Kova: Sitaki malumbano *Adai sakata la Dkt. Ulimboka liachiwe mahakama *Asema ni kinyume cha katiba kujadili jambo hilo
Na Stella Aron
KAMANDA wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, amesema jeshi hilo haliwezi kuingia
kwenye mtego wa malumbano na taasisi za dini ambazo zinaongozwa na
Wakristo, Waislamu au madhehebu mengine.
Kamanda Kova aliyasema hayo Dar es Salam jana
wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kauli iliyotolewa na
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufua na Uzima, Josephat Gwajima.
Katika
mahubili yake yaliyofanyika kanisani hapo Dar es Salaam juzi, Mchungaji
Gwajima alikanusha taarifa zilizotolewa na Jeshi la Polisi kuwa,
mtuhumiwa anayedaiwa kumteka nyara, Dkt. Steven Ulimboka, alikwenda
kwenye katika hilo kufanya toba.
“Hivi sasa sakata hili
halizungumziki kwa kuwa mtuhumiwa tayari amefikishwa Mahakamani, kesi
yake ni PI 5/2012 na yupo rumande gerezani akikabiliwa na shtaka la
utekaji nyaraka na kujaribu kuua.
Kamanda Kova aliongeza kuwa,
sakata la Dkt. Ulimboka (Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini) na
kukamatwa kwa mtuhumiwa Bw. Joshua Gitu Mhindi, limefungwa kwani
kuendelea kulizungumza ni kuingilia uhuru wa mahakama.
“Ni
kinyume cha Katiba ya Tanzania kujadili jambo ambalo liko Mahakamani
kama ilivyo katika shauri hili, kama tukiendelea kulizungumzia,
Mahakama itashindwa kuendelea na kesi.
“Namheshimu sana
Mchungaji Gwajima, nisingependa kujibu hoja zote alizotoa, kazi ya
Jeshi la Polisi ni kufanya doria za mwili, mitaa, vijiji na viongozi wa
dini wanafanya doria za kiroho ambapo utii wa sheria bila shuruti ni
kazi ya polisi, utii ni thawabu kwa Waislamu na baraka za utii kwa
Wakristo,” alisema Kamanda Kova.
Alisema polisi wana wajibu wa
kudumisha amani ili waumini wa dini zote wasali kwa uhuru bila hofu
hivyo jeshi hilo halipo tayari kuendelea na malumbano hayo.
“Tunawaomba
wananchi waendelee kuliamini Jeshi la Polisi na kutupa ushirikino kwa
kutoa taarifa za uhalifu kwani kumekuwa na uvumi unaosababisha
upelelezi kuchelewa,” alisema na kuongeza kuwa, kuna uvumi unaondelea
kuhusu suala la utekwaji nyara Dkt. Ulimboka ambao unaweza kuchelewa
upelelezi.
Kamanda Kova alisema, jeshi hilo lina uhakika na
ushahidi wa mtuhumiwa Bw. Mhindi, kutokana na maelezo aliyotoa polisi
hivyo na wasingependa kuyaeleza kwani wataingilia uhuru wa mahakama.
Kuhusu
madai kuwa mtuhumiwa ni kichaa au mwendawazimu, Kamanda Kova alisema,
mwenye uwezo kisheria wa kuthibitisha madai hayo ni daktari pekee.
“Hata
kichaa anamilikiwa na sheria, kama akifanya makosa ya jinai
anashughulikiwa kama mhalifu ambaye kama atafanya kosa la jinai, hawezi
kuachwa hivi hivi,” alisema.
Juzi Mchungaji Gwajima, alilitupia
lawama Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kudai kuwa,
mtuhimiwa Bw. Mhindi hakufika katika kanisa lake kufanya sala ya toba
na kudai kuwa, mtuhumiwa huyo ni kichaa.