Tuesday, May 8, 2012


MKAPA MAHAKANI KISUTU




•  Waliotemwa uwaziri wamsusa


na Mwandishi wetu

RAIS mstaafu, Benjamin Mkapa, jana aliikaanga serikali ya Jakaya Kikwete mahakamani akidai kuwa hakuna ubadhirifu wowote uliofanywa na aliyekuwa Balozi wa Italia, Prof. Costa Mahalu, katika ununuzi wa jengo la ubalozi nchini humo.
Akiongozwa na wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa, baada ya kuapa alieleza kuwa kati ya mwaka 1995-2005 akiwa Rais alifahamu ununuzi wa jengo la ubalozi nchini Italia kwa euro 3,098,741.40, na kuwa hata aliyekuwa Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye ni Rais wa sasa, Jakaya Kikwete alikubaliana na ununuzi huo.
Mkapa ambaye ni shahidi wa Mahalu katika kesi hiyo alisema mwaka 2003 yeye ndiye aliyekwenda mjini Rome-Italia kulizindua jengo hilo la kisasa, Profesa Mahalu akiwa balozi.
“Serikali yangu iliarifiwa bei na taratibu za kulinunua na mimi kama Rais wa nchi nilitaarifiwa kuwa muuzaji alitaka malipo yafanywe mara mbili tofauti katika akanti zake …na mimi kwa niaba ya serikali yangu nikatoa idhini linunuliwe kwa mtindo huo nilioutaja hapo juu,” alidai Rais Mkapa.
Mahalu anatuhumiwa kuidhinisha kwa niaba ya serikali ununua wa jengo la ubalozi kwa thamani ya euro milioni 3 kwa njia ya mikataba miwili na kwa akaunti mbili.
Mawakili: Wewe au serikali ya awamu ya tatu iliwahi kupokea malalamiko toka serikali ya Italia kuwa ubalozi wetu nchini humo ulivunja sheria kuhusu mchakato mzima wa ununuzi wa jengo hilo?
Mkapa: Hapana, sijawahi kupokea malalamiko.
Mawakili: Ukiwa Rais hujawahi kupokea malalamiko kuwa fedha za serikali yetu zilizotumwa kwa ajili ya kumlipa muuzaji wa jengo hilo kuwa hazijamfikia?
Mkapa: Hadi leo hii natoa ushahidi hapa mahakamani sijawahi kupokea malalamiko ya aina hiyo.
Mawakili: Uliwahi kupata malalamiko toka kwa CAG, Wizara ya Mambo ya Nje, Katibu Mkuu Kiongozi, Waziri wa Mambo ya Nje, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wala Ofisi ya DPP kuhusu ubadhirifu wa ununuzi wa jengo hilo?
Mkapa: Sijawahi kupata.
Mawakili: Nini ufahamu wako kuhusu utumishi wa Profesa Mahalu?
Mkapa: Namfahamu kama msomi mzuri, mchapakazi, muadilifu na kiongozi anayetenda haki.
Mawakili: Mawasiliano kati ya serikali na balozi yanafanyika kwa njia zipi?
Mkapa: Balozi anaweza kuwasiliana na serikali yake kwa njia ya barua kwa Wizara ya Mambo ya Nje, Katibu Mkuu Kiongozi, Rais au kwa njia ya mdomo. Na mawasiliano siyo lazima yafanyike kwa njia ya maandishi tu kwa sababu maelekezo mengine ambayo anapewa balozi na serikali yake ni ya siri kwa maslahi ya taifa hivyo anaweza kuitwa nyumbani na kupatiwa maagizo hayo kwa njia ya mdomo.
Mawakili: Kwa wadhifa wako ule wa urais, kabla ya kwenda kuzindua jengo hilo Januari 23, 2003, hukuwahi kupokea taarifa toka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na DPP za kukukataza usiende kuzindua jengo hilo kwa sababu kulikuwa na harufu za ubadhirifu wa fedha za umma?
Mkapa: Ofisi hizo hazikuwahi kunipatia taarifa hizo.
Yafuatayo ni mahojiano baina ya mawakili wa serikali
Mawakili: Hebu ieleze mahakama ni kwa nini bei za jengo zinatofautiana maana risiti za manunuzi zinaonyesha lilinuliwa kwa euro milioni 3 na hansard ya Bunge iliyosomwa na Kikwete bungeni mwaka 2004 inasema ilinuliwa kwa shilingi bilioni 2.9?
Mkapa: Kazi yangu siyo kufanya uthamini wa fedha za kigeni kwamba wakati huo hizo euro milioni 3 zilikuwa na thamani gani kwa fedha Tanzania (kicheka).
Mawakili: Nani aliagiza upelelezi wa manunuzi ya jengo la Italia ufanyike?
Mkapa: Sijui.
Mawakili: Uchunguzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wewe ukiwa madarakani?
Mkapa: Sijui, nilikuja kuona Balozi Mahalu kashtakiwa mwaka 2007 nikiwa tayari nimestaafu. Nilithibitisha taarifa hizo kupitia vyombo vya habari kuwa ameshtakiwa.
Mawakili: Nani alikupa taarifa za muuzaji wa jengo hilo anataka kulipwa kwa mtindo huo wa akaunti mbili?
Mkapa: Ni Mahalu na alinipa taarifa kwa mdomo na alikuwa ameandaa ripoti juu ya ununuzi na akawa anaomba ridhaa ya serikali kabla ya kulinunua.
Mawakili: Ulisema hukuweza kuzuia ununuzi wa jengo, je ulikuwa na madaraka ya kuweza kuzuia lisinunuliwe?
Mkapa: Eh! Mimi ndiye nilikuwa Rais wa nchi; nilikuwa na madaraka hayo na badala yake fedha hizo zingeelekezwa kwenye mahitaji mengine ila kwa sababu nilikuwa ninajua umuhimu na faida ya nchi kununua jengo lile ndiyo maana nikaridhia kwa mdomo linunuliwe.
Wakili: Ulitoa maelekezo kwa nani?
Mkapa: Nilitoa maelekezo kwa njia ya mdomo kwa watendaji na maagizo hayo yalipaswa yatekelezwe na Wizara ya Mambo ya Nje na ilikuwa jukumu la Mahalu kuieleza wizara hiyo na ubalozi utekeleze maagizo yangu.
Wakili: Kwa hiyo unaieleza mahakama kuwa Wizara ya Mambo ya Nje, ilituma malipo kwa mtindo wa akaunti mbili tofauti?
Mkapa: Inahusu nini sasa? Mimi nilitoa maagizo, hivyo lilikuwa ni jukumu la Balozi Mahalu kuieleza wizara yake. Sasa suala la hayo makaratasi ya kufanya mchakato wa kulinunua, mimi kama Rais siwezi kuingilia. Watendaji walipaswa watekeleze.
Mawakili: Utajisikiaje tukikwambia kuwa yule muuzaji aliyetuuzia jengo kwa mtindo wa akaunti mbili alikuwa akikwepa kodi kwa serikali ya Italia?
Mkapa: Aaah! Mi’ sioni tatizo; kikubwa hapa Tanzania tumepata jengo, Alhamdulilah (kicheko).
Mawakili: Utajisikiaje ukisikia Mahalu alitumia zile euro milioni 3 kwa matumizi yake binafsi?
Mkapa: Nitashangaa sana. Pia wewe wakili wa serikali ndiyo nitakushangaa zaidi kwani hansard ya Bunge iliyosomwa na Kikwete bungeni imetamka bayana kuwa serikali ilimlipa muuzaji wa jengo na kwamba taratibu na sheria ya manunuzi ya umma zilifuatwa na hadi sasa huyo muuzaji hajawahi kulalamika kuwa hajalipwa fedha zake.
Rais Mkapa aliingia mahakamani hapo saa 3:45 asubuhi akiwa katika gari aina VX lenye namba T 745 BQE akiongozwa na walinzi wake.
Maafisa toka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) walionekana kuingia katika viwanja vya mahakama hiyo kabla ya kiongozi huyo kuwasili.
Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Ilvin Mugeta, aliahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo mshtakiwa wa pili aliyekuwa Meneja Utumishi na Utawala wa Ubalozi huo, Grace ataanza kujitetea
www.freemedia.co.tz