TAARIFA za kwamba Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), imebaini
kuwa Jeshi la Polisi lina askari 700 wenye majina yanayofanana na
waajiriwa wengine serikalini huku Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
likiwa na askari 248 zimeshtua taifa.
Taarifa hizi za kutisha
zilipatikana baada ya Nida kuanza utekelezaji wa kuwapatia wafanyakazi
wa Serikali vitambulisho vya taifa katika Jiji la Dar es Salaam kabla
ya kuwapatia watu wa kada nyingine nchini kote.
Kutokana na
uchambuzi wa Nida, polisi na wanajeshi hao wamebainika kutumia cheti
kimoja na wafanyakazi wengine wa Serikali kitendo ambacho ni kosa la
kisheria.
Kutokana na jambo lenyewe kuwa nyeti na ambalo
litakiwa kufanyiwa ufuatiliaji wa haraka, tayari Jeshi la Polisi
limeunda tume ya kuchunguza kashfa hii ya vyeti ndani ya taasisi yake.
Hakika
ni jambo lisiloweza kufikirika kwamba taasisi zetu muhimu za kulinda
raia na mali zao, kulinda mipaka yetu zina wafanyakazi ambao hawana
maadili kiasi cha kuthubutu kughusi vyeti kwa lengo la kupata ajira.
Tunaamini
kwamba watumishi wa aina hii si hatari ndani ya jeshi, lakini ni
hatari kwa raia kwani wanaweza kufanya lolote hata kama linakiuka
maadili ya kazi zao kwa kuwa wao wameweka maslahi binafsi mbele,
uadilifu wa kazi wameuweka kando.
Ndio maana leo katika majeshi
yetuna idara kadhaa za Serikali kuna watumishi wengi wasio na maadili
kazini kwa kuwa hawajasomea fani husika, bali wametumia njia za hila
kupata ajira hizo kama Nida walivyobaini.
Ndio maana
tunawapongeza Nida kwa kuweza kugundua kashfa ambayo huenda ikawakumba
wengi zaidi hasa pale ambapo wataanza kutoa vitambulisho nchi nzima na
hasa kwenye Halmashauri za Wilaya ambako tunaambiwa kuwa kuna idadi
isiyo na kifani ya watu wanaotumia vyeti vya watu wengine, wakiwamo
walio hai na waliokufa.
Idadio hii kubwa ya waajiriwa wa Serikali
wamefanya udanganyifu mkubwa na wanachostahili baada ya uchunguzi
kukamilika ni kufukuzwa kazi na kufunguliwa kesi za jinai kwa kughushi
ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kufanya mchezo mchafu kama
huo.
Kwa kuwa Nida wamefanya uandikishaji wa watumishi wa
Serikali katika Jiji la Dar es Salaam pekee, tunaamini kwamba kashfa
hii si tu polisi na wanajeshi pekee bali itagusa maeneo yote.
Mbaya
zaidi kashfa za kutumia vyeti bandia huenda vikaikumba sekta ya elimu
ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikilalamikiwa kwamba elimu inayotelewa na
baadhi ya walimu haikidhi viwango halisi.
Matokeo yake, wanafunzi
wengi wanaomaliza elimu ya msingi nchini hawajui kusoma wala kuandika
na kibaya zaidi kuna wengine wenye udhaifu huo wanachaguliwa kuendelea
na elimu ya sekondari.
Sote tumeshuhudia askari wengi wakifanya kazi
chini ya kiwango kumbe kuna tatizo la msingi nalo ni kutokuwa na elimu
inayoendana na kazi wanayoifanya.
Lakini jambo muhimu la
kujiuliza inakuwaje vyombo vya usalama ambavyo vina mkono mrefu
vimeshindwa kufuatilia hawa watu kama kweli vyeti wanavyomiliki ni
vyao? Je ndani ya vyombo vyetu vya usalama watumishi wote ni raia au
kuna wageni? Yote haya ni majibu ambayo tume ya polisi inapaswa kuweka
wazi kwa wananchi.
Tunadhani Serikali na vyombo vya dola
vitachukulia sakata hili kwa umakini mkubwa ili wale wote wanaohusika
waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Ni maoni yetu kwamba
wafanyakazi wote ambao wamegushi vyetu vyao na kuajiriwa serikalini na
katika sekata binafsi waachie ngazi mara moja na hatua za kisheria
zianze dhidi yao kwa uvunjaji wa maadili ambao katu hauvumiliki.
source Mwananchi