Serikali
itawekeza katika kilimo cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya
Kilombero, Wami, Kagera na Malagarasi pamoja na miradi ya kilimo cha
umwagiliaji. Hatua nyingine ni pamoja na kuendelea kuimarisha
miundombinu ya usafirishaji na masoko; kuimarisha mfumo wa masoko
kwenye maeneo yanayozalisha chakula kwa wingi hususan mikoa ya nyanda
za juu kusini na mipakani. Kwa upande wa nishati ya umeme, Serikali
itaendeleza vyanzo mbadala vya umeme kama vile umeme wa gesi, nguvu za
jua, upepo, miwa ili kupunguza matumizi ya mafuta kama chanzo cha
nishati.
Kupanua fursa za Ajira
92. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ajira hasa kwa vijana, Serikali
itaendelea kupanua huduma za fedha ikiwa ni pamoja na kuanzisha Benki
ya Kilimo na kuongeza mitaji kwa Benki za Rasilimali, Wanawake, Posta
na Twiga Bancorp. Hatua nyingine zitakazochukuliwa na kuchangia
ongezeko la ajira ni pamoja na kujenga miundombinu ya barabara, umeme,
kilimo na mawasiliano. Aidha, sekta binafsi itahamasishwa kutumia fursa
zinazotolewa na Benki na Maendeleo ya Afrika kupitia Dirisha la
kuendeleza sekta binafsi. Kadhalika, Serikali itaajiri watumishi 71,756
katika sekta za Elimu, Afya, Kilimo na kada nyingine.
IV. MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO:
93. Mheshimiwa Spika, katika miaka ya hivi karibuni, Serikali imefanya
maboresho katika mfumo wa kodi kwa nia ya kupanua wigo wa kodi na
kuongeza mapato ya ndani. Maboresho yaliyofanywa ni pamoja na
marekebisho ya sheria za kodi, kanuni na taratibu za usimamiaji wa
kodi. Aidha hatua hizi zimechangia katika kuimarisha ukusanyaji wa
mapato ya kodi na yasiyo ya kodi. Hata hivyo kuna changamoto katika
kuhuisha mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa bajeti hatua kwa
hatua. Kwa
kuzingatia hali hiyo Serikali itaendelea kuchukua hatua zenye kuboresha sera za kodi na usimamiaji wa mapato.
94. Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwenye
mfumo wa kodi, napendekeza kufanya maboresho katika sheria mbalimbali
za kodi kama ifuatavyo:-
a) Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
b) Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
c) Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
d) Sheria ya Ushuru wa Mauzo Nje, SURA 196;
e) Sheria ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act), SURA, 41;
f) Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124;
g) Sheria ya Ushuru wa Viwanja vya Ndege, SURA, 365;
h) Misamaha ya Kodi ya magari kupitia sheria za kodi na matangazo ya Serikali (GNs);
i) Marekebisho mengine katika baadhi ya sheria za kodi na sheria za Usimamizi wa Fedha; na
j) Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea.
k) Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004;
A. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
95. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 kama ifuatavyo: -
(i) Kuanzisha kiwango kipya (VAT Rate) cha asilimia 10 cha Kodi ya
Ongezeko la Thamani kwa baadhi ya watu, taasisi na mashirika yanayopata
unafuu wa kodi hiyo
(special relief). Kwa mantiki hiyo, wale waliokuwa hawalipi kodi hiyo
kuanzia sasa watalipa asilimia 10. Hatua hii itazihusu Kampuni binafsi,
watu binafsi na Kampuni zitakazopewa vyeti vya Kituo cha Uwekezaji
Tanzania isipokuwa zile zenye vyeti hivyo kwa sasa. Aidha, itahusu pia
Mashirika yasiyo ya Kiserikali isipokuwa yale yaliyopewa msamaha wa
kodi pale yanapotoa huduma ya chakula, dawa baridi na vifaa kama vile
sabuni ambavyo vinatolewa msaada kwenye vituo mahsusi vya kulelea
watoto yatima na shule;
(ii) Kurekebisha kifungu cha 19 cha Jedwali la Pili la Sheria ya Kodi
ya Ongezeko la Thamani ili kuongeza Mashine za Elektroniki za kutoa
stakabadhi za kodi (Electronic Fiscal Devices - “EFDs”) katika orodha
ya vifaa vinavyopata msamaha wa kodi hiyo. Lengo ni kuwawezesha walipa
kodi kupata vifaa hivi kwa gharama nafuu na kuhamasisha matumizi yake
kwa kuwa ni muhimu katika kutoa stakabadhi za mauzo ya bidhaa na huduma;
(iii) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa Vifaa vitakavyotumika
kwa ajili ya gesi iliyoshindiliwa na gesi ya mabomba (Compressed
Natural Gas and Piped Natural Gas). Msamaha wa kodi unatolewa ili
kuhamasisha matumizi ya gesi katika magari, kupikia, nyumbani, taasisi
na viwandani. Aidha, Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC)
litawajibika kuhakiki vifaa hivyo ili kuhakikisha kwamba vitatumika
kujenga miundo mbinu ya gesi.
