Wednesday, February 29, 2012





WATU AMBAO HAWANA HURUMA NA UTU WAKIMCHOMA MOTO MTU ALIYEDAIWA NI MWIZI WA PIKIPIKI , KWELI SISI BINADAMU  IMEFIKA HATUA MTU ANAMTOA ROHO MWEZAKE , KWANINI SHERIA ZIKAWEKWA?KIJANA ANAYEMCHOMA MOTO MWEZAKE ANA FAMILIA NAJISIAKIAJE ATAPOKUTA NDUGU YAKE AU MTOTO WAKE AMEFANYIWA KITENDO HICHO KWELI MIMI KIMENIUMA MPAKA NIMELIA ,BINABAMU TUMRUDIE MUNGU JAMANI TUNAKWENDA WAPI?




























HOTUBA YA KIKWETE
HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 29 FEBRUARI, 2012

Ndugu Wananchi,
Naomba sote tumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma kwa kutuwezesha
kuzungumza tena mwisho wa mwezi huu.  Katika mwezi tunaoumaliza leo taifa
letu lilipata msukosuko mkubwa kufuatia mgomo wa madaktari.  Nashukuru
mgomo huo umeisha lakini makovu yake yatabaki maisha katika kumbukumbu za
historia ya taaluma ya tiba hapa nchini.
Leo, Mheshimiwa Waziri Mkuu amenipa taarifa kuwa Kamati aliyounda
kushughulikia madai ya madaktari imekamilisha kazi yake na kuwasilisha
taarifa yake kwake.  Kuanzia kesho Serikali itaifanyia kazi taarifa hiyo na
kuamua ipasavyo kulingana na uwezo uliopo.  Nawaomba ndugu zetu madakatari
kuwa na moyo wa subira.  Napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia ndugu
zetu madaktari na watumishi wengine wote wa sekta ya afya kwamba Serikali
inatambua, inajali na kuthamini kazi wazifanyazo na mchango wao katika
kulinda na kudumisha afya za wananchi wa Tanzania.  Aidha, narudia kutoa
pole zangu za dhati kwa wananchi na hasa wagonjwa nchini kwa mateso
waliyoyapata katika kipindi cha mgomo.  Ni matumaini yangu kuwa hali kama
ile haitajirudia tena katika nchi yetu.
Ndugu Wananchi,
Tukio lingine la kusikitisha ni mauaji ya Songea. Yapo yale yanayohusishwa
na imani za ushirikina,  na yapo yale ambayo yalitokea kwenye maandamano.
 Napenda kutumia nafasi hii kuelezea masikitiko yangu kwa vifo hivyo na
kutoa pole na rambirambi zangu na za wananchi wa Tanzania kwa ndugu wa
marehemu wetu hao. Tupo pamoja nanyi katika misiba hii mikubwa na majonzi.
 Napenda kuwahakikishia wananchi wa Songea kwamba Serikali kupitia vyombo
vyake vya usalama imekuwa inafanya na itaendelea kufanya uchunguzi wa kina
wa mauaji haya mpaka wahusika wote wapatikane na kufikishwa kwenye vyombo
vya sheria. Nimearifiwa kuwa, mpaka sasa kwa mauaji 13 yanayohusishwa na
imani za ushirikina watuhumiwa 26 wamekwishakamatwa.  Na kwa mauaji
yaliyotokana na maandamano, askari polisi wanne wamekamatwa na upelelezi
unaendelea.
Ndugu Wananchi;
Nashukuru kwamba amani na utulivu vimerejea katika Manispaa ya Songea.
Nawapongeza sana viongozi wa ngazi zote na wananchi kwa ujumla kwa kazi
nzuri waliyoifanya ya kuwezesha usalama na utulivu kupatikana.  Tafadhali
endeleeni na juhudi hizo mpaka mambo yatengemae kabisa.
Ndugu Wananchi;
Katika mwezi huu pia, Bunge letu Tukufu lilifanya mkutano wake wa sita na
miongoni mwa maamuzi makubwa yaliyofanywa ni kupitisha Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 hususan kuhusu
Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba ya nchi.
 Nimekwishatia saini marekebisho hayo tarehe 20 Februari, 2012 na hivyo
sasa yako tayari kutumika.
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi kwa Wabunge wetu kwa kazi kubwa na
nzuri waliyoifanya ya kupitisha marekebisho hayo.  Aidha, natoa pongezi
maalum kwa vyama vya siasa vya CCM, CHADEMA, CUF na NCCR - Mageuzi pamoja
na Baraza la Taifa la Asasi Zisizokuwa za Kiserikali kwa maoni na
mapendekezo yao ambayo ndiyo yalikuwa chachu ya marekebisho yaliyofanyika.
 Pia, nawashukuru kwa ushirikiano wao uliowezesha mafanikio kupatikana.
Tulipotoka
Ndugu Wananchi;
 Bila ya shaka mtakumbuka kuwa baada ya Bunge kupitisha Muswada wa Sheria
ya Mabadikiko ya Katiba tarehe 18 Novemba, 2011, kulikuwepo na maneno mengi
na maoni mbalimbali katika jamii.  Wapo baadhi ya wadau hasa baadhi ya
vyama vya siasa na asasi za kiraia ambao waliniomba nisitie sahihi Muswada
huo kuwa Sheria na badala yake niagize Bunge liuzungumze upya.  Aidha,
vyama vya siasa vya CHADEMA, CUF na NCCR – Mageuzi na Baraza la Taifa la
Asasi Zisizokuwa za Kiserikali waliomba kukutana nami tuzungumzie mchakato
mzima wa Katiba.  Sikusita kuwakubalia na kwa nyakati mbalimbali tulikutana
na kuzungumza nao.
Ndugu Wananchi;
Katika mazungumzo yangu nao niliwaeleza ugumu niliouona kuhusu kuacha kutia
sahihi Muswada huo na kuurudisha tena Bungeni kujadiliwa upya.  Nilichelea
kuliingiza taifa letu katika mgogoro mkubwa wa kisiasa na kikatiba usiokuwa
na lazima.  Mgogoro ambao tunaweza kuuepuka kwa kutumia njia nyingine za
kikatiba na kisheria kufikia malengo yale yale.  Kitendo cha mimi kukataa
kutia sahihi kingejenga chuki kwa upande wa Wabunge walio wengi ambao
waliujadili Muswada na kuupitisha.  Wengeweza kuhisi wamedharauliwa na
kuonekana hawana thamani.
 Katika mazingira hayo mtakapowarudishia Muswada huo kuujadili kuna hatari
ya kutokupata ushirikiano wao na kushindwa kupata kile kinachotarajiwa.
 Wanaweza kujadili na kuamua kukataa mapendekezo yote mapya na kubakia na
msimamo wao ule ule.
Ndugu Wananchi;
Kwa ajili hiyo, busara ilinielekeza kuwa tusitumie njia hii bali tutumie
njia za kawaida za kufanya marekebisho ya Sheria zilizotungwa na Bunge.
 Hakuna Sheria iliyotungwa na Bunge ambayo haiwezi kufanyiwa marekebisho.
 Kinachotakiwa ni kupeleka mapendekezo ya vifungu au vipengele vya Sheria
husika vinavyotakiwa kurekebishwa.  Bunge litavijadili na kama hoja
zinatosheleza vitafanyiwa marekebisho.  Mimi nilipendelea busara na hekima
hiyo.  Niliwaeleza wadau sababu za kuamua kutia sahihihi Sheria na kuwasihi
wakubali tufanye lililo bora zaidi ambalo ni kupeleka Bungeni mapendekezo
ya sheria hiyo katika maeneo ambayo tunataka marekebisho hayo yafanywe.
Nilitahadharisha kuwa hata kufanya hivyo kunaweza kuwa na ugumu wake hasa
pale dhana zisizokuwa sahihi zitakapopandikizwa kwa Wabunge.  Niliwaomba
tushirikiane kuhakikisha dhana potofu hazijitokezi na zinapojitokeza
tuzisahihishe.  Niliwahakikishia utayari wa Serikali kushirikiana nao
katika hatua zote, tangu kutayarisha mpaka kuwasilisha mapendekezo hayo
Bungeni iwapo watapenda Serikali ifanye hivyo.  Aidha, niliwaambia kuwa
hata sisi Serikalini tulikuwa na dhamira ya kupeleka marekebisho kwa baadhi
ya vifungu vya Sheria hiyo kwa sababu mbalimbali.
  Nafurahi kwamba, kwa pamoja licha ya tofauti zetu kuhusu uamuzi wangu wa
kutia saini Muswada tulikubaliana kushirikiana kutoa mapendekezo ya
marekebisho ya Sheria hiyo, ambayo tuliyawasilisha katika Bunge lililopita.
 Nafurahi na kufarijika kwamba, baada ya mjadala mkali, na Wabunge kufanya
marekebisho kadhaa na hata kuingiza mambo mengine mapya, Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ulipitishwa na Bunge tarehe
10 Februari, 2012.  Baadaye uliwasilishwa kwangu na nikatia sahihi kuwa
Sheria tarehe 20 Februari, 2012.  Sina budi pia kukitambua Chama cha
Mapinduzi ambacho kilileta mapendekezo yake.  Mapendekezo hayo
yalizingatiwa kama ilivyofanywa kwa yale ya wadau wengine.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa vyama vya siasa vya
CHADEMA, CUF, NCCR – Mageuzi na CCM na Baraza la Taifa la Asasi Zisizokuwa
za Kiserikali kwa uelewa wao na ushirikiano wao kulikotuwezesha kufikia
hapa tulipo katika mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya kwa usalama, utulivu
na kwa  maelewano.    Kwa kweli, jinsi hali ilivyokuwa huko nyuma, hatuna
budi kushukuru na kujipongeza.  Ni matumaini yangu na rai yangu kuwa
tutaendeleza ushirikiano na utamaduni huu wa mazungumzo tuliouanzisha na
kuutumia katika hatua zingine zinazofuata.
Nchi imetulia joto na jazba kuhusu Katiba havipo.  Kumbe tukiamua na hasa
tukizungumza inawezekana.  Naomba wadau wote tuazimie kuwa mambo yaendelee
hivi hata katika hatua zijazo za mchakato huu na masuala mengine muhimu kwa
maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Katika mazungumzo yetu na wadau tulikubaliana kwamba tushughulikie
marekebisho ya Sheria hii kwa awamu.  Kwa kuanzia tushughulikie mambo
yanayohusu Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi Kuhusu Katiba
ili iundwe na kuanza kazi.  Baada ya hapo tuangalie mambo yahusuyo Bunge
Maalum na Kura ya Maoni.
 Bahati nzuri Sheria ya sasa inaelekeza kuwa Kura ya Maoni itatungiwa
Sheria yake maalum, hivyo mambo yanaweza kusubiri wakati huo.  Hivyo basi,
baada ya muda si mrefu, Serikali na wadau tutaanza mazungumzo kuhusu
mapendekezo ya marekebisho kuhusu Bunge Maalum.  Kama yatakuwepo na kama
kutafikiwa makubaliano, mapendekezo yatafikishwa katika Bunge letu tukufu
kwa hatua zipasazo.
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri pia kuna kipindi kirefu kidogo wakati Tume inaendelea na kazi
yake mpaka hapo Bunge Maalum litakapoanza kazi.  Tume imepangiwa
kukamilisha kazi yake ndani ya miezi 18 na inaweza kuongezwa miezi miwili.
 Wadau wanaweza kutumia sehemu ya muda huo wa Tume kushughulikia na kufanya
marekebisho yahusuyo Bunge Maalum.  Hata hivyo, kama mapendekezo
yatakamilika mapema ni bora zaidi yafikishwe Bungeni na kushughulikiwa
ipasavyo.
Wadau Kupendekeza Majina
Ndugu Wananchi;
Miongoni mwa marekebisho muhimu yaliyofanywa katika Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba katika Bunge lililopita ni kuwekwa kwa utaratibu wa wadau
kupendekeza kwa Rais majina ya watu wanaoona wanafaa kuteuliwa kuwa Wajumbe
wa Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni kuhusu Katiba.  Nafurahi kutoa
taarifa kwamba nimekwishatoa mwaliko kwa wadau husika, yaani vyama vya
siasa vyenye usajili wa kudumu, jumuiya za kidini, asasi za kiraia pamoja
na jumuiya, taasisi na makundi mengine yenye malengo yanayofanana kuleta
mapendekezo hayo.
Mwaliko wangu huo umeshatangazwa katika Gazeti la Serikali Namba 66 la
Ijumaa tarehe 24 Februari, 2012.  Kuanzia kesho itatangazwa katika magazeti
ya kawaida.  Katika mwaliko huo, wadau wanatakiwa kupendekeza majina
yasiyozidi matatu ya watu wanaokidhi sifa zilizotamkwa katika kifungu cha 6
cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.  Sifa hizo ni hizi zifuatazo:-
(a) Uzoefu  katika kufanya mapitio ya katiba na sifa za kitaaluma za
wajumbe kwenye mambo ya katiba, sheria, utawala, uchumi, fedha na sayansi
ya jamii.
(b) Jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
na
(c) Umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii.
Aidha, nimeelekeza kuwa siku ya mwisho ya wadau kuwasilisha mapendekezo yao
ni tarehe 16 Machi, 2012.  Wadau wanatakiwa kupitishia mapendekezo yao kwa
Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Muungano au Katibu wa Baraza la
Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
 Nimewapa viongozi watendaji wakuu hao jukumu la kupokea mapendekezo ya
majina na kuyawasilisha kwangu.  Baada ya hapo nitashauriana na Rais wa
Zanzibar kuteua Wajumbe wa Tume pamoja na Mwenyekiti na Makamu wake.
Ndugu Wananchi;
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba pia inatoa fursa kwa Rais kuteua Wajumbe wa
Tume kutoka hata nje ya orodha ya wadau.  Ilionekana ni vyema kufanya hivyo
kwani wapo watu wengine wazuri ambao wanaweza kuwa hawamo katika makundi
yaliyotajwa na Sheria hii.  Aidha, upo uwezekanao kwa mapendekezo ya
makundi kutozingatia baadhi ya mambo ya msingi kama vile jinsia, jiografia
na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kadhalika.
   Fursa hii aliyopewa Rais itasaidia katika kuzingatia matakwa haya ya
Sheria.
Pamoja na hayo napenda kuwahakikishia kuwa iwapo nitaitumia fursa hiyo watu
hao hawatakuwa wengi kuliko wale waliopendekezwa na makundi yaliyotajwa
katika kifungu cha 6 (6) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha wadau na wananchi kwa jumla kuwa
Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni Kuhusu Katiba ina Wajumbe 30 tu
wanaopatikana kwa idadi sawa kutoka sehemu zotu mbili za Muungano wetu
yaani 15 kutoka Tanzania Bara na 15 kutoka Zanzibar.  Unapoongeza
Mwenyekiti na Makamu wake kwa jumla Tume itakuwa na wajumbe 32 yaani 16
kila upande.  Hivyo basi, fursa ya kila aliyeleta majina kupata nafasi
katika Tume si kubwa.
Nayasema haya kutahadharisha juu ya ukweli huu ili tusijipe matumaini
makubwa mno na wala tusije tukashutumiana baada ya uteuzi.  Hata hivyo,
pamoja na ugumu wa kuchagua miongoni mwa orodha ya watu wengi wazuri,
nitajitahidi tu Wajumbe wa Tume wawe watu makini, wanaowakilisha sura pana
ya jamii za nchi yetu na makundi yake muhimu na utashi wa watu wa Tanzania
yetu.
Tunapokwenda
Ndugu Wananchi;
Ni matarajio yangu kuwa zoezi la kuunda Tume litakamilika muda mfupi kadri
inavyowezekana, baada ya kupokea mapendekezo ya makundi.  Kama
nilivyokwishawahi kudokeza siku za nyuma, napenda Tume ikamilike kuundwa
katika robo ya pili ya mwaka huu na kuanza kazi muda mfupi baada ya hapo.
Naomba nitumie nafasi hii  kutoa wito maalum kwa wananchi wenzangu kuanza
kujiweka tayari kutoa maoni yao kwenye Tume.  Mambo yataanza miezi michache
ijayo.  Najua Tume itatengeneza utaratibu wa kuelimisha wananchi kuhusu
Katiba.  Lakini nawaomba kila mtu binafsi yake aanze kuchukua hatua za
kuifahamu Katiba iliyopo sasa ili apate ufahamu wa maudhui muhimu ya
Katiba.  Kufanya hivyo kutamuwezesha kuamua kwa usahihi anataka kupendekeza
nini kiwemo katika Katiba mpya.  


Nimeagiza Mpiga Chapa wa Serikali
kuhakikisha kuwa vitabu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania


vinachapishwa kwa wingi ili wananchi waweze kuwa navyo na kuvisoma.


 Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!