WAKATI mpasuko ndani ya Chadema ukiwaumiza kichwa viongozi wa chama
hicho, Sekretarieti ya Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA),
inakutana leo kama ilivyoahidiwa mwanzoni mwa wiki hii.
Taarifa ya Katibu wa Bavicha, Deogratias Siale iliyotumwa jana kwa
vyombo vya habari, ilieleza kuwa katika kikao hicho kilichoitwa cha
kawaida, kutajadiliwa mada zinazohusu mustakabali wa vijana wa
Tanzania.
Hata hivyo, pamoja na taarifa hiyo kutokuelezea chochote kuhusu
mpasuko unaoendelea ndani ya Chadema ulioanzia Bavicha, mkutano wa leo
unatarajiwa kutekwa na mjadala kuhusu mpasuko huo.
Mjadala wa mpasuko huo ni dhahiri kuteka kikao hicho leo hasa baada
ya viongozi wa juu wa baraza hilo; Mwenyekiti, John Heche na makamu
wake, Juliana Shonza kutofautiana hadharani.
Chanzo cha mpasuko Mpasuko huo wa Chadema ulioanzia Bavicha,
ulitokana na kauli ya Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda kutangaza
nia ya kugombea urais 2015 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya
CCM na kuweka wazi kuwa angependa Rais Jakaya Kikwete awe meneja wa
kampeni yake kwa kuwa atakuwa akimaliza muda wake.
Shibuda alitangaza nia hiyo alipoalikwa katika kikao cha NEC kama
mmoja wa wajumbe wa Mpango wa Afrika wa Kujitathimini Kiutawala Bora
(APRM), anayewakilisha Bunge. APRM katika kikao hicho ilialikwa kutoa
semina kuhusu utawala bora.
Baada ya kauli hiyo, Heche alimjibu na kusema Bavicha haitamruhusu
Shibuda kugombea urais kwa kuwa ametangaza nia hiyo akiwa katika kikao
cha CCM na kumtaka Rais Kikwete kuwa meneja wa kampeni zake.
“Kauli hii tunaamini vijana wa Chadema, kuwa mamlaka za nidhamu
hazitakaa kimya na kuiachia bila kutakiwa maelezo ya kina, tutaitisha
kikao cha Baraza na tutaijadili na kuwasilisha mapendekezo yetu kwenye
vikao halali vya chama,” ilisema taarifa ya Bavicha ilyosainiwa na
Heche.
Heche katika taarifa hiyo, aliwataka vijana wote Chadema wajiandae
kukabiliana na mtu yeyote atakayeonekana kuwa kikwazo kwa chama chao
kuelekea kuchukua Dola mwaka 2015.
Baada ya kauli hiyo, Shibuda aliitaka Bavicha kumuomba radhi kwa
kuwa alitumia haki yake ya kidemokrasia kutangaza nia na kutishia kuwa
isipofanya hivyo, atatumia mbinu ya Chadema ya kuishitaki Serikali kwa
wananchi, kuigeuzia kibao Bavicha na kuishitaki kwa wananchi.
Kitisho hicho cha Shibuda, kilimuibua Makamu Mwenyekiti wa Bavicha,
Juliana Shonza aliyesema kuwa Heche alitoa kauli binafsi na haihusu
Bavicha na kuhoji kwa nini Shibuda asulubiwe kwa kauli hiyo wakati hata
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto alitangaza nia na
hakushughulikiwa.
Shonza alisema Heche hakufuata utaratibu unaoongoza baraza hilo
wala hakushirikisha viongozi wowote wa juu wa chama na sekretarieti ya
baraza, jambo alilosema limekichafua Chama na Baraza.
“Mimi kama Makamu Mwenyekiti, siwezi kuvumilia kukaa na kaa la moto
mfukoni, na hili naliongea kutaka kuweka wazi kwamba tamko alilotoa
John Heche sio la baraza bali ni tamko lake, na mimi kama kiongozi wa
juu nina ujasiri na uhalali wa kisiasa na kisheria wa kutamka hili,”
alisema.
Heche ashughulikiwe Kutokana na msimamo huo, Shonza alimshauri
Shibuda ashughulike na Heche mwenyewe, badala ya kutaka baraza kumuomba
radhi wakati halihusiki na kauli hiyo. Shonza alisema kama Shibuda
alikuwa amekosea, Heche angeshauriana na baraza na kwenda kuzungumza na
mhusika badala ya kukejeli hadharani.
“Hatutavumilia kumwona kijana wa chama, kiongozi wa ngazi yoyote
ndani ya chama kulitumia baraza kwa ajili ya kufikisha matamanio ya
fikra zake, tutalinda baraza kulingana na mwongozo wa baraza,” alisema
Shonza aliyedai ametoa kauli hiyo kama yeye na si baraza. Bavicha
kushughulikiana
Kauli hiyo ya Shonza ilimuibua tena Heche ambaye aliitisha kikao
cha kushauriana na Katibu Mkuu wa Bavicha, Siale ambaye baada ya
mashauriano ambayo hayakumhusisha Shonza, Siale alituma taarifa katika
vyombo vya habari kuitisha kikao cha Sekretariati ya Bavicha leo.
Kikao hicho kwa mujibu wa Siale, ni kwa ajili ya kujadili na
kuwasilisha mapendekezo kuhusu kauli ya Shibuda katika vikao halali vya
chama kwa ajili ya hatua zaidi.
Hata hivyo, taarifa iliyotumwa jana katika vyombo vya habari,
haikuzungumza chochote kuhusu mpasuko huo na badala yake ikajikita
zaidi kujadili masuala ya kawaida.
“Sekretarieti ya Bavicha inakutana wakati ambapo hali na
mustakabali wa vijana inazidi kuwa tete. Tatizo la ukosefu wa ajira
limeendelea kuota mizizi. Vijana wengi, wakiwemo wahitimu wa ngazi
mbalimbali za elimu, ikiwemo vyuo hawajui wafanye nini, maana hakuna
fursa zinazotengenezwa ili wazitumie kujitafutia maendeleo yao na
maendeleo ya taifa kwa ujumla,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilidai kuwa Serikali iliyoko madarakani, chini ya CCM
imepoteza mwelekeo katika kushughulikia matatizo yanayowakabili vijana,
hususan hili la ajira.
“Sera na mikakati yake imekuwa ni ya kubabaisha ama haitekelezeki.
Hivyo kama Bavicha tunapokutana katika kikao cha kawaida cha
Sekretarieti tutatoa mawazo ya nini kifanyike katika hali hii ambayo
vijana sasa nchini wanakumbana nayo,” ilieleza taarifa hiyo.
Baada ya kikao hicho kwa mujibu wa taarifa hiyo, mawazo
yatawasilishwa kwa wabunge wa Chadema ili kupitia Bunge la Bajeti watoe
ushauri mbadala na kuiagiza Serikali ya CCM, hatua gani zinatakiwa
kuchukuliwa kunusuru kundi la vijana kwa ajili ya maendeleo ya jamii
yoyote ile.
Wakati Chadema wakivurugana, CCM imeelezea kusubiri chochote
kitakachotokea na ikiwa Shibuda atavuliwa uanachama, kirejee Maswa
Magharibi kwa uchaguzi mdogo.
Katibu wa CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema hayo wakati
akiunga mkono kauli ya wanachama wa CCM katika Wilaya ya Maswa mkoani
Simiyu waliodai kuwa iwapo Chadema, kitamvua uanachama na kumfukuza
Shibuda watahakikisha kuwa Jimbo hilo linanyakuliwa na chama hicho.
Nape alisema jimbo hilo ni lao, kwani kuna makosa yalifanyika
wakati wa uchaguzi mkuu uliopita ambayo wameyabaini na kuyafanyia
marekebisho.
“Iwapo Chadema itamfukuza Shibuda na jimbo likawa wazi
nawahakikishieni ya kuwa ni lazima tulinyakue kwani katika Uchaguzi
Mkuu uliopita sisi Wana CCM katika majimbo yote mawili ya Maswa
Mashariki na Maswa Magharibi wagombea wetu wa ubunge walikuwa
hawakubaliki kwa wananchi ndio maana tulishindwa vibaya,” alisema
Hassan Tindo, mmoja wa wanachama wa CCM.
Mwanachama mwingine, Nuru Mselemo alisema sasa wanao ushirikiano
kuanzia ngazi ya shina hadi wilaya na kuongeza kuwa ana uhakika wa
kufanya vizuri.
Mnyika apuuza Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John
Mnyika alipohojiwa, alisema kuna mambo ya msingi ya uchumi, siasa na
jamii yanayopaswa kupewa kipaumbele kuliko hilo na kutaka kiongozi wa
Chadema wa Maswa azungumzie hali hiyo.
Katibu wa Chadema wilayani Maswa, Luhende Mipawa alipohojiwa naye
alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia chochote kuhusu suala hilo na
kuwataka CCM kuacha kufanya kazi kwa kupiga ramli.
“Suala hilo mimi siwezi kulizungumzia kwa sasa kwani liko katika
ngazi za juu la vikao vya chama na utaratibu wetu Chadema mambo yetu
yote tunayamalizia kwenye vikao hao wanaodai Shibuda atafukuzwa waache
kufanya kazi kw