96. Mheshimiwa Spika, Mitambo na vifaa vya kujenga miundombinu ya gesi asili vinavyoombewa msamaha wa kodi ni kama ifuatavyo:-
i. CNG vehicles conversion kits – vifaa vinavyoongezewa kwenye magari yaweze kutembea kwa kutumia nishati ya gesi asili;
ii. High pressure vessels (CNG and LPG cylinders) – mitungi maalumu ya kutunzia gesi asili iliyoshindiliwa na gesi ya LPG;
iii. Natural Gas Compression plants equipments – vifaa kwa ajili ya mitambo ya kushindilia gesi asili;
iv. Natural gas pipes (Transportation and Distribution pipes) – mabomba maalum ya kusafirishia na kusambazia gesi asili;
v. CNG storage cascades – mitungi maalum ya pamoja ya kusafirishia na kuhifadhia gesi asili iliyoshindiliwa;
vi. CNG transportation trailers - magari na matela ya kusafirishia gesi asili iliyoshindiliwa;
vii. Natural gas metering equipments – mita za kupimia kiasi cha gesi asili;
viii. Pipeline fittings and valves – vifaa vya kuunganishia mabomba na kuruhusu/kuzuia gesi kupita;
ix. CNG Refueling/filling equipment – vifaa vya kujazia gesi asili kwenye magari;
x. PNG/CNG accessories – vifaa vidogo vidogo vinavyotumika katika
ujenzi wa mabomba ya gesi asili na katika mitambo ya kushindilia gesi
asili;
xi. Gas Receiving Unit – vifaa vya kupokelea gesi ya mabomba;
xii. Condensate Stabilizer – vifaa vya mifumo ya kuimarisha uhifadhi wa condensate;
xiii. Flare Gas System – vifaa kwa ajili ya mifumo ya kuunguza gesi kwa ajili ya usalama;
xiv. Air & Nitrogen System – vifaa vya mifumo ya hewa na ya Nitrogen;
xv. Condensate Tanks and Loading Facility – matanki ya kuhifadhia condensate na vifaa vya kupakilia;
xvi. System piping on piperack – mifumo ya kubeba mabomba ya gesi asili;
xvii. Instrumentation – vifaa vya umeme na udhibiti kwenye mifumo ya gesi asili.
xviii. Majiko yaliyotengenezwa mahsusi kwa ajili ya matumizi ya gesi pekee.
Hatua hizi katika Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa pamoja zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 22,565.1
B. Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
97. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kama ifuatavyo: -
i. Kuweka kiwango cha chini cha mapato ghafi ya wafanyabiashara wadogo
cha shilingi 3,000,000 kisichotozwa kodi na kurekebisha matabaka
(bands) ya walipa kodi. Lengo la hatua hii ni kulinda mapato halisi ya
Serikali na kuhakikisha kwamba wenye mapato ya chini ya kiwango cha
kutozwa kodi cha shilingi 3,000,000 hawatozwi kodi chini ya mfumo wa
kukadiria kodi Walipa kodi wadogo “Presumptive Scheme” kama ilivyo
kwenye mapato yatokanayo na ajira. Hivi sasa Wafanyabiashara wenye
kipato hicho wanatozwa Sh. 35,000.
Viwango vya sasa na vinavyopendekezwa ni kama ifuatavyo: -
Viwango vya sasa
Thamani ya Mauzo Kodi kwa wasiokuwa na kumbukumbu za mauzo Kodi kwa wenye kumbukumbu za mauzo
(i) Kwa mauzo yasiyozidi Shs. 3,000,000/= Shs. 35,000/= 1.1% ya mauzo
(ii) Kwa mauzo yanayozidi Shs. 3,000,000/= na yasiyozidi Shs.
7,000,000/= Shs. 95,000/= Shs. 33,000/= + 1.3% ya mauzo yanayozidi Shs.
3,000,000/=
(iii) Kwa mauzo yanayozidi Shs. 7,000,000/= na yasiyozidi Shs.
14,000,000/= Shs. 291,000/= Shs. 85,000/= + 2.5% ya mauzo yanayozidi
7,000,000/=
(iv) Kwa mauzo yanayozidi Shs. 14,000,000/= na yasiyozidi Shs.
20,000,000/= Shs. 520,000/= Shs. 260,000/= + 3.3% ya mauzo yanayozidi
Shs. 14,000,000/=
Viwango vinavyopendekezwa
Thamani ya Mauzo Kodi kwa wasiokuwa na kumbukumbu za mauzo Kodi kwa wenye kumbukumbu za mauzo
(i) Kwa mauzo yasiyozidi Shs. 3,000,000/= Asilimia sifuri (0%) Asilimia sifuri (0%)
(ii) Kwa mauzo yanayozidi Shs 3,000,000/= na yasiyozidi Shs 7,500,000/= Shs. 100,000/= 2% ya mauzo yanayozidi
Shs 3,000,000/=
(iii) Kwa mauzo yanayozidi Shs 7,500,000/= na yasiyozidi Shs
11,500,000/= Shs. 212,000/= Shs. 90,000/= plus 2.5% ya mauzo yanayozidi
Shs 7,500,000/=
(iv) Kwa mauzo yanayozidi Shs 11,500,000/= na yasiyozidi Shs
16,000,000/= Shs. 364,000/= Shs. 190,000/= + 3.0% ya mauzo yanayozidi
Shs 11,500,000/=
(v) Kwa mauzo yanayozidi Shs 16,000,000/= na yasiyozidi Shs
20,000,000/= Shs. 575,000/= Shs. 325,000/= + 3.5% ya mauzo yanayozidi
Shs 16,000,000/=
ii. Kutoza Kodi ya Zuio ya asilimia 10 kwenye mapato yatokanayo na riba
inayotolewa na mabenki kwa wafanyabiashara ambao si wakaazi
(non-residents). Lengo ni kuweka usawa kwa walipa kodi wote.
iii. Kufanya marekebisho ya kifungu cha 54 (2) cha sheria ya kodi ya
mapato ili kufuta msamaha wa kodi ya mapato kwa makampuni yenye hisa
zipatazo asilimia 25 au zaidi. Lengo la marekebisho haya ni kuleta
usawa kwa walipa kodi wanapopata gawio.
iv. Kuanzisha kodi itokanayo na uuzaji wa raslimali ya uwekezaji
(capital gains tax) kwenye uuzaji wa hisa za kampuni za ndani
unaofanywa na Kampuni mama ya nje ya nchi.
v. Kuongeza kima cha chini cha kutozwa kodi (threshold) kwenye mapato
ya ajira kutoka shilingi 135,000 hadi 170,000. Hatua hii itaongeza
kipato kwa mfanyakazi.
vi. Kutoa msamaha wa Kodi ya Mapato kwa soko la Hisa la Dar es Salaam
(Dar es salaam Stock Exchange). Lengo ni kulifanya soko hilo kukua.
vii. Kusamehe Kodi ya Mapato (kwa wenye leseni) yatokanayo na michezo
ya kubahatisha iliyokwishalipiwa kodi chini ya sheria ya kodi ya
michezo ya kubahatisha, SURA 41. Lengo la hatua hii ni kuepusha wenye
leseni za biashara ya michezo ya kubahatisha kulipa kodi mara mbili.
viii. Kusamehe Kodi ya Zuio kwenye riba ya mikopo inayotozwa na mabenki
ya nje kwa wawekezaji wanaowekeza kwenye sekta na shughuli muhimu
katika mkakati wa kukuza uchumi (Strategic Investors). Lengo la hatua
hii ni kutoa unafuu kwa wawekezaji hao wanapopata mikopo kutoka kwenye
mabenki ya nje ya nchi na hivyo kuhamasisha uwekezaji hapa nchini.
Hatua hizi za Kodi ya Mapato zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 105,672.3
C. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
98. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 kama ifuatavyo:-
i. Kufuta Ushuru wa bidhaa uliokuwa unatozwa kwenye mafuta mazito ya
kuendeshea mitambo. Hivi sasa mafuta hayo yanatozwa ushuru wa bidhaa wa
shilingi 40 kwa lita. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za
uzalishaji katika viwanda hapa nchini. Aidha, hatua hii itaongeza
uzalishaji na kuleta ushindani sawa kwa wenye viwanda katika nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuwa nchi nyingine hivi sasa
hazitozi ushuru kwenye bidhaa hiyo.
ii. Mheshimiwa Spika, kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha wasanii
kudurufiwa kazi zao za sanaa na kukosa maslahi kwa kazi wanazofanya.
Ili kutatua tatizo hili, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato itaanza
kurasimisha biashara ya bidhaa za muziki na filamu kwa nia ya
kuhakikisha kwamba uasili wake unatambulika na hivyo kuzuia vitendo vya
kudurufu kazi za sanaa (piracy of artists work) hali ambayo inadumaza
ukuaji wa sanaa na vipaji hapa nchini. Aidha, Mamlaka ya Mapato itaweka
stampu kwenye bidhaa hizo ili uuzaji wa kazi hizo uwe rasmi na
kuwawezesha wasanii kupata kipato stahili kutokana na kazi zao.
Vilevile hatua hii itaiingizia serikali mapato.
Kwa kuwa yanahitajika maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na
kurekebisha sheria na kanuni mbalimbali, utekelezaji wa hatua hii
utaanza rasmi tarehe 1 Januari, 2013.
iii. Kufuta msamaha wa Ushuru wa Bidhaa kwa magari kwa wote waliokuwa
wananufaika na msamaha huo isipokuwa kwa miradi inayotekelezwa kwa
misaada ya wafadhili yenye msamaha wa kodi kwenye mkataba, mashirika ya
dini, Balozi, Ofisi za Balozi, Wanabalozi na Wawakilishi wa mashirika
ya kimataifa (Diplomats and Diplomatic Missions). Aidha haitahusu
Kampuni za Madini zenye mikataba yenye kutoa misamaha.
iv. Ili kulinda viwanda vya hapa nchini vinavyotengeneza maji ya
matunda (juisi) dhidi ya ushindani usio haki wa bidhaa hiyo kutoka nje,
maji ya matunda kutoka nje yatatozwa ushuru wa bidhaa wa shilingi 83
kwa lita ambapo yanayozalishwa hapa nchini yatatozwa ushuru wa bidhaa
wa shilingi 8 tu kwa lita.;
v. Kurejea msamaha wa ushuru wa mafuta ya petroli (fuel levy)
uliotolewa mwaka 2011/12 kwenye mafuta yanayotumika kuendesha meli, na
vifaa vingine vinavyotumika katika utafiti wa mafuta na gesi ili
usomeke kama Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty) kwenye mafuta ya Petroli.
vi. Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Ushuru wa bidhaa unaotozwa
kwenye pombe, vinywaji baridi, sigara, na mvinyo kama ifuatavyo: -
a. Vinywaji baridi kutoka shilingi 69 kwa lita hadi shilingi 83 kwa lita ikiwa ni nyongeza ya shilingi 14;
b. Mvinyo uliotengenezwa kwa Zabibu inayozalishwa hapa nchini kwa
kiwango kinachozidi asilimia 75 kutoka shilingi 420 kwa lita hadi
shilingi 145 kwa lita, ikiwa ni punguzo la shilingi 275;
c. Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa
kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi 1,345 kwa lita hadi
shilingi 1,614 kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 269;
d. Vinywaji vikali, kutoka shilingi 1,993 kwa lita hadi shilingi 2,392 kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 399.
e. Bia inayotengenezwa na nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa,
kutoka shilingi 248 kwa lita hadi shilingi 310 kwa lita, ikiwa ni
nyongeza ya shilingi 62;
f. Bia nyingine zote, kutoka shilingi 420 kwa lita hadi shilingi 525
kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 105 sawa na shilingi 52.5 kwa
chupa yenye ujazo wa nusu lita;
Marekebisho ya viwango vya Ushuru wa bidhaa kwenye sigara ni kama ifuatavyo: -
a) Sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku
inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka
shilingi 6,820 hadi shilingi 8,210 kwa sigara elfu moja. Hii ni sawa na
nyongeza ya shilingi 1,390 kwa sigara elfu moja au shilingi 1.4 kwa
sigara moja;
b) Sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku
inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka
shilingi 16,114 hadi shilingi 19,410 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni
nyongeza ya shilingi 3,296 au shilingi 3.3 kwa sigara moja;
c) Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (a) na (b) kutoka shilingi
29,264 hadi shilingi 35,117 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni nyongeza ya
shilingi 5,853 sawa na shilingi 5.8 kwa sigara moja;
d) Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) kutoka
shilingi 14,780 hadi shilingi 17,736 kwa kilo, ikiwa ni nyongeza ya
shilingi 2,956 kwa kilo; na,
e) Ushuru wa “Cigar” unabaki kuwa asilimia 30.
vii. Kutoza Ushuru wa bidhaa kwenye Gesi asilia inayotumika viwandani
kwa kiwango cha Shilingi 0.35 kwa kila futi ya ujazo (Shs 0.35 per
cubic feet);
viii. Kuongeza Ushuru wa bidhaa kwenye muda wa maongezi (airtime)
kwenye simu za mkononi kutoka asilimia 10 kwenda asilimia 12. Lengo la
hatua hii ni kuwianisha ushuru wa bidhaa unaotozwa kwa huduma hii
katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa wakati huu ambapo tupo
kwenye soko la pamoja.
Hatua hizi katika Ushuru wa Bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 144,054.9
D. Sheria ya Ushuru wa Mauzo Nje, Sura 196;
99. Mheshimiwa Spika, napendekeza kuongeza kiwango cha Ushuru wa mauzo
nje (export levy) kwenye bidhaa za ngozi ghafi zinazosafirishwa kwenda
nje ya nchi kutoka asilimia 40 za sasa au Shilingi 400 kwa kilo moja
hadi asilimia 90 au Shilingi 900 kwa kilo moja kutegemea kiwango kipi
ni kikubwa. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha usindikaji wa ngozi hapa
nchini na kuongeza thamani ya bidhaa za ngozi. Aidha hatua hii
itachangia katika kukuza ajira viwandani na kuongeza mapato ya Serikali.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 26,431.8
E. Sheria ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act), SURA, 41;
100. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya
Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act), SURA 41; kama ifuatavyo:-
i. Kuongeza tozo la Gaming Tax kwa casino kutoka asilimia 13 ya mapato
ghafi ya mchezo wa kubahatisha (Gross Gaming Revenue) hadi asilimia 15;
ii. Kutoza tozo kwenye michezo ya Utabiri wa matokeo ya michezo (Sports Betting) kwa asilimia 6 ya “total stakes”;
iii. Kutoza tozo la Gaming Tax kwa kiwango cha asilimia 43 kwenye michezo ya “SMS Lotteries”;
iv. Kutoza tozo la Gaming Tax kwa kiwango cha asilimia 15 kwa michezo ya Internet Casino.
v. Kuweka kipengele katika Sheria ya Kodi ya Michezo ya kubahatisha kinachotamka kwamba “gaming tax shall be conclusive tax”.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 6,360.
F. Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124;
101. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya
Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124 kwa kuanzisha utaratibu wa
kumiliki usajili wa namba za magari zenye utambulisho wa taarifa za mtu
binafsi kwenye gari lake kwa ada ya shilingi 5,000,000 kwa miaka
mitatu.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 50
G. Sheria ya Ushuru wa Viwanja vya Ndege, SURA, 365;
102. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya
Ushuru wa Viwanja vya Ndege, SURA, 365 kwa kuongeza tozo ya huduma za
viwanja vya ndege (Airport Service Charges) kutoka kiwango cha sasa cha
Dola za Kimarekani 30 hadi Dola 40 kwa safari za nje na kutoka Shilingi
za Tanzania 5,000 hadi Shilingi 10,000 kwa safari za ndani.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 11,597.7
H. Misamaha ya kodi ya magari kupitia sheria za kodi na matangazo ya Serikali (GNs)
103. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye sheria
husika za kodi na matangazo ya Serikali yanayotoa msamaha wa kodi
kwenye magari kwa walengwa mbalimbali ili kuweka ukomo wa umri wa miaka
nane (8) kwa magari hayo badala ya miaka 10. Aidha, magari yenye umri
wa zaidi ya miaka nane (8) yatatozwa Ushuru wa bidhaa wa asilimia 20.
Lengo la hatua hii ni kupunguza wimbi la uagizaji wa magari chakavu na
kulinda mazingira.
I. Marekebisho mengine katika baadhi ya Sheria za Kodi na sheria za Usimamizi wa Fedha
104. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho mengine madogo
madogo yasiyo ya kisera katika Sheria mbalimbali za kodi ili ziwe
sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake.
105. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika sheria ya
Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki, SURA 231 ili kwanza, kuweka
kinga dhidi ya mali zinazomilikiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika
Mashariki ikiwemo nyumba, akiba, fedha na akaunti za benki dhidi ya
mashauri ya kisheria, maamuzi ya kimahakama na utaifishaji. Pili, kuipa
hadhi ya mdai benki hii kama ilivyo kwa Taasisi ya Fedha ya Kimataifa
(IMF), Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika ili kuiwezesha
kupewa upendeleo endapo yatatokea matatizo yoyote katika soko la fedha.
Tatu, kumpa mamlaka Waziri wa Fedha kutekeleza maamuzi ya Baraza la
uongozi (Governing Board) la EADB kwa kurekebisha Jedwali la Sheria hii
kupitia Tangazo la Serikali na baadaye kuwasilisha taarifa Bungeni.
Nne, kutoa tafsiri ya mali za benki ili kutoa ufafanuzi kwamba mali za
benki ni pamoja na nyumba za benki, akiba za fedha zilizokasimiwa kwa
EADB kwa ajili ya utendaji wake.
J. Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea
106. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya
ada na tozo mbali mbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara
zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa
uchumi.
K. Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004
107. Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
walifanya Kikao cha maandalizi ya Bajeti (Pre-Budget Consultations of
EAC Ministers for Finance) mnamo tarehe 18 Mei 2012 jijini Kampala,
Uganda. Kikao hicho kilipendekeza marekebisho ya viwango vya Ushuru wa
Pamoja wa Forodha (EAC-Common External Tariff “CET”) na Sheria ya
Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Customs Management Act,
2004) kwa mwaka wa fedha wa 2012/13. Mapendekezo hayo yanalenga katika
kuboresha Sekta za Viwanda, Usafirishaji, Afya, Nishati, Mifugo,
Mawasiliano na Habari.
108. Mheshimiwa Spika, maeneo yanayopendekezwa kufanyiwa marekebisho kwenye viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha ni: -
i. Kutoza ushuru wa asilimia sifuri (0%) badala ya asilimia 35 kwenye
ngano inayotambuliwa katika HS Code 1001.90.20 na HS Code 1001.90.90
kwa kipindi cha mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za
uingizaji wa bidhaa hii nchini kwa vile uzalishaji wa ndani bado ni wa
chini kuweza kutosheleza mahitaji.
ii. Kuongeza Ushuru wa Forodha kwenye galvanized wire kutoka asilimia
sifuri (0%) hadi asilimia 10 inayotambuliwa katika HS Code 7217.20.00.
Hatua hii inalenga katika kuwianisha viwango vya utozaji wa Ushuru wa
Forodha kwa vile bidhaa hii inatengenezwa kutokana na hot rolled steel
wire rods zinazotambuliwa katika HS Code 7213.20.00 ambayo inatozwa
ushuru wa asilimia 10.
iii. Kutenganishwa kwa bidhaa zinazotambulika katika HS Code 2106.90.91
ili kutenganisha virutubisho vya chakula na madini (food supplements
and mineral premix) vinavyotumika katika kutengeneza chakula cha watoto
wachanga na kuzitoza Ushuru wa Forodha wa asilimia sifuri (0%). Hatua
hii inalenga katika kuwezesha watoto wachanga na wagonjwa kuweza kupata
vyakula vyenye virutubisho kwa bei nafuu na kuimarisha afya zao.
iv. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia sifuri
kwenye ving’amuzi (set top boxes) vinavyotambuliwa katika HS Code
8528.71.00 ili kuwezesha mabadiliko ya kutoka katika teknolojia ya
analogi na kwenda katika teknolojia ya digitali. Hatua hii inatekeleza
makubaliano ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwamba
ifikapo Desemba 2015 ziwe zimetoka kwenye mfumo wa utangazaji wa
analogi kwenda digitali.
v. Kupunguza Ushuru wa Forodha kwenye umeme (HS Code 2716.00.00) kutoka
asilimia 10 hadi asilimia sifuri (0%). Hatua hii inalenga katika
kupunguza gharama ya umeme unaonunuliwa kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji katika nchi hizo.
vi. Kupunguza Ushuru wa Forodha kwenye glasi za ndani (inner glass) za
chupa za chai (thermos) zinozotambuliwa katika HS Code 7020.00.90
kutoka asilimia 25 hadi asilimia sifuri ili kutoa unafuu na kuchochea
ukuaji wa viwanda vya kuunganisha chupa za chai katika nchi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki kwa kuwa bidhaa hiyo haipatikani katika Jumuiya.
vii. Kutenganisha programu (software) inayotambulika katika HS Code
8523.80.00 ili kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia sifuri (0%). Lengo
ni kuhamasisha ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano na hivyo kuongeza mchango
wake katika Pato la Taifa.
viii. Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwenye
malighafi ya kutengeneza sabuni (Palm Sterini, RBD) inayotambuliwa
katika HS Code 1511.90.40 kwa kipindi cha mwaka moja. Hatua hii
inalenga katika kuvipa unafuu viwanda vidogo vya kutengeneza sabuni
hapa nchini na kuviwezesha kumudu ushindani katika bidhaa hiyo
inapoingizwa kutoka nje.
ix. Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa malighafi
ya kutengeneza sabuni inayojulikana kama LABSA inayotambuliwa katika HS
Code 3402.11.00; HS Code 3402.12.00 na HS Code 3402.19.00 kwa kipindi
cha mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kuimarisha uzalishaji na
kukuza viwanda vidogo vya sabuni nchini.
x. Kupunguza Ushuru wa Forodha kwenye bidhaa inayojulikana kama
cathodes inayotambuliwa katika HS Code 7403.11.00 kutoka asilimia 10
hadi sifuri (0%). Hivi sasa bidhaa hii inatozwa ushuru wa asilimia 10
ambapo shaba iliyotengenezwa kwa ukamilifu (refined alloys/refined
copper) hutozwa ushuru wa asilimia (0%), ambapo ni kinyume na matakwa
ya sheria ya ushuru wa forodha ya jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka
2004. Lengo la hatua hii ni kuwianisha ushuru wa malighafi inayotumika
kuzalisha bidhaa hii ili iendane na kanuni/taratibu za kutoza ushuru
zinazozingatia viwango vya usindikaji.
xi. Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya
asilimia 35 kwenye saruji inayotambuliwa katika HS Code 2523.90.00 kwa
kipindi cha mwaka mmoja.
xii. Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa
wazalishaji wanaotumia mafuta ya kutengeneza vilainishi (castor oil and
its fraction) inayotambuliwa katika HS Code 1515.30.00 Hatua hii
imezingatia kwamba bidhaa hii ni mali ghafi inayotumika katika
kutengeneza vilainishi;
xiii. Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye vyuma vinavyowekwa
kwenye kingo za barabara vijulikanavyo kama road guard rails kwa
kutenganisha HS Code 7308.90.90. Lengo ni kutoa unafuu katika ujenzi wa
miundombinu ya barabara. Aidha, hatua hii inazingatia kwamba bidhaa hii
haizalishwi kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya soko la Jumuiya ya
Afrika Mashariki;
109. Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki walifanya marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Customs Management Act, 2004) kama
ifuatavyo:-
i. Kufanya marekebisho katika Kifungu 30(b) cha Sehemu B ya Jedwali la
Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye mitambo (machinery) na vipuri vyake
vinavyotumika kwenye uchimbaji wa madini. Msamaha huu hautahusisha
vipuri vya magari vitakavyoagizwa na makampuni yanayojihusisha na
uchimbaji wa madini.
ii. Kufanya marekebisho katika aya ya 22 (a) ya Jedwali la Tano la
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuongeza
“refrigerated trailers” katika bidhaa zinazopata msamaha wa Ushuru wa
Forodha. Hatua hii inalenga katika kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha
kwenye magari ya trela yenye majokofu ili kuimarisha biashara ya
usambazaji bidhaa kama vile nyama, maziwa n.k.
iii. Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye malighafi zinazotumika
katika kutengeneza vifaa vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa (medical
diagnostic kits) kwa kuwa vifaa hivyo hutozwa asilimia sifuri (0%)
vinapoagizwa kutoka nje. Aidha, lengo pia ni kuhamasisha uzalishaji wa
bidhaa hiyo katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
iv. Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano, B kwenye aya ya 15 ili
kuongeza vifaa vinavyotumika katika ufugaji na kurina asali na kuvipa
msamaha wa ushuru wa forodha vinapoagizwa nje na wafugaji wa nyuki.
Lengo ni kuhamasisha na kuchochea ukuaji wa sekta ya ufugaji wa nyuki.
v. Kuendelea kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye migahawa ya Majeshi ya Ulinzi kwa kipindi cha mwaka mmoja.
vi. Kufanya marekebisho katika Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya mwaka 2004 ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty
remission) kwa wazalishaji wa vyakula vinavyotengenezwa mahsusi kwa
lishe ya watoto wenye utapia mlo na watu wanaoishi na virusi vya
ukimwi. Hatua hii inalenga katika kuwawezesha kupata vyakula hivyo kwa
gharama nafuu na kuboresha afya zao.
110. Mheshimiwa Spika, Marekebisho mengine ninayotarajia kufanya kwenye Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo: -
i. Kufuta msamaha wa Ushuru wa Forodha kwa magari yenye ujazo wa cc
3000. Hatua hii haitahusu miradi inayotekelezwa kwa misaada ya
wafadhili yenye msamaha wa kodi kwenye mikataba, mabalozi na
wawakilishi wa mashirika ya kimataifa (Diplomats and Diplomatic
missions).
ii. Kupunguza msamaha wa kodi uliokuwa unatolewa kwenye bidhaa
zinazotambulika kama “deemed capital goods” kutoka asilimia 100 hadi
asilimia 90. Kwa mantiki hiyo, mwekezaji atatakiwa kulipa asilimia 10
ya kodi zote zinazotozwa kwenye bidhaa husika.
Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 12,805
Mheshimiwa Spika, hatua zote za mapato kwa ujumla zimezingatia azma ya
Serikali ya kukuza uchumi na kuongeza mapato ili hatimaye kupunguza
utegemezi wa bajeti kutoka kwa wahisani. Aidha, ili kutekeleza azma
hiyo, hatua za mapato zinalenga katika kupunguza misamaha ya kodi hatua
kwa hatua ili kufikia kiwango cha asilimia 1 ya Pato la Taifa kama
ilivyo katika nchi nyingine Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
L. Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi
111. Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kodi zinazopendekezwa zitaanza
kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2012, isipokuwa pale ilipoelezwa
vinginevyo.
V. SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2012/13
112. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za uchumi pamoja na misingi
na sera za bajeti, Serikali inatarajia kukusanya shilingi bilioni
15,119.6. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya
kodi na yasiyo ya kodi ya jumla ya shilingi bilioni 8,714.8 sawa na
asilimia 18 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato kutokana na vyanzo vya
Halmashauri ni shilingi bilioni 362.2 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la
Taifa.
113. Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuendelea
kutusaidia mwakani kwa kutupatia misaada na mikopo ya jumla ya shilingi
bilioni 3,156.7. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 842.5 ni misaada
na mikopo ya kibajeti na shilingi bilioni 2,314.2 ni mikopo na misaada
kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikijumuisha Basket Funds na fedha za
Millenium Challenge Account (MCA - T).
114. Mheshimiwa Spika, Serikali inategemea kukopa kiasi cha shilingi
bilioni 2,886.1 kutoka vyanzo vya ndani na nje kuziba pengo la mapato.
Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1,148.1 ni kwa ajili ya kulipia
hatifungani na dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva, shilingi
bilioni 483.9 ambayo ni asilimia moja ya Pato la Taifa na shilingi
bilioni 1,254.1 ni mikopo yenye masharti ya kibiashara.
115. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa matumizi, Serikali imepanga
kutumia jumla ya shilingi bilioni 15,119.6 katika mwaka 2012/13 kwa
ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Jumla ya shilingi bilioni
10,591.8 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikijumuisha
shilingi bilioni 3,781.1 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa
Serikali, Taasisi na Wakala za Serikali na shilingi bilioni 2,745.1 kwa
ajili ya Mfuko Mkuu wa Serikali. Aidha, jumla ya shilingi bilioni
4,527.8 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, ambapo kiasi cha
shilingi bilioni 2,213.6 kitagharamiwa kwa fedha za ndani na shilingi
bilioni 2,314.2 kitagharamiwa kwa fedha za nje (misaada na mikopo ya
miradi ya maendeleo ikijumuisha miradi ya MCA (T) na basket fund).
116. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama ulivyoelezwa
hapo juu, sura ya bajeti kwa mwaka 2012/13 inakuwa kama ifuatavyo:-
Mapato Shilingi Milioni
A. Mapato ya Ndani 8,714,671
(i) Mapato ya Kodi (TRA) 8,070,088
(ii) Mapato yasiyo ya Kodi 644,583
B. Mapato ya Halmashauri 362,206
C. Mikopo na Misaada ya Kibajeti 842,487
D. Mikopo na Misaada ya Miradi ya Maendeleo ikijumuisha MCA (T) 2,314,231
E. Mikopo ya Ndani 1,631,957
F. Mikopo yenye Masharti ya Kibiashara 1,254,092
JUMLA YA MAPATO YOTE 15,119,644
Matumizi
G. Matumizi ya Kawaida 10,591,805
(i) Deni la Taifa 2,745,056
(ii) Mishahara 3,781,100
(iii) Matumizi Mengineyo 4,065,649
Wizara 3,311,399
Mikoa 49,701
Halmashauri 704,549
H. Matumizi ya Maendeleo 4,527,839
(i) Fedha za Ndani 2,213,608
(ii) Fedha za Nje 2,314,231
JUMLA YA MATUMIZI YOTE 15,119,644
117. Mheshimiwa Spika, mambo yaliyozingatiwa wakati wa mgao wa fedha kwa bajeti ya mwaka 2012/13 ni pamoja na yafuatayo:-
i. Kuweka mafungu yote katika kiwango cha mgao wa fedha kinacholingana
na matarajio ya matumizi ya mafungu husika kwa mwaka 2011/12;
ii. Kuyatengea fedha matumizi yasiyoepukika kama vile posho za kisheria, “ration allowance”, nk.
iii. Maeneo mapya ya utawala;
iv. Fedha zinazotolewa kwa wizara zenye utaratibu wa kubakiza (retention);
v. Maeneo ya vipaumbele (strategic na non-strategic).
118. Mheshimiwa Spika, bajeti ninayoiwasilisha ina uwiano wa asilimia
70 kwa matumizi ya kawaida na asilimia 30 kwa matumizi ya maendeleo.
Viwango hivyo vya uwiano vimezingatia ukweli kwamba makisio ya matumizi
ya maendeleo kwa fedha za ndani ya Shilingi 1,871.5 bilioni na makisio
ya matumizi ya maendeleo kwa fedha za nje ya Shilingi 3,054.1 bilioni
yenye jumla ya Shilingi 4,925.6 kwa mwaka 2011/12 hayatafikiwa. Hivyo,
inatarajiwa kwamba hali halisi ya matumizi ya maendeleo itakuwa
Shilingi 2,983 bilioni ambayo ni karibu ya asilimia 22. Kwa kipindi
kilichoishia Aprili, 2012 matumizi ya maendeleo kwa fedha za ndani
yalifikia 1,201.6 bilioni na matumizi ya maendeleo kwa fedha za nje ni
shilingi 1,450.4 bilioni. Sababu za kutofikiwa kwa malengo hayo ya
matumizi nimezieleza hapo awali ikiwa ni pamoja na kutopatikana kwa
fedha za mikopo ya kibiashara na kuchelewa kwa fedha za misaada na
mikopo ya miradi ya maendeleo kutoka kwa wahisani. Aidha, uwiano huo
umezingatia maeneo niliyoyataja hapo juu ambayo ni matumizi muhimu.
VI. HITIMISHO
119. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia bajeti hii imejipanga
kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13 ambao unaelekeza
uwekezaji wa rasilimali za Taifa kwenye maeneo machache ya kipaumbele
kwa lengo la kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi na kupunguza umaskini.
Serikali itaendelea kuhamasisha sekta binafsi kwa kuwekeza zaidi katika
maeneo ya kipaumbele. Aidha, kila mwananchi anapaswa kushiriki
kikamilifu katika kutumia fursa zinazojitokeza kwa kutoa huduma na
kuzalisha mali ili kujiongezea kipato.
120. Mheshimiwa Spika, kufanikiwa kwa Bajeti ya Mwaka 2012/13
kunahitaji nidhamu ya hali ya juu kwa kila Wizara, Idara, Mikoa,
Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ukusanyaji wa mapato na
matumizi ya fedha za umma. Matumizi yasiyokuwa na tija na ambayo si
muhimu ni vyema yakaepukwa. Sekta binafsi ina uwezo mkubwa wa kuchangia
katika uchumi. Hivyo, ni muhimu kila Wizara, Idara, Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa kutoa fursa kwa sekta binafsi ili waweze kuchangia
kikamilifu katika kukuza uchumi wa Taifa letu.
121. Mheshimiwa Spika, Mkutano wa Bunge la Bajeti mwaka huu unafanyika
miezi michache kabla ya zoezi muhimu la Sensa ya Watu na Makazi
itakayofanyika tarehe 26 Agosti 2012. Kauli mbiu ya sensa ya mwaka huu
ni ‘‘Sensa kwa Maendeleo Jiandae Kuhesabiwa’’. Napenda kutoa wito kwa
Waheshimiwa Wabunge na viongozi wengine katika ngazi zote kuhamasisha
wananchi kushiriki katika zoezi hili ambalo matokeo yake yatawezesha
kupata takwimu muhimu zitakazowezesha Serikali kupanga mipango kwa
ajili ya maendeleo ya wananchi kwa usahihi.
122. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wapiga
kura wangu wote wa Jimbo la Kalenga kwa kunichagua kuwa Mbunge wao na
kwa ushirikiano wanaonipatia. Napenda kuwaahidi kuwa nitaendelea
kushirikiana nanyi kuliletea maendeleo Jimbo letu la Kalenga. Mwisho
namshukuru mke wangu mpendwa pamoja na familia kwa kuwa msaada kwangu
katika kutekeleza majukumu haya mapya.
123. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.