Wednesday, April 25, 2012

KESHO SIKU YA MUUNGANO WA TANZANIA NA ZANZIBAR

Na Heri Shaaban
 
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete anatarajia kuwa mgeni rasmi katika madhimisho ya miaka 48 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitakazofanyika katika uwanja wa Uhuru Dar es Salam.
 
 Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa mkoa wa Dar es Salam jana,Bi.Mwamtumu Mahiza alisema kuwa sherehe hizo zitaanza majira ya saa mbili asubuhi ambapo milango ya uwanja huo itafunguliwa kuanzia saa 12 asubuhi.
 
 ''Sherehe hizi za kiistoria za Muungano zilizo asisiwa na waasisi wetu Baba wa Taifa Julius Nyerere na Hayati Habeid Amani Karume zinatarajia kufana"alisema Bi Mahiza.
 
 
Alisema kuwa  viongozi mbalimbali wa chama na Serikali wataudhuria sherehe hizo akiwemo Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt.Mohamed Shein. 
 
Alisema kuwa katika kipindi cha miaka 48 Serikali imepata mafanikio makubwa ya kujivunia  katika nyanja mbalimbali zikiwemo za maendeleo ya jamii,uchumi,siasa ulinzi,usalama pamoja na uhusiano wa kimataifa.
 
Bi.Mahiza alisema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ni miaka 48 ya Muungano  shiriki kikamilifu katika sensa na mchakato wa mabadiliko ya katiba.
 
''Sherehe hizi zitapambwa na gwaride ,halaiki na ngoma kutoka mikoa mbalimbali Tanzania,ambapo pia aliwaomba  SUMATRA na wamiliki wa vyombo vya usafiri kuelekeza magari yao katika kuelekea uwanja wa Uhuru ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wa Dar es Salaam"alisema.
 
Aliwaomba watanzania kudumisha Muungano kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho wache kusikia maneno ya mitaani kwa kuwa viongozi waliopita wasisi wetu waliomba tudumishe muungano huo.