Jumatano, July 18, 2012
Taarifa ya Serikali Meli iliyozama
MAAFA YA KUZAMA KWA MELI ZANZIBAR
Meli ya Mv. Star Gate imezama
karibu na Kisiwa cha Chumbe ambapo watu 12 wamefariki hadi muda huu na
wengine kadhaa wamejeruhiwa.
Akitoa taarifa fupi kwa
waandishi wa habari,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi,Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini alisema taarifa za
kuzama kwa meli hiyo ilitolewa na Boti iendayo kasi ya Kilimanjaro III
iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Zanzibar ndipo ilipoiona meli
hiyo ikizama.
“Tulipata taarifa kutoka Boti
ya abiria ya Kilimanjaro III saa 7:50 mchana waliporipoti kuona meli
ikizama karibu na Kisiwa cha Chumbe” Alisema Waziri Mwinyihaji.
Waziri huyo alisema Meli hiyo
imezama maili sita kuelekea Kisiwa cha Yasin Kusini mwa Kisiwa cha
Chumbe kilichopo Unguja maili kadhaa kutoka Bandari ya Malindi.
Waziri Mwinyihaji alisema idadi
ya abiria walikuwa 250 ambao ni watu wazima, watoto 31 na mabaharia 6.
“Tumepeleka waokoaji, kuna boti tano zipo eneo la tukio kushirikiana na
waokoaji wengine” Alisema Waziri Mwinyihaji.
Alisema maiti zote zitapelekwa
viwanja vya Maisara Zanzibar kwa ajili ya ndugu na jamaa kuzitambua
maiti za ndugu zao ambapo majeruhiwa wote watatibiwa Hospitali Kuu ya
Mnazi Mmoja.
Katika Bandari ya Malindi
mwandishi wetu ameshuhudia maiti kadhaa zikiwemo za watoto zikishushwa,
Miongoni mwa abiria waliookolewa ni raia 13 wa Mataifa mbalimbali ya
nje huku raia mmoja ambaye hakuweza kutambuliwa utaifa wake amepoteza
maisha.
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar,
Balozi Seif Ali Idd alifika eneo la Bandari ya Malindi Zanzibar pamoja
viongozi wengine akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir
Kificho, Mawaziri na baadhi ya Wajumbe a Baraza la Wawakilishi
walikuwepo kutoa msaada unaohitajika.
Katika eneo la pembezoni mwa
bandari ya Malindi, makundi ya wananchi yalikuwa yamekusanyika
wakisubiri taarifa za tukio hilo tangu saa 8:30 mchana.
Vikosi vya ulinzi na usalama, msalaba mwekundu na watoaji wengine wa misaada ya dharura walifika kwa haraka eneo la tukio.
Hadi sasa kazi ya uokoaji inaendelea karibu na Kisiwa cha Yasin ilikozama meli hiyo.
Meli ya Mv. Star Gate
inamilikiwa na kampuni ya kizalendo ya Sea Gull Sea Transport Ltd
ambayo mwaka 2009 Meli yake nyengine ya Mv. Fatih ilipinduka na kuzama
katika Bandari ya Malindi Zanzibar na kua watu sita.
Mwaka jana Zanzibar ilikumbwa
na maafa baada ya Meli ya Mv. Spice Islanders kuzama katika bahari ya
Hindi eneo la Nungwi katika Kisiwa cha Unguja ikielekea Kisiwani Pemba
ambapo taarifa rasmi ya Serikali ilisema watu 197 walipoteza maisha na
wengine wengi kujeruhiwa.