Thursday, April 26, 2012

TGNP Yaitaka Serikali Iwajibishe Mawaziri Wabadhirifu


TGNP Yaitaka Serikali Iwajibishe Mawaziri Wabadhirifu

Na Mwandishi Wetu

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) imeitaka Serikali kuwawajibisha mara moja mawaziri, manaibu waziri na watendaji wakuu wa Serikali na mashirika ya umma ambao wametajwa kuhusika na matumizi mabaya ya fedha za umma ama kushindwa kusimamia rasilimali za taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Anna Kikwa katika taarifa yake aliyoisambaza kwa vyombo vya habari. Aidha amemtaka mkuu wa nchi awafute kazi watendaji wanaotumia vibaya fedha za umma na kuwaongezea wananchi umasikini, ili iwe fundisho kwa watendaji wa Serikali wenye tabia kama hiyo na wachukuliwe hatua za kisheria.

Hata hivyo TGNP imeishauri Serikali kuboresha mifumo ya kusimamia rasilimali za nchi yetu ili wananchi wote waweze kufaidi keki ya taifa kwa sababu mara zote Serikali imekuwa ikisema Tanzania hatuna rasilimali lakini hali halisi ni kwamba rasilimali za taifa zinaliwa na mafisadi wachache wa ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, mtandao huo umetoa pongezi kwa wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu, Ardhi Maliasili na Utalii kwa kusimamia vema na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za serikali zinazotokana na walipa kodi na kuwasilisha ripoti zao Bungeni ambazo zimeibua uozo mkubwa na kujenga mjadala mpana unaotaka uwajibikaji kwa wanaohusika.
“Tunawapongeza pia baadhi ya wabunge  walioshiriki katika mijadala  kwa kuzijadili ripoti hizo kwa undani bila kujali urafiki, itikadi za kisiasa, hasa ile ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa  kuibua  uozo uliojificha na kusimamia maslahi ya Taifa.” amesema Bi. Kikwa katika taarifa hiyo.
“Tumeshuhudia mara kadhaa kupitia vyombo vya habari  wabunge wakiacha itikadi zao za kisiasa na kusimamia kwa dhati dhana ya kushinikiza uwajibikaji katika vyombo vinavyohusika kutokana na ufisadi kama Richmond, Dowans nk. Hata hivyo, TGNP kwa muda mrefu tumekuwa tukipinga ubadhirifu wa fedha za umma  na kudai haki ili kutokomeza ufisadi uliokithiri, lakini bado ufisadi umezidi kushamiri hasa katika Wizara na taasisi za umma.
“Sisi kama wanaharakati tunasema kuendelea kwa ufisadi ni aibu kwa serikali iliyoko madarakani, TGNP tuko mstari wa mbele  kushinikiza rasilimali za taifa ziwanufaishe wananchi wote, hasa walioko pembezoni, kamwe hatutanyamazia aina yoyote ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya wananchi zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.” Imesema taarifa hiyo.
"Tumeshuhudia wanawake na wasichana wakiendelea kuwa maskini na kukumbana na mifumo kandamizi kwa kukosa haki za kufikia huduma za msingi kama vile maji, barabara, afya, elimu, kilimo, utawala bora n.k. Fedha zinazopotea zinatokana na kodi za wananchi na jamii ina haki ya kuhoji uwajibikaji na wahusika wanatakiwa kuchukuliwa  hatua za kisheria," imeongeza taarifa hiyo kwa vyombo vya habari.
Vilevile tunawapongeza wabunge wote walioshiriki kwa dhati katika zoezi la kusaini kusudio la kutaka viongozi waliotajwa/kutuhumiwa  kwenye ripoti hizo kuwajibika. Ili kuonesha dhana ya uwajibikaji na utawala bora unaozingatia misingi ya haki za binadamu.
Kutoka Fullshangwe