Tuesday, March 13, 2012

RAIS KIKWETE ATOA AHADI KWA MADKTARI

 SAKATA LA MADAKTARI

RAIS Jakaya Kikwete amesema atahakikisha anajenga hali ya kuaminiana katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii baada ya kubaini kuwepo kwa tatizo hilo alipokutana na viongozi wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), hivi karibuni.

Rais alikutana na madaktari hao Ijumaa iliyopita baada ya kuitisha mgomo kwa mara ya pili, safari hii wakishinikiza Waziri wa Afrika na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya wajiuzulu au wawajibishwe kabla ya kuendelea na mazungumzo ambayo yalikuwa yameanza ikiwa ni utekelezaji wa kumaliza mgomo wa kwanza.

Alisema baada ya mazungumzo hayo alichobaini ni kutoaminiana na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo kwa kutengeneza mazingira mazuri yatakayowezesha watumishi kufanya kazi kwa kushirikiana.

Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alitumia muda mrefu kueleza mlolongo mzima wa mgogoro huo na jinsi Serikali ilivyoushughulikia na kisha kuelezea jinsi alivyokutana na madaktari hao.

Akielezea mazungumzo kati yake na madaktari hao, Rais alisema aliwaomba wampe sababu za msingi ambazo zimekuwa zikiwafanya wamtake awawajibishe mawaziri hao kabla ya kuendelea na mazungumzo akisema kabla ya mazungumzo hayo hakuwa ameona tuhuma za msingi za kuwang’oa mawaziri hao licha ya kuwa na mamlaka ya kufanya hivyo.

“Nikawaambia nielezeni kwa kina sababu za kutaka niwaondoe vinginevyo mtajikuta na ninyi mnaambiwa mna sababu zenu za kisiasa,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Hoja yao moja ilikuwa ni kwamba wangependa kuzungumza na watu wapya, lakini mimi nikawaambia ni vizuri wakazungumzia zaidi matatizo yao ya kimfumo ili hata akija mwingine mambo yao yasiharibike.”

Alisema mawaziri ni watu wanaopita katika wizara akito mfano wa Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli kwa kusema: “Magufuli alianza Wizara ya Ardhi, baadaye akaenda wizara ya samaki na ng’ombe, sasa hivi yuko wizara ya barabara... sasa jambo la msingi ni kuzungumza matatizo yenu. Hawa ni watu wa kupita na uchaguzi ni miaka mitatu ijayo hivyo mawaziri wataondoka na madaktari watabaki. Nimewaeleza kuwa wao wapo tu.”



Awali, Rais Kikwete alielezea kusikitishwa kwake na hatua ya madaktari hao kugoma akisema hatua yao ilikuwa ni kinyume cha sheria na kanuni za utumishi ambazo licha ya kubainisha hatua zinazopaswa kuchukuliwa kabla ya wafanyakazi kugoma, watumishi wa kada hiyo hawatakiwi kisheria kuchukua hatua hiyo.

Awashukia wanaharakatiKatika hotuba hiyo Rais Kikwete aliwashukia wanaharakati wa haki za binadamu kwa kushabikia mgomo wa madaktari kwa kuishutumu Serikali badala ya kuwataka madaktari kurejea kazini kuokoa roho za binadamu akisema: “Haki ya kwanza ya binadamu ni kuishi.”

“Humu katikati ya mgomo kukajitokeza mambo mengi, adui yako muombee njaa... wakajitokeza hawa wanaojiita wanaharakati na kuanza kushabikia mgomo, hii imenishangaza sana. Nashangaa wanaharakati wa haki za binadamu kujiingiza kwenye hili.

Hivi kuna haki gani kubwa zaidi ya haki ya kuishi? Hii ndiyo haki ya kwanza.”
Rais  alisema wanaharakati wamemfedhehesha kwa kuwa hata kama wangekuwa na ajenda za kisiasa, kwenye suala la mgomo wa madaktari hawakutakiwa kutafuta umaarufu

.UteteziAkizungumzia hotuba hiyo ya Rais, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema harakati zao zililenga kuitaka Serikali iwasikilize madaktari ili wamalize mgomo na warudi kazini.

“Sisi tulikuwa tunataka Serikali iwasikilize madaktari. Vipo vingi tu ambavyo Rais hajavizungumzia ikiwemo mazingira magumu ya kazi, ukizungumza na madaktari watakwambia kuwa kuna vifaa muhimu wanakosa na wagonjwa wanawafia mikononi,” alisema na kuongeza:

“Kuna daktari aliniambia kwa siku hata wagonjwa wanane wanaweza kumfia mbele ya macho yake kwa kukosa vifaa vidogo tu ambavyo vingeweza kuokoa maisha yao. Kwa mfano, mwanamke mjamzito akikosa kuchomwa sindano ya kukata damu baada ya kujifungua yote haya hajayazungumzia.”


Alisema hoja kubwa ya wanaharakati ilikuwa ni kutaka madaktari wasikilizwe haraka na Serikali ili warudi kazini kuokoa maisha ya watu.


“Mwenyewe amekiri kuwa madaktari ni watu muhimu, sasa kwa nini walikuwa hawashughulikii matatizo yao kwa haraka? Wanayashughulikia tu kama vile ni madereva wa trekta wamegoma, kama wanajua ni muhimu ilibidi wakikohoa tu wasikilizwe, mshahara wanaosema waliongezewa Serikali ilifanya hivyo baada ya mgomo wa mwaka 2005,” alisema

SOURCE MWANANCHI