Wednesday, April 18, 2012

KAJALA ASOMEWA MAELEZO YA AWALI



Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana ilimsomea maelezo ya awali msanii wa Filamu nchini, Kajala Masanja na mumewe Faraja Mchambo baada ya upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo.

Washatakiwa hao walisomewa maelezo hayo jana na wakili wa serikali kutoka  Takukuru, Leornad Swai mbele ya Hakimu Sundi Fimbo anayesikiliza kesi hiyo.

Baada ya kusomewa maelezo hao washtakiwa hao walikiri mahakamani kuuza nyumba iliyokuwa chini ya uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leornad Swai aliwasomea maelezo hayo ambapo washtakiwa walikiri kuwa ni mume na mke halali wa ndoa  na kwamba walishirikiana kuuza nyumba hiyo kwa Emiliana Rugarulila.

Mchambo alikiri kwamba nyumba hiyo ilikuwa chini ya uchunguzi wa Takukuru na kwamba kabla hajafunguliwa mashtaka hayo alikuwa mtumishi wa Benki ya NBC.

Kadhalika, Mchambo amekiri kuhusika na akaunti za Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) lakini hakufanya utakatishaji wa fedha haramu kupitia akaunti hizo.

Katika hatua nyingine , Kajala na Mchamba walikana kupokea amri (notes) kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikiwataka kutojihusisha na chochote ikiwemo kuuza nyumba hiyo kwa sababu ilikuwa chini ya uchunguzi wa Takukuru.

Aidha, wamepinga kushirikiana kuuza nyumba hiyo iliyozuiliwa kuuzwa na kwamba hawakwenda kinyume na amri iliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wakili Swai alidai kuwa baada ya washtakiwa kukana baadhi ya maelezo hayo, upande wa mashtaka unatarajia kuita mashahidi 13 na kuwasilishwa vielelezo tisa dhidi ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wanadai  kula njama  kinyume na kifungu cha 34 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 ambapo washtakiwa wote kwa pamoja  walitenda kosa hilo la kula njama la kuamisha umiliki wa nyumba  iliyopo Kunduchi Salasala jijini Dar es Salaam.

Shtaka la pili ni kwamba Aprili 14 mwaka 2010 waliamisha isivyo halali umiliki wa nyumba hiyo  kinyume na kifungu cha 34(2)A(3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.

Ilidai shtaka la tatu ni la kutakatisha fedha ambalo walilitenda  siku hiyo ya Aprili 14 mwaka 2010 huku wakijiua ni kinyume na sheria hiyo.

Kesi hiyo itaanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka Aprili 30, mwaka huu.

Soma Majira