Wednesday, May 16, 2012

Mdogo wa Aziz aachiwa huru

Mdogo wa Rostam Aziz aachiliwa huru

Mahakama Kuu Kanda ya Tanga imemwachilia huru mdogo wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Igunga (CCM), Rostam Aziz, Assad Aziz Abdulrasul, aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kula njama na kuingiza dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 92. 2 ambazo zina thamani ya sh bilioni 2.4 baada ya kumuona hana kesi ya kujibu.

Abdulrasul katika kesi namba 19B ya mwaka 2011 alikuwa akikabiliwa na makosa mawili ya kula njama na kusafirisha kiasi hicho cha dawa za kulevya aina ya heroine na alikuwa akitetewa na wakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza. Washtakiwa wengine ni Kileo Bakari Kileo, Yahaya Zumo Makame, Mohammadal Gholamghader Pourdad na Saidi Ibrahim Hamis.


Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Kipenka Mussa, aliyesema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, ushahidi ulitolewa na mashahidi 200 na vielelezo 25 vya upande wa jamhuri, mahakama hiyo imeona ushahidi na vielelezo hivyo havithibitishi mshtakiwa wa saba (Abdulrasul) kuwa alitenda makosa hayo mawili aliyoshtakiwa nayo.


Jaji Kipenka alisema ushahidi na vielelezo vyote umeweza kuishawishi mahakama iwaone washtakiwa waliosalia kuwa wana kesi ya kujibu.
“Kwa sababu hiyo mahakama hii inamuachilia huru mshtakiwa wa saba (Abdulrasul) kwa sababu upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi dhidi yake ila kwa washtakiwa wengine waliobakia katika mahakama hii imewaona wana kesi ya kujibu hivyo watatakiwa wapande kizimbani wajitetee katika tarehe itakayopangwa na mahakama hii,” alisema Jaji Kipenka.


Mapema 2011 ilidaiwa kuwa mshtakiwa alikula njama kusafirisha dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 pamoja na kifungu cha 22(a) and 25 cha Sheria ya Dawa za Kulevya.

Kuwa washtakiwa wote kwa pamoja kati ya Aprili Mosi na Machi 8 mwaka 2009 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, Tanga na Jamhuri ya Iran ,washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama kusafirisha dawa hizo na kosa la pili ni ni la kukutwa na dawa hizo Machi 8, 2010 huko kijiji cha Kabuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga, kitendo ambacho ni kinyume na kifungu cha 16(1)(b)(1) cha Sheria ya Dawa za Kulevya