Thursday, May 24, 2012

CAG KUFUATILIA FEDHA ZA WAATHIRIKA MBAGALA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufuatilia Sh milioni 216 zilizotokana na michango ya taasisi na watu mbalimbali kwa ajili ya waathirika wa mabomu ya Mbagala ambapo zaidi ya Sh bilioni 9 zimelipwa hadi kufikia sasa.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, John Cheyo, alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati wa ziara iliyofanywa na Kamati hiyo, kutembelea maeneo mbalimbali yaliyoathirika na milipuko ya mabomu hayo iliyotokea mwaka 2009 kwa lengo la kujiridhisha na fidia iliyokuwa imetolewa kwa ajili ya waathirika hao.

Akizungumzia fedha hizo pamoja na zingine Sh milioni 48 zinazodaiwa kulipwa kwa watu ambao hawakufanyiwa tathmini yoyote, Cheyo alisema ni vizuri kama Ofisi ya CAG itafanya uchunguzi wa fedha hizo ili kujua zimekwenda wapi au zimetumikaje.

“Tumeambiwa kuwa kumbukumbu nzima ya fedha hizi zipo kwa RAS (Katibu Tawala wa Mkoa), hivyo ni vyema Mkaguzi Mkuu akafuatilia hili kujua kama kuna aina yoyote ya dosari iliyojitokeza,” alisema Cheyo.

Kauli ya Cheyo imetokana na Mwenyekiti wa Kamati ya Waathirika wa Mabomu hayo, Steven Gimange kumwomba Mwenyekiti huyo kusaidia kubaini michango ya fedha hizo sambamba na vitu mbalimbali vilivyotolewa mara baada ya milipuko hiyo huku vikidaiwa kutowafikia walengwa.

Mbali na hatua hiyo, Cheyo ameagiza pia uchunguzi ufanyike katika fedha mbalimbali zilizolipwa kwa waathirika hao zikiwamo Sh milioni 185 zinazodaiwa kulipwa zaidi tofauti na tathmini iliyofanywa.

Awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo, alisema hadi kufikia sasa, Sh bilioni 9 zimelipwa kwa wakazi zaidi ya 10,000 baada ya tathmini mbili kufanyika, huku wakikusudia kumaliza mchakato huo baada ya kukamilisha tathmini ya tatu hivi karibuni.