WAZIRI wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira juzi alipanda
kizimbani kutoa ushahidi katika kesi ya kupinga matokeo yaliyompatia
ushindi Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu katika Uchaguzi Mdogo
uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.
Akiongozwa na Wakili wa upande wa utetezi, Kayaga Kamaliza mbele ya
Jaji Mary Shangali, Wasira alikanusha madai kuwa CCM ilitoa ahadi ya
kugawa mahindi kwa baadhi ya sehemu jimboni humo ili ichaguliwe katika
uchaguzi huo.
Alipotakiwa na Wakili Kamaliza kueleza alishiriki vipi katika
uchaguzi huo, Wasira alidai kuwa alishiriki kama mpiga kampeni wa CCM
na kutaja baadhi ya viongozi alioshirikiana nao kuwa ni Mweka Hazina wa
chama hicho, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde.
“Tulishiriki viongozi wengi tu wa chama akiwepo Mwigulu Nchemba na
Mbunge wa Mtera, Lusinde na wengine wengi,’’ alidai Wasira na kueleza
kuwa alikwenda katika uchaguzi huo kichama, hata mavazi yake hayakuwa
ya kiserikali kwani alitumia nguo za chama kwa muda wote aliokuwa
akiishi hapo Igunga.
Kuhusu hoja za wakili wa upande wa mlalamikaji, Profesa Abdallah
Safari, kuwa Igunga alienda kama nani, cheo chake cha Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais alimkabidhi nani na alijitambulisha katika mkutano kama
nani, Wasira alijibu kuwa uwaziri haukabidhiwi kwa mtu.
Alisisitiza kuwa Igunga alikwenda kama kiongozi wa CCM, Mjumbe wa
Kamati Kuu na cheo chake hakukikabidhi kwa mtu yeyote kwa kuwa cheo
hicho huwa hakikabidhiwi, lakini alipata ruhusa. Kuhusu kujitambulisha,
Wasira alidai kuwa alijitambulisha kama Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Akijibu madai kwamba CCM ilikuwa ikitoa ahadi ya mahindi katika
baadhi ya kata na ahadi ya ujenzi wa daraja la Mbutu mmoja ya mambo
makubwa yanayotazamwa katika kesi hiyo, alidai hakutoa ahadi hizo.
“Mimi siwezi kugawa mahindi, huo ni uongo, ni uzushi tu kabisa pia
Chama Cha Mapinduzi hakina mahindi, ni chama cha kisiasa… waliotoa
ushahidi huo ni waongo sijatoa ahadi yoyote inayohusu mahindi,”
alieleza na kuongeza kuwa ahadi ya ujenzi wa daraja la Mbutu ipo katika
llani ya Uchaguzi wa mwaka 2010 ya CCM.
Awali kabla ya Wasira kutoa ushahidi huo, Msimamizi wa Uchaguzi
huo, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Igunga, Protace Magayane alitoa ushahidi. Alitumia zaidi ya saa saba
kizimbani kufafanua hoja mbalimbali ikiwamo madai ya CCM kutoa mahindi
na kukiukwa maadili ya uchaguzi.
|