Mwandishi Wetu
MAREKANI imeungana na Uingereza kushinikiza
kutambuliwa kwa haki za mashoga, ikitumia rungu la misaada yake
inayotoa kwa nchi mbalimbali duniani, huku ikitenga Dola za Marekani 3
milioni sawa na Sh5.1bilioni, kwa ajili ya kufanikisha mkakati huo.
Shinikizo
hilo la Marekani ambalo ni taifa kubwa kiuchumi duniani, linazidi
kuchochea mjadala ulioibuliwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David
Cameron, ambaye alitangaza katika mkutano wa Jumuiya ya Madola
uliofanyika Uswis hivi karibuni kwamba, nchi yake itasitisha misaada
kwa nchi zote duniani ambazo hazitambui haki za mashoga.
Baada
ya Cameron, Rais Barack Obama wa Marekani naye juzi alitangaza kwamba,
taifa hilo kubwa litatumia uwezo wake wote ikiwamo misaada inayotoa kwa
nchi mbalimbali kuhakikisha haki za mashoga zinatambuliwa na
kuthaminiwa duniani.
Rais Obama alitoa msimamo huo jijini
Washington katika hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya
Nje wa Nchi hiyo , Hillary Clinton ambaye ndiye alikuwa mzungumzaji
mkuu.
“Wengine wanasema kuwa haki za mashoga na haki za
binaadamu ni vitu tofauti na havifanani, lakini ukweli ni kwamba ni
kitu kimoja na chenye usawa,”alisema Clinton wakati akisoma taarifa
hiyo maalumu yenye baraka za Obama.
Clinton alisema, “Tayari
tumetenga kiasi cha Dola za Marekani 3 Milioni kwa ajili ya programu ya
kutangaza haki za mashoga ili kuondokana na ubaguzi na unyanyasaji
dhidi yao.”
Waziri huyo wa mambo ya nje, alisema mpango huo
unazitaka nchi ambazo sheria zake bado hazitambui haki za mashoga na
kubadilisha sheria hizo ili jamii hiyo ya watu ianze kutambulika.
“Kwa
nchi ambazo watu wanafungwa, kupigwa kutokana na kuwa mashoga ni muhimu
viongozi wa nchi hizo, kuangalia jinsi gani wanaweza kukiangalia
kikundi hicho cha watu. Si kwamba mashoga hawafanyi makosa, wanaweza
kufanya au kutokufanya kama watu wa kawaida, lakini isiwe ni kosa la
jinai mtu kuwa shoga,”alisema.
Kwa mujibu wa Clinton, haki za
mashoga ni haki za kimataifa. "Hazina tofauti na haki za binadamu
zilizotambuliwa na nchi 48 lililotolewa baada ya Vita Kuu ya Pili ya
Dunia.
Naibu Msemaji wa Baraza la Usalama la Marekani, Caitlin
Hayden alisema Serikali ya nchi hiyo si kwamba itapunguza au kuzuia
misaada yake ya kimataifa ili kubadilisha utamadini wa nchi nyingine,
bali inataka kuhakikisha haki za mashoga zinapewa pia kipaumbele.
Hii
ni mara ya kwanza kwa Rais Obama kujitokeza hadharani na kutetea haki
za mashoga, lakini aliwahi kupitisha sera iitwayo “ don’t ask, don’t
tell” ikimaanisha “usiulize, usiseme” ambayo inawazuia mashoga kujiunga
na kufanya kazi za jeshi kwa uwazi.
Mmoja wa viongozi wa
Republican ambaye atawania nafasi ya Urais, Gavana Rick Perry alisema
Obama kwa mara nyingine amewakosea Wamarekani kwa aina tofauti ya
maisha yao kwa kuingiza aina hiyo ya maisha kitu ambacho mtu kama yeye
Perry hawezi kukifanya.
Kauli hiyo ya viongozi wa Marekani
inaonekana kuungana na ile iliyotolewa na Cameron aliyesema, "Hii ni
moja ya vitu vinavyoongoza sera yetu ya misaada kwa mataifa mbalimbali
na tayari tumeanza kuitekeleza katika maeneo kadhaa.