Utouh kukagua mahesabu Umoja wa Mataifa |
New York IKIWA imebaki takribani miezi miwili kabla ya Tanzania kupitia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ( NAOT) kuingia rasmi katika Ujumbe wa Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa ( UNBOA). Mkuu wa chombo hicho, Ludovick Utouh amesema yeye na ofisi yake wamejipanga vema kulikabili jukumu hilo. Utouh alisema hayo juzi wakati alipofanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , Asha- Rose Migiro alipomtembelea ofisini kwake. Utouh yupo hapa Umoja wa Mataifa akifuatana na wasaidizi wake watatu kwa ziara ya kikazi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awali kujiunga na bodi hiyo. Katika mazungumzo hayo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali, alimhakikishia Naibu Katibu Mkuu kwamba anatambua ukubwa wa kazi inayomkabili mbele yake, na dhamana anayoibeba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Watanzania wote. “Tanzania tumeaminiwa, sifa zetu zinafahamika na ndiyo maana tukapendekezwa kuingia kwenye bodi hii . Tumejiandaa na kujipanga, tutatumia uwezo wetu na maarifa yetu kulikabili jukumu hili na heshima hii tuliyopewa” alisisitiza Utouh. Alisema yeye na wataalamu wake, na kwa kushirikiana na wajumbe wengine wa bodi hiyo, watalitekeleza jukumu hilo kwa uwazi na siyo kuviziana. “Tumejipanga kuifanya kazi hii kwa misingi na taratibu zote zilizoweka , tutafanya ukaguzi kwa uwazi, tutajadiliana na wahusika, na siyo kuviziana lengo ni kuboresha utendaji wa chombo hiki muhimu” alisisitiza. Alibainisha zaidi kwa kusema, ukaguzi wa kuviziana na kuumbuana umeshapitwa na wakati. “Ukaguzi wa kuviziana ni wa kizamani hata nyumbani ( Tanzania) hatufanyi aina hiyo, tumeendelea, tunafanya ukaguzi wa viwango, tunajadiliana , kuelekezana na siyo kuviziana au kukomoana tunataka kujenga na si kubomoa” alisisitiza. Katika mazungumzo hayo, Naibu Katibu Mkuu Asha- Rose Migiro alimpongeza Utouh, ofisi yake na Serikali kwa ujumla kwa kupata fursa hiyo ya kuingia kwenye Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa. Akasema kuwa, Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa katika Bara la Afrika katika eneo hilo la ukaguzi wa mahesabu kiasi cha kutambuliwa na Umoja wa Mataifa. Mwishoni mwa mwaka jana, Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa lilipitisha uteuzi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa. Tanzania inachukua nafasi inayoachwa wazi na Afrika ya Kusini Julai mwaka huu na itafanya kazi na wajumbe wengine wawili wa bodi hiyo kutoka Uingereza na China. |