Wednesday, May 16, 2012

UTOUH UMOJA WA MATAIFA

Utouh kukagua  mahesabu Umoja wa Mataifa  

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,Ludovick Utouh
Mwandishi Maalumu,
New York
IKIWA imebaki  takribani miezi miwili  kabla ya Tanzania  kupitia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa Hesabu za Serikali ( NAOT) kuingia rasmi katika  Ujumbe wa Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa ( UNBOA).  Mkuu wa  chombo hicho, Ludovick Utouh amesema yeye na ofisi yake wamejipanga vema  kulikabili jukumu hilo.

Utouh alisema hayo  juzi wakati alipofanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ,   Asha- Rose Migiro alipomtembelea ofisini  kwake.

Utouh yupo hapa Umoja wa Mataifa akifuatana na   wasaidizi wake  watatu   kwa  ziara ya kikazi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awali  kujiunga na bodi hiyo.

Katika mazungumzo hayo,  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali,  alimhakikishia Naibu Katibu Mkuu kwamba anatambua ukubwa wa  kazi inayomkabili mbele yake,  na dhamana  anayoibeba  kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Watanzania wote.

“Tanzania tumeaminiwa, sifa zetu zinafahamika na ndiyo maana tukapendekezwa kuingia kwenye bodi  hii . Tumejiandaa na kujipanga, tutatumia uwezo wetu na  maarifa yetu  kulikabili jukumu hili na heshima hii tuliyopewa” alisisitiza Utouh.

Alisema yeye na wataalamu wake, na kwa kushirikiana na wajumbe wengine wa bodi hiyo, watalitekeleza jukumu hilo kwa uwazi na siyo kuviziana.

“Tumejipanga kuifanya  kazi hii kwa misingi  na taratibu zote zilizoweka , tutafanya ukaguzi kwa uwazi, tutajadiliana na wahusika,  na siyo kuviziana lengo ni kuboresha utendaji wa chombo hiki muhimu” alisisitiza.

Alibