Thursday, April 26, 2012

Waziri Akiri Kununua Nyumba Ya Mamilioni


Waziri Akiri Kununua Nyumba Ya Mamilioni


NI EZEKIEL MAIGE, ADAI ALIINUNUA KWA DOLA 410,00, LEMBELI APINGA, ASEMA ALIINUNUA KWA DOLA 700,000 TASLIMU
Fidelis Butahe na Daniel Mjema
SIKU chache baada ya gazeti hili kuripoti taarifa za uchunguzi kwamba kuna mawaziri wawili ambao wamenunua nyumba mbili zenye thamani ya Sh1.8 bilioni, mmoja wa mawaziri hao, Ezekiel Maige wa Maliasili na Utalii ameibuka na kukiri.Maige aliliambia gazeti hili jana kuwa nyumba yake hiyo iliyoko Mbezi Beach, Dar es Salaam, ameinunua kwa Dola za Marekani 410,000 (takriban Sh656 milioni) ambazo anadai kuwa ni mkopo kutoka Benki ya CRDB.

Waziri wa Maliasili na Utalii,Ezekiel Maige
Hata hivyo, wakati Waziri Maige akieleza kuwa nyumba hiyo ina thamani hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli amedai kuwa taarifa alizonazo ni kwamba ilinunuliwa kwa fedha taslimu Dola 700,000 za Marekani (takriban Sh1.1 bilioni).

Awali, habari zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa Waziri Maige alinunua nyumba hiyo kutoka kwa Kampuni ya Savana Real Estate.

Mmoja wa madalali wanaouza nyumba za kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Athuman (Ustadhi) alilithibitishia gazeti hili kwamba Waziri Maige amenunua nyumba moja kati ya nne zilizoko sokoni.

Hata hivyo, dalali huyo hakutaka kueleza alinunua nyumba hiyo lini na kwa gharama gani baada ya kueleza kuwa yeye si msemaji wa kampuni hiyo.

“Nyumba zipo nne na mbili zimeshauzwa. Maige kanunua nyumba moja. Nyumba nyingine mbili bado hazijauzwa na kwa sasa tunamalizia kuziwekea milango na bustani,” alisema Athuman.

Akizungumza na gazeti hili jana, Waziri Maige alisema hakununua nyumba hiyo kwa Dola 700,000 kama inavyodaiwa, bali alinunua kwa Dola za Marekani 410,000.Mbali ya kukiri, alifafanua jinsi alivyoinunua na kuonyesha nyaraka mbalimbali huku akieleza kuwa sehemu ya fedha alizonunulia, zilikuwa za mkopo kutoka Benki ya CRDB.

Alisema mwaka 2005 alipoanza kuwa mbunge alipata mkopo na yeye na wenzake watatu, waliunda kampuni ya kusafirisha mzigo ya Splendid Logistic na kuanza kununua magari matatu na baadaye magari hayo yaliongezeka na kufikia saba.

Soma zaidi:http://www.mwananchi.co.tz