Thursday, May 24, 2012

MNYIKA MBUNGE HALALI JIMBO LA UBUNGO


Flaviani Matata amwaga chozi Kumbukumbu MV Bukoba







Flaviani Matata akishindwa kujizuia na kuangua kilio wakati wa ibaada ya kumbukumbu ya miaka 16 ya ajari ya meli ya MV Bukoba alipotembelea baadhi ya makaburi ya watu waliopoteza maisha katika ajari hiyo yaliyopi Igoma jijini Mwanza, katika ajali hiyo Flaviana alimpoteza pia mama yake mzazi.

CAG KUFUATILIA FEDHA ZA WAATHIRIKA MBAGALA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufuatilia Sh milioni 216 zilizotokana na michango ya taasisi na watu mbalimbali kwa ajili ya waathirika wa mabomu ya Mbagala ambapo zaidi ya Sh bilioni 9 zimelipwa hadi kufikia sasa.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, John Cheyo, alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati wa ziara iliyofanywa na Kamati hiyo, kutembelea maeneo mbalimbali yaliyoathirika na milipuko ya mabomu hayo iliyotokea mwaka 2009 kwa lengo la kujiridhisha na fidia iliyokuwa imetolewa kwa ajili ya waathirika hao.

Akizungumzia fedha hizo pamoja na zingine Sh milioni 48 zinazodaiwa kulipwa kwa watu ambao hawakufanyiwa tathmini yoyote, Cheyo alisema ni vizuri kama Ofisi ya CAG itafanya uchunguzi wa fedha hizo ili kujua zimekwenda wapi au zimetumikaje.

“Tumeambiwa kuwa kumbukumbu nzima ya fedha hizi zipo kwa RAS (Katibu Tawala wa Mkoa), hivyo ni vyema Mkaguzi Mkuu akafuatilia hili kujua kama kuna aina yoyote ya dosari iliyojitokeza,” alisema Cheyo.

Kauli ya Cheyo imetokana na Mwenyekiti wa Kamati ya Waathirika wa Mabomu hayo, Steven Gimange kumwomba Mwenyekiti huyo kusaidia kubaini michango ya fedha hizo sambamba na vitu mbalimbali vilivyotolewa mara baada ya milipuko hiyo huku vikidaiwa kutowafikia walengwa.

Mbali na hatua hiyo, Cheyo ameagiza pia uchunguzi ufanyike katika fedha mbalimbali zilizolipwa kwa waathirika hao zikiwamo Sh milioni 185 zinazodaiwa kulipwa zaidi tofauti na tathmini iliyofanywa.

Awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo, alisema hadi kufikia sasa, Sh bilioni 9 zimelipwa kwa wakazi zaidi ya 10,000 baada ya tathmini mbili kufanyika, huku wakikusudia kumaliza mchakato huo baada ya kukamilisha tathmini ya tatu hivi karibuni.

 

HATIMA YA MNYIKA LEO

HATIMA ya Mbunge wa Ubungo John Mnyika (Chadema) itajulikana leo wakati Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam itakapotoa hukumu ya kesi ya uchaguzi inayomkabili.

Kesi hiyo namba 107 ya mwaka juzi ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hawa Ng’humbi akipinga matokeo yaliyompa ushindi Mnyika katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 kwa madai taratibu na sheria ya uchaguzi zilikiukwa.

Jaji Upendo Msuya anatarajiwa ama kutengua ubunge wa Mnyika au kumtangaza kuwa mbunge halali wa jimbo hilo leo asubuhi mahakamani.

Katika kesi hiyo, Ng’humbi ana hoja tano za msingi ambazo ni kuwepo kwa tuhuma za kashfa kuwa aliuza jengo la Umoja wa Wanawake, kubadilishwa kimakosa kwa kura katika fomu za matokeo ya ubunge, kuwepo kwa watu kimakosa katika chumba cha majumuisho ya kura .

Hoja nyingine ni matumizi ya kompyuta za Mnyika wakati wa majumuisho ya kura na ukiukwaji wa taratibu za kisheria katika uchaguzi huo ambao ulisababisha kuwepo kwa kura hewa 14,854 .

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na upande wa mdai, katika fomu ya matokeo jumla ya kura halisi zilizoandikwa ni 119,823 lakini ukijumlisha kura za wagombea wote unapata kura 132,493 na ukitoa kura halisi na jumla ya kura za wagombea zinabaki kura 14,854.

Wakili wa Ng’humbi Issa Maige alidai kuwa licha ya upande wa wadaiwa kukiri kuwepo kwa kura hewa zaidi ya 14,000 ulishindwa kutoa maelezo ya kina na ufafanuzi kuhusu hizo kura zilitoka wapi na kuiomba Mahakama kubatilisha matokeo hayo.

Wakili wa Mnyika Edson Mbogoro na Wakili Mkuu wa Serikali Justus Mulokozi, waliiomba Mahakama itupilie mbali madai ya Ng’humbi wakidai kuwa ameshindwa kuthibitisha madai yake kwa kiwango kinachokidhi kisheria.

Walidai Ng’humbi alishindwa kuthibitisha hoja alizozitoa; ziliathiri vipi matokeo ya uchaguzi katika jimbo hilo na hata kama kura zilizozidi akipewa Ng’humbi haziwezi kumpa ushindi.

Wakili Mbogoro aliitumia hukumu ya kesi ya uchaguzi wa ubunge wa jimbo la Segerea iliyokuwa imefunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Fred Mpendazoe dhidi ya Mbunge wa jimbo hilo Dk. Makongoro Mahanga wa CCM.

Walalamikiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wasimamizi wasaidizi na Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi ambao wanatetewa na Wakili Mkuu wa Serikali Justus Mulokozi huku Mnyika akitetewa na Mbogoro.

 

Wasira apanda kizimbani

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira juzi alipanda kizimbani kutoa ushahidi katika kesi ya kupinga matokeo yaliyompatia ushindi Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu katika Uchaguzi Mdogo uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Akiongozwa na Wakili wa upande wa utetezi, Kayaga Kamaliza mbele ya Jaji Mary Shangali, Wasira alikanusha madai kuwa CCM ilitoa ahadi ya kugawa mahindi kwa baadhi ya sehemu jimboni humo ili ichaguliwe katika uchaguzi huo.

Alipotakiwa na Wakili Kamaliza kueleza alishiriki vipi katika uchaguzi huo, Wasira alidai kuwa alishiriki kama mpiga kampeni wa CCM na kutaja baadhi ya viongozi alioshirikiana nao kuwa ni Mweka Hazina wa chama hicho, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde.

“Tulishiriki viongozi wengi tu wa chama akiwepo Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Mtera, Lusinde na wengine wengi,’’ alidai Wasira na kueleza kuwa alikwenda katika uchaguzi huo kichama, hata mavazi yake hayakuwa ya kiserikali kwani alitumia nguo za chama kwa muda wote aliokuwa akiishi hapo Igunga.

Kuhusu hoja za wakili wa upande wa mlalamikaji, Profesa Abdallah Safari, kuwa Igunga alienda kama nani, cheo chake cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais alimkabidhi nani na alijitambulisha katika mkutano kama nani, Wasira alijibu kuwa uwaziri haukabidhiwi kwa mtu.

Alisisitiza kuwa Igunga alikwenda kama kiongozi wa CCM, Mjumbe wa Kamati Kuu na cheo chake hakukikabidhi kwa mtu yeyote kwa kuwa cheo hicho huwa hakikabidhiwi, lakini alipata ruhusa. Kuhusu kujitambulisha, Wasira alidai kuwa alijitambulisha kama Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.

Akijibu madai kwamba CCM ilikuwa ikitoa ahadi ya mahindi katika baadhi ya kata na ahadi ya ujenzi wa daraja la Mbutu mmoja ya mambo makubwa yanayotazamwa katika kesi hiyo, alidai hakutoa ahadi hizo.

“Mimi siwezi kugawa mahindi, huo ni uongo, ni uzushi tu kabisa pia Chama Cha Mapinduzi hakina mahindi, ni chama cha kisiasa… waliotoa ushahidi huo ni waongo sijatoa ahadi yoyote inayohusu mahindi,” alieleza na kuongeza kuwa ahadi ya ujenzi wa daraja la Mbutu ipo katika llani ya Uchaguzi wa mwaka 2010 ya CCM.

Awali kabla ya Wasira kutoa ushahidi huo, Msimamizi wa Uchaguzi huo, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Protace Magayane alitoa ushahidi. Alitumia zaidi ya saa saba kizimbani kufafanua hoja mbalimbali ikiwamo madai ya CCM kutoa mahindi na kukiukwa maadili ya uchaguzi.

   
                                             

VIJANA KUMJADILI SHIBUDA

WAKATI mpasuko ndani ya Chadema ukiwaumiza kichwa viongozi wa chama hicho, Sekretarieti ya Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA), inakutana leo kama ilivyoahidiwa mwanzoni mwa wiki hii.

Taarifa ya Katibu wa Bavicha, Deogratias Siale iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa katika kikao hicho kilichoitwa cha kawaida, kutajadiliwa mada zinazohusu mustakabali wa vijana wa Tanzania.

Hata hivyo, pamoja na taarifa hiyo kutokuelezea chochote kuhusu mpasuko unaoendelea ndani ya Chadema ulioanzia Bavicha, mkutano wa leo unatarajiwa kutekwa na mjadala kuhusu mpasuko huo.

Mjadala wa mpasuko huo ni dhahiri kuteka kikao hicho leo hasa baada ya viongozi wa juu wa baraza hilo; Mwenyekiti, John Heche na makamu wake, Juliana Shonza kutofautiana hadharani.

Chanzo cha mpasuko Mpasuko huo wa Chadema ulioanzia Bavicha, ulitokana na kauli ya Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda kutangaza nia ya kugombea urais 2015 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na kuweka wazi kuwa angependa Rais Jakaya Kikwete awe meneja wa kampeni yake kwa kuwa atakuwa akimaliza muda wake.

Shibuda alitangaza nia hiyo alipoalikwa katika kikao cha NEC kama mmoja wa wajumbe wa Mpango wa Afrika wa Kujitathimini Kiutawala Bora (APRM), anayewakilisha Bunge. APRM katika kikao hicho ilialikwa kutoa semina kuhusu utawala bora.

Baada ya kauli hiyo, Heche alimjibu na kusema Bavicha haitamruhusu Shibuda kugombea urais kwa kuwa ametangaza nia hiyo akiwa katika kikao cha CCM na kumtaka Rais Kikwete kuwa meneja wa kampeni zake.

“Kauli hii tunaamini vijana wa Chadema, kuwa mamlaka za nidhamu hazitakaa kimya na kuiachia bila kutakiwa maelezo ya kina, tutaitisha kikao cha Baraza na tutaijadili na kuwasilisha mapendekezo yetu kwenye vikao halali vya chama,” ilisema taarifa ya Bavicha ilyosainiwa na Heche.

Heche katika taarifa hiyo, aliwataka vijana wote Chadema wajiandae kukabiliana na mtu yeyote atakayeonekana kuwa kikwazo kwa chama chao kuelekea kuchukua Dola mwaka 2015.

Baada ya kauli hiyo, Shibuda aliitaka Bavicha kumuomba radhi kwa kuwa alitumia haki yake ya kidemokrasia kutangaza nia na kutishia kuwa isipofanya hivyo, atatumia mbinu ya Chadema ya kuishitaki Serikali kwa wananchi, kuigeuzia kibao Bavicha na kuishitaki kwa wananchi.

Kitisho hicho cha Shibuda, kilimuibua Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Juliana Shonza aliyesema kuwa Heche alitoa kauli binafsi na haihusu Bavicha na kuhoji kwa nini Shibuda asulubiwe kwa kauli hiyo wakati hata Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto alitangaza nia na hakushughulikiwa.

Shonza alisema Heche hakufuata utaratibu unaoongoza baraza hilo wala hakushirikisha viongozi wowote wa juu wa chama na sekretarieti ya baraza, jambo alilosema limekichafua Chama na Baraza.

“Mimi kama Makamu Mwenyekiti, siwezi kuvumilia kukaa na kaa la moto mfukoni, na hili naliongea kutaka kuweka wazi kwamba tamko alilotoa John Heche sio la baraza bali ni tamko lake, na mimi kama kiongozi wa juu nina ujasiri na uhalali wa kisiasa na kisheria wa kutamka hili,” alisema.

Heche ashughulikiwe Kutokana na msimamo huo, Shonza alimshauri Shibuda ashughulike na Heche mwenyewe, badala ya kutaka baraza kumuomba radhi wakati halihusiki na kauli hiyo. Shonza alisema kama Shibuda alikuwa amekosea, Heche angeshauriana na baraza na kwenda kuzungumza na mhusika badala ya kukejeli hadharani.

“Hatutavumilia kumwona kijana wa chama, kiongozi wa ngazi yoyote ndani ya chama kulitumia baraza kwa ajili ya kufikisha matamanio ya fikra zake, tutalinda baraza kulingana na mwongozo wa baraza,” alisema Shonza aliyedai ametoa kauli hiyo kama yeye na si baraza. Bavicha kushughulikiana

Kauli hiyo ya Shonza ilimuibua tena Heche ambaye aliitisha kikao cha kushauriana na Katibu Mkuu wa Bavicha, Siale ambaye baada ya mashauriano ambayo hayakumhusisha Shonza, Siale alituma taarifa katika vyombo vya habari kuitisha kikao cha Sekretariati ya Bavicha leo.

Kikao hicho kwa mujibu wa Siale, ni kwa ajili ya kujadili na kuwasilisha mapendekezo kuhusu kauli ya Shibuda katika vikao halali vya chama kwa ajili ya hatua zaidi.

Hata hivyo, taarifa iliyotumwa jana katika vyombo vya habari, haikuzungumza chochote kuhusu mpasuko huo na badala yake ikajikita zaidi kujadili masuala ya kawaida.

“Sekretarieti ya Bavicha inakutana wakati ambapo hali na mustakabali wa vijana inazidi kuwa tete. Tatizo la ukosefu wa ajira limeendelea kuota mizizi. Vijana wengi, wakiwemo wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu, ikiwemo vyuo hawajui wafanye nini, maana hakuna fursa zinazotengenezwa ili wazitumie kujitafutia maendeleo yao na maendeleo ya taifa kwa ujumla,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilidai kuwa Serikali iliyoko madarakani, chini ya CCM imepoteza mwelekeo katika kushughulikia matatizo yanayowakabili vijana, hususan hili la ajira.

“Sera na mikakati yake imekuwa ni ya kubabaisha ama haitekelezeki. Hivyo kama Bavicha tunapokutana katika kikao cha kawaida cha Sekretarieti tutatoa mawazo ya nini kifanyike katika hali hii ambayo vijana sasa nchini wanakumbana nayo,” ilieleza taarifa hiyo.

Baada ya kikao hicho kwa mujibu wa taarifa hiyo, mawazo yatawasilishwa kwa wabunge wa Chadema ili kupitia Bunge la Bajeti watoe ushauri mbadala na kuiagiza Serikali ya CCM, hatua gani zinatakiwa kuchukuliwa kunusuru kundi la vijana kwa ajili ya maendeleo ya jamii yoyote ile.

Wakati Chadema wakivurugana, CCM imeelezea kusubiri chochote kitakachotokea na ikiwa Shibuda atavuliwa uanachama, kirejee Maswa Magharibi kwa uchaguzi mdogo.

Katibu wa CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema hayo wakati akiunga mkono kauli ya wanachama wa CCM katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu waliodai kuwa iwapo Chadema, kitamvua uanachama na kumfukuza Shibuda watahakikisha kuwa Jimbo hilo linanyakuliwa na chama hicho.

Nape alisema jimbo hilo ni lao, kwani kuna makosa yalifanyika wakati wa uchaguzi mkuu uliopita ambayo wameyabaini na kuyafanyia marekebisho.

“Iwapo Chadema itamfukuza Shibuda na jimbo likawa wazi nawahakikishieni ya kuwa ni lazima tulinyakue kwani katika Uchaguzi Mkuu uliopita sisi Wana CCM katika majimbo yote mawili ya Maswa Mashariki na Maswa Magharibi wagombea wetu wa ubunge walikuwa hawakubaliki kwa wananchi ndio maana tulishindwa vibaya,” alisema Hassan Tindo, mmoja wa wanachama wa CCM.

Mwanachama mwingine, Nuru Mselemo alisema sasa wanao ushirikiano kuanzia ngazi ya shina hadi wilaya na kuongeza kuwa ana uhakika wa kufanya vizuri.

Mnyika apuuza Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alipohojiwa, alisema kuna mambo ya msingi ya uchumi, siasa na jamii yanayopaswa kupewa kipaumbele kuliko hilo na kutaka kiongozi wa Chadema wa Maswa azungumzie hali hiyo.

Katibu wa Chadema wilayani Maswa, Luhende Mipawa alipohojiwa naye alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia chochote kuhusu suala hilo na kuwataka CCM kuacha kufanya kazi kwa kupiga ramli.

“Suala hilo mimi siwezi kulizungumzia kwa sasa kwani liko katika ngazi za juu la vikao vya chama na utaratibu wetu Chadema mambo yetu yote tunayamalizia kwenye vikao hao wanaodai Shibuda atafukuzwa waache kufanya kazi kw

MSAIDIZI WA KAZI ZA NDANI ALIYETUHUMIWA KUUA MTOTO AKAMATWA

MSICHANA wa kazi za ndani anayetuhumiwa kumuua mtoto wa bosi wake, juzi usiku alinusurika kudhuriwa baada ya kukamatwa na bosi wake aliyejulikana kwa jina moja la Mama Angel.

Gazeti hili lilishuhudia msichana huyo mwenye umri wa miaka 17 (jina limehifadhiwa), akikamatwa juzi saa 6 usiku Sinza nyumbani kwa Mama Angel. Baada ya kukamatwa, majirani wa Mama Angel ambao walishiriki msiba wa mtoto huyo, walishirikiana kutaka kumchukulia sheria mkononi.

Inadaiwa kuwa msichana huyo alisababisha kifo cha mtoto huyo wa miezi saba wakati Mama Angel akiwa kazini Machi mwaka huu na kutoroka nyumbani hapo.

Kijana wa mwenye nyumba hiyo, Ally Hasan alidai alikuwa wa kwanza kugundua kuwa mtoto huyo amekufa baada ya Mama Angel kumpigia akimuomba kumuangalizia mtoto wake huyo aliyekuwa amemuacha amelala.

Hasan alidai alipoingia ndani ya chumba cha Mama Angel, alimkuta mtoto huyo akiwa amelala na hakugundua kuwa alikuwa ameshakufa.

Kwa mujibu wa madai ya Hasan, alitoa taarifa kwa Mama Angel kuwa mwanawe amelala na mama huyo alimuomba amuamshe ndipo alipogundua kuwa amekufa baada ya kuona haamki na kulazimika kutoa taarifa kwa mama mwenye mtoto alirudi nyumbani haraka.

Alidai kuwa mama wa mtoto huyo alipofika na kukuta mtoto ameshakufa kwa kushirikiana na majirani walitoa taarifa Polisi na kumzika.

Hasan alidai walianza harakati za kumtafuta msichana huyo wa kazi na kila walipompigia simu yake, inadaiwa alikuwa akiwajibu kimkato huku akikiri kuwa ameua mtoto huyo.

Naye Mama Angel akizungumza na gazeti hili juzi usiku, alidai alifunga kula na akaamua kufanya ibada kumuomba Mungu amuoneshe alipo msichana huyo, ndipo juzi alipokuwa akipita eneo la Mwananyamala akiwa na mumewe, wakamuona akiwa mtaani.

Alidai kuwa baada ya kumuona, walimkamata na wakampandisha katika teksi na kumpeleka nyumbani kwao Sinza ili kumhoji zaidi.

Mwandishi wa gazeti hili aliyekuwa eneo la tukio wakati dada huyo akishushwa, alimshuhudia mfanyakazi huyo akilumbana na Mama Angel ambapo alimng’ata mama huyo katika bega hali iliyozua tafrani baada ya majirani wa mama huyo kujitokeza kwa wingi kumsaidia.

Baada ya tafrani hiyo, msichana huyo wa kazi aliokolewa na wanaume waliokuwa eneo la jirani ambao walimkamata na kumpeleka nyuma ya nyumba wakamzunguka na kumlinda asidhurike na akinamama hao ambao wengi walikuwa wakidai kama msichana huyo amesababisha kifo, iweje yeye asiuawe.

Mama mzazi wa mtoto huyo akiwa mwenye uchungu, alisikika akieleza kuwa binti huyo anapaswa kuchukuliwa hatua kwa mauaji ya mwanawe, huku akitaka kumuadhibu. Hata hivyo, wanaume waliokuwapo walizuia msichana huyo wa kazi asidhuriwe.

Baadhi ya watu walipomhoji kuhusu kifo cha mtoto huyo, msichana huyo ambaye awali alionesha ujeuri kwa kusema watamfanya nini, baadaye alikuwa mpole na kudai mtoto huyo alimuacha ndani na hajui kilichomkuta.

Baada ya saa moja, waliwasili askari Polisi wa Kituo cha Polisi Mabatini eneo la Sinza waliomchukua na kuondoka naye huku wananchi waliokuwapo nje wakitaka kumdhuru.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alipoulizwa, alisema analifuatilia suala hilo na atatoa taarifa baadaye.