KAMATI ya Kudumu ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), kufuatilia Sh milioni 216 zilizotokana na
michango ya taasisi na watu mbalimbali kwa ajili ya waathirika wa
mabomu ya Mbagala ambapo zaidi ya Sh bilioni 9 zimelipwa hadi kufikia
sasa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, John Cheyo, alitoa kauli hiyo juzi jioni
wakati wa ziara iliyofanywa na Kamati hiyo, kutembelea maeneo
mbalimbali yaliyoathirika na milipuko ya mabomu hayo iliyotokea mwaka
2009 kwa lengo la kujiridhisha na fidia iliyokuwa imetolewa kwa ajili
ya waathirika hao.
Akizungumzia fedha hizo pamoja na zingine Sh milioni 48 zinazodaiwa
kulipwa kwa watu ambao hawakufanyiwa tathmini yoyote, Cheyo alisema ni
vizuri kama Ofisi ya CAG itafanya uchunguzi wa fedha hizo ili kujua
zimekwenda wapi au zimetumikaje.
“Tumeambiwa kuwa kumbukumbu nzima ya fedha hizi zipo kwa RAS
(Katibu Tawala wa Mkoa), hivyo ni vyema Mkaguzi Mkuu akafuatilia hili
kujua kama kuna aina yoyote ya dosari iliyojitokeza,” alisema Cheyo.
Kauli ya Cheyo imetokana na Mwenyekiti wa Kamati ya Waathirika wa
Mabomu hayo, Steven Gimange kumwomba Mwenyekiti huyo kusaidia kubaini
michango ya fedha hizo sambamba na vitu mbalimbali vilivyotolewa mara
baada ya milipuko hiyo huku vikidaiwa kutowafikia walengwa.
Mbali na hatua hiyo, Cheyo ameagiza pia uchunguzi ufanyike katika
fedha mbalimbali zilizolipwa kwa waathirika hao zikiwamo Sh milioni 185
zinazodaiwa kulipwa zaidi tofauti na tathmini iliyofanywa.
Awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo, alisema
hadi kufikia sasa, Sh bilioni 9 zimelipwa kwa wakazi zaidi ya 10,000
baada ya tathmini mbili kufanyika, huku wakikusudia kumaliza mchakato
huo baada ya kukamilisha tathmini ya tatu hivi karibuni.