Wednesday, July 18, 2012

Kova

Kova: Sitaki malumbano *Adai sakata la Dkt. Ulimboka liachiwe mahakama *Asema ni kinyume cha katiba kujadili jambo hilo



Na Stella Aron

KAMANDA wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, amesema jeshi hilo haliwezi kuingia kwenye mtego wa malumbano na taasisi za dini ambazo zinaongozwa na Wakristo, Waislamu au madhehebu mengine.

Kamanda Kova aliyasema hayo Dar es Salam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kauli iliyotolewa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufua na Uzima, Josephat Gwajima.

Katika mahubili yake yaliyofanyika kanisani hapo Dar es Salaam juzi, Mchungaji Gwajima alikanusha taarifa zilizotolewa na Jeshi la Polisi kuwa, mtuhumiwa anayedaiwa kumteka nyara, Dkt. Steven Ulimboka, alikwenda kwenye katika hilo kufanya toba.

“Hivi sasa sakata hili halizungumziki kwa kuwa mtuhumiwa tayari amefikishwa Mahakamani, kesi yake ni PI 5/2012 na yupo rumande gerezani akikabiliwa na shtaka la utekaji nyaraka na kujaribu kuua.

Kamanda Kova aliongeza kuwa, sakata la Dkt. Ulimboka (Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini) na kukamatwa kwa mtuhumiwa Bw. Joshua Gitu Mhindi, limefungwa kwani kuendelea kulizungumza ni kuingilia uhuru wa mahakama.

“Ni kinyume cha Katiba ya Tanzania kujadili jambo ambalo liko Mahakamani kama ilivyo katika shauri hili, kama tukiendelea kulizungumzia, Mahakama itashindwa kuendelea na kesi.

“Namheshimu sana Mchungaji Gwajima, nisingependa kujibu hoja zote alizotoa, kazi ya Jeshi la Polisi ni kufanya doria za mwili, mitaa, vijiji na viongozi wa dini wanafanya doria za kiroho ambapo utii wa sheria bila shuruti ni kazi ya polisi, utii ni thawabu kwa Waislamu na baraka za utii kwa Wakristo,” alisema Kamanda Kova.

Alisema polisi wana wajibu wa kudumisha amani ili waumini wa dini zote wasali kwa uhuru bila hofu hivyo jeshi hilo halipo tayari kuendelea na malumbano hayo.

“Tunawaomba wananchi waendelee kuliamini Jeshi la Polisi na kutupa ushirikino kwa kutoa taarifa za uhalifu kwani kumekuwa na uvumi unaosababisha upelelezi kuchelewa,” alisema na kuongeza kuwa, kuna uvumi unaondelea kuhusu suala la utekwaji nyara Dkt. Ulimboka ambao unaweza kuchelewa upelelezi.

Kamanda Kova alisema, jeshi hilo lina uhakika na ushahidi wa mtuhumiwa Bw. Mhindi, kutokana na maelezo aliyotoa polisi hivyo na wasingependa kuyaeleza kwani wataingilia uhuru wa mahakama.

Kuhusu madai kuwa mtuhumiwa ni kichaa au mwendawazimu, Kamanda Kova alisema, mwenye uwezo kisheria wa kuthibitisha madai hayo ni daktari pekee.

“Hata kichaa anamilikiwa na sheria, kama akifanya makosa ya jinai anashughulikiwa kama mhalifu ambaye kama atafanya kosa la jinai, hawezi kuachwa hivi hivi,” alisema.

Juzi Mchungaji Gwajima, alilitupia lawama Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kudai kuwa, mtuhimiwa Bw. Mhindi hakufika katika kanisa lake kufanya sala ya toba na kudai kuwa, mtuhumiwa huyo ni kichaa.