Thursday, May 24, 2012

VIJANA KUMJADILI SHIBUDA

WAKATI mpasuko ndani ya Chadema ukiwaumiza kichwa viongozi wa chama hicho, Sekretarieti ya Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA), inakutana leo kama ilivyoahidiwa mwanzoni mwa wiki hii.

Taarifa ya Katibu wa Bavicha, Deogratias Siale iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa katika kikao hicho kilichoitwa cha kawaida, kutajadiliwa mada zinazohusu mustakabali wa vijana wa Tanzania.

Hata hivyo, pamoja na taarifa hiyo kutokuelezea chochote kuhusu mpasuko unaoendelea ndani ya Chadema ulioanzia Bavicha, mkutano wa leo unatarajiwa kutekwa na mjadala kuhusu mpasuko huo.

Mjadala wa mpasuko huo ni dhahiri kuteka kikao hicho leo hasa baada ya viongozi wa juu wa baraza hilo; Mwenyekiti, John Heche na makamu wake, Juliana Shonza kutofautiana hadharani.

Chanzo cha mpasuko Mpasuko huo wa Chadema ulioanzia Bavicha, ulitokana na kauli ya Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda kutangaza nia ya kugombea urais 2015 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na kuweka wazi kuwa angependa Rais Jakaya Kikwete awe meneja wa kampeni yake kwa kuwa atakuwa akimaliza muda wake.

Shibuda alitangaza nia hiyo alipoalikwa katika kikao cha NEC kama mmoja wa wajumbe wa Mpango wa Afrika wa Kujitathimini Kiutawala Bora (APRM), anayewakilisha Bunge. APRM katika kikao hicho ilialikwa kutoa semina kuhusu utawala bora.

Baada ya kauli hiyo, Heche alimjibu na kusema Bavicha haitamruhusu Shibuda kugombea urais kwa kuwa ametangaza nia hiyo akiwa katika kikao cha CCM na kumtaka Rais Kikwete kuwa meneja wa kampeni zake.

“Kauli hii tunaamini vijana wa Chadema, kuwa mamlaka za nidhamu hazitakaa kimya na kuiachia bila kutakiwa maelezo ya kina, tutaitisha kikao cha Baraza na tutaijadili na kuwasilisha mapendekezo yetu kwenye vikao halali vya chama,” ilisema taarifa ya Bavicha ilyosainiwa na Heche.

Heche katika taarifa hiyo, aliwataka vijana wote Chadema wajiandae kukabiliana na mtu yeyote atakayeonekana kuwa kikwazo kwa chama chao kuelekea kuchukua Dola mwaka 2015.

Baada ya kauli hiyo, Shibuda aliitaka Bavicha kumuomba radhi kwa kuwa alitumia haki yake ya kidemokrasia kutangaza nia na kutishia kuwa isipofanya hivyo, atatumia mbinu ya Chadema ya kuishitaki Serikali kwa wananchi, kuigeuzia kibao Bavicha na kuishitaki kwa wananchi.

Kitisho hicho cha Shibuda, kilimuibua Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Juliana Shonza aliyesema kuwa Heche alitoa kauli binafsi na haihusu Bavicha na kuhoji kwa nini Shibuda asulubiwe kwa kauli hiyo wakati hata Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto alitangaza nia na hakushughulikiwa.

Shonza alisema Heche hakufuata utaratibu unaoongoza baraza hilo wala hakushirikisha viongozi wowote wa juu wa chama na sekretarieti ya baraza, jambo alilosema limekichafua Chama na Baraza.

“Mimi kama Makamu Mwenyekiti, siwezi kuvumilia kukaa na kaa la moto mfukoni, na hili naliongea kutaka kuweka wazi kwamba tamko alilotoa John Heche sio la baraza bali ni tamko lake, na mimi kama kiongozi wa juu nina ujasiri na uhalali wa kisiasa na kisheria wa kutamka hili,” alisema.

Heche ashughulikiwe Kutokana na msimamo huo, Shonza alimshauri Shibuda ashughulike na Heche mwenyewe, badala ya kutaka baraza kumuomba radhi wakati halihusiki na kauli hiyo. Shonza alisema kama Shibuda alikuwa amekosea, Heche angeshauriana na baraza na kwenda kuzungumza na mhusika badala ya kukejeli hadharani.

“Hatutavumilia kumwona kijana wa chama, kiongozi wa ngazi yoyote ndani ya chama kulitumia baraza kwa ajili ya kufikisha matamanio ya fikra zake, tutalinda baraza kulingana na mwongozo wa baraza,” alisema Shonza aliyedai ametoa kauli hiyo kama yeye na si baraza. Bavicha kushughulikiana

Kauli hiyo ya Shonza ilimuibua tena Heche ambaye aliitisha kikao cha kushauriana na Katibu Mkuu wa Bavicha, Siale ambaye baada ya mashauriano ambayo hayakumhusisha Shonza, Siale alituma taarifa katika vyombo vya habari kuitisha kikao cha Sekretariati ya Bavicha leo.

Kikao hicho kwa mujibu wa Siale, ni kwa ajili ya kujadili na kuwasilisha mapendekezo kuhusu kauli ya Shibuda katika vikao halali vya chama kwa ajili ya hatua zaidi.

Hata hivyo, taarifa iliyotumwa jana katika vyombo vya habari, haikuzungumza chochote kuhusu mpasuko huo na badala yake ikajikita zaidi kujadili masuala ya kawaida.

“Sekretarieti ya Bavicha inakutana wakati ambapo hali na mustakabali wa vijana inazidi kuwa tete. Tatizo la ukosefu wa ajira limeendelea kuota mizizi. Vijana wengi, wakiwemo wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu, ikiwemo vyuo hawajui wafanye nini, maana hakuna fursa zinazotengenezwa ili wazitumie kujitafutia maendeleo yao na maendeleo ya taifa kwa ujumla,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilidai kuwa Serikali iliyoko madarakani, chini ya CCM imepoteza mwelekeo katika kushughulikia matatizo yanayowakabili vijana, hususan hili la ajira.

“Sera na mikakati yake imekuwa ni ya kubabaisha ama haitekelezeki. Hivyo kama Bavicha tunapokutana katika kikao cha kawaida cha Sekretarieti tutatoa mawazo ya nini kifanyike katika hali hii ambayo vijana sasa nchini wanakumbana nayo,” ilieleza taarifa hiyo.

Baada ya kikao hicho kwa mujibu wa taarifa hiyo, mawazo yatawasilishwa kwa wabunge wa Chadema ili kupitia Bunge la Bajeti watoe ushauri mbadala na kuiagiza Serikali ya CCM, hatua gani zinatakiwa kuchukuliwa kunusuru kundi la vijana kwa ajili ya maendeleo ya jamii yoyote ile.

Wakati Chadema wakivurugana, CCM imeelezea kusubiri chochote kitakachotokea na ikiwa Shibuda atavuliwa uanachama, kirejee Maswa Magharibi kwa uchaguzi mdogo.

Katibu wa CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema hayo wakati akiunga mkono kauli ya wanachama wa CCM katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu waliodai kuwa iwapo Chadema, kitamvua uanachama na kumfukuza Shibuda watahakikisha kuwa Jimbo hilo linanyakuliwa na chama hicho.

Nape alisema jimbo hilo ni lao, kwani kuna makosa yalifanyika wakati wa uchaguzi mkuu uliopita ambayo wameyabaini na kuyafanyia marekebisho.

“Iwapo Chadema itamfukuza Shibuda na jimbo likawa wazi nawahakikishieni ya kuwa ni lazima tulinyakue kwani katika Uchaguzi Mkuu uliopita sisi Wana CCM katika majimbo yote mawili ya Maswa Mashariki na Maswa Magharibi wagombea wetu wa ubunge walikuwa hawakubaliki kwa wananchi ndio maana tulishindwa vibaya,” alisema Hassan Tindo, mmoja wa wanachama wa CCM.

Mwanachama mwingine, Nuru Mselemo alisema sasa wanao ushirikiano kuanzia ngazi ya shina hadi wilaya na kuongeza kuwa ana uhakika wa kufanya vizuri.

Mnyika apuuza Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alipohojiwa, alisema kuna mambo ya msingi ya uchumi, siasa na jamii yanayopaswa kupewa kipaumbele kuliko hilo na kutaka kiongozi wa Chadema wa Maswa azungumzie hali hiyo.

Katibu wa Chadema wilayani Maswa, Luhende Mipawa alipohojiwa naye alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia chochote kuhusu suala hilo na kuwataka CCM kuacha kufanya kazi kwa kupiga ramli.

“Suala hilo mimi siwezi kulizungumzia kwa sasa kwani liko katika ngazi za juu la vikao vya chama na utaratibu wetu Chadema mambo yetu yote tunayamalizia kwenye vikao hao wanaodai Shibuda atafukuzwa waache kufanya kazi kw