Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa Jijini Dar es
Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk
Albina Chuwa alisema, katika kipindi kati ya Aprili mwaka jana na
Aprili mwaka huu kumekuwa na mwenendo mzuri wa bei kwa huduma
mbalimbali.
“Kupungua kwa mfumuko wa bei Aprili mwaka huu kuna
maanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi
uliopita imepungua ikilinganishwa na kasi ya upandaji Machi mwaka huu”
alisema Dk Chuwa na kuongeza:
Mfumuko wa bei umekuwa na mwenendo
wa kupanda kutoka asilimia 8.6 Aprili 2011 na kufikia asilimia 19.8
Desemba 2011 ambapo kuanzia Januari mwaka huu mwenendo wa mfumuko wa
bei ulianza kushuka kutoka asilimia 19.7 hadi kufikia asilimia 18.7
Aprili mwaka huu.
Dk Chuwa alisema, mfumuko wa bei wa vyakula na
vinywaji baridi umepungua hadi kufikia asilimia 25.3 Aprili mwaka huu
kutoka asilimia 25.7 Machi mwaka huu.
“Kasi ya ongezeko la bei
kwa bidhaa zisizo za vyakula imepungua hadi asilimia 11.2 mwezi
uliopita kama ilivyokuwa Machi mwaka huu” alisema Dk Chuwa.
Dk
Chuwa alifafanua kuwa mfumuko wa bei ambao haujumuishi vyakula na
nishati kwa Aprili mwaka huu umeongezeka hadi asilimia 9.0 kutoka
asilimia 8.8 Machi mwaka huu.
“Kwa upande mwingine mfumuko wa bei
wa nishati umepungua hadi asilimia 24.9 Aprili mwaka huu kutoka
asilimia 29.4 Machi mwaka huu” alisema Dk Chuwa
Dk Chuwa
alisema , baadhi ya vyakula vinavyochangia kuongezeka kwa bei ni pamoja
na mchele kwa asilimia 3.0,mahindi asilimia 1.6,unga wa mahindi
asilimia 0.5,vitafunwa asilimia 7.3,unga wa mihogo asilimia 6.7,mayai
kwa asilimia 2.1,siagi asilimia 2.9,machungwa asilimia 6.8,ndizi mbivu
asilimia 4.8.
“Bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka
kwa bei ni pamoja na mavazi asilimia 0.9,gesi asilimia 3.9,mafuta ya
taa asilimia 2.3,mkaa asilimia 5.3,Petroli asilimia 3.9 na begi za
mikononi kwa asilimia 5.6” alisema Dk Chuwa.
Source Mwananchi