Friday, May 11, 2012
WAGONJWA KUTIBIWA BILA KIBALI CHA POLISI
JESHI la Polisi nchini limetoa ruksa kwa hospitali za Serikali kutoa matibabu ya wagonjwa wa ajali mbalimbali bila kibari cha jeshi .
Tamko hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Kamishna wa Operesheni nchini Bw. Paul Chagonja kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Said Mwema wakati wa kuadhimisha siku ya wauguzi duniani.
Bw.Chagonja alisema kuwa jeshi hilo limetoa ruksa ili wagonjwa wa ajali waweze kupata matibabu ya haraka pindi wanapopata ajali za barabarani.
"Kuanzia leo jeshi langu linatoa agizo kwa hosptali zote kutoa matibabu kwa wagonjwa kunusuru maisha yao kwa kutoa matibabu mapema ndipo kibali cha polisi kifuate baadae"alisema Bw.Chagonja.
Alisema kuwa katika utendaji kazi kati ya Jeshi la Polisi na hospitali hasa idara ya wauguzi,wauguzi ni kiungo muhimu kwa kazi hizo na taasisi ya afya kutokana na wauguzi kupokea wahanga wa ajali na watuhumiwa waliopigwa.
Aliwataka wauguzi wote wanapomkumbuka Frolence Nightingale ambaye ni mwanzilishi wa fani hiyo pia wakumbuke maadili katika nafasi hiyo ikiwa ni tegemeo la matumaini ya wagonjwa au majeruhi wanapofika hospitali.
"Mgonjwa anapopata mapokezi mazuri na muuguzi katika kituo cha afya au hospitali yoyote asilimia 100 ya ugonjwa wake utakuwa imepata tiba kabla matibabu kutokana na kauli nzuri ya aliyopewa hata kama ana hali mbaya" alisema.
Pia alisema kuwa Serikali inaingia gharama kubwa katika kutibu wagonjwa wa ajali kwa kuanzia huduma za wodini,matibabu pamoja na vifaa vikiwemo viungo bandia.
Aliwaomba madereva kuzingatia sheria kwa kufuata kanuni na taratibu za matumizi sahihi barabarani ili kuepusha ajali zinazotokea za kizembe.
Bw.Chagonja aliongeza kuwa jeshi hilo pamoja na idara ya wauguzi watashirikiana kwa ajili ya kubadirishana uzoefu katika utendaji wa kazi za kila siku.
Kwa upande wa risala ya wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyosomwa na Katibu wa (TANNA) tawi la Taasisi ya Mifupa na Ufahamu na Ubongo MOI Bi.Dafrosa Mzava alisema kuwa MOI imefanikiwa kupunguza ongezeko la wagonjwa mawodini kwa upande wa upasuaji siku za jumamosi na siku za sikukuu.
Bi.Mzava alisema kuwa pia Mkurugenzi Mtendaji anawapatia elimu ya kutosha katika kuwaendeleza wauguzi kitaaluma ili waweze kutoa matibabu kwa ufanisi.
Kuhusu changamoto za Kitengo cha MOI alisema kuwa kitengo hicho kinaongezeko kubwa la wagonjwa kupelekea wagonjwa kulala chini, na kusababisha watoa huduma kuhudumia wagonjwa wakiwa wamelala jambo ambalo kuleta madhara kwa wahudumu.
"Kutokana na changamoto hizi tulizozitaja wakati wa kuhudumia wagonjwa wakiwa wamelala chini tunapata madhara kama kuumwa migongo na mengineyo.
Alisema kuwa mwaka 2005 kulikuwa na vyumba viwili vya kutoa huduma lakini sasa hivi vimeongezeka na kufikia vitano lakini bado havitoshelezi kutokana na idadi ya wakazi wa Mkoa Dar es Salaam kuongezeka na kufikia zaidi ya milioni 4 kutoka milioni 2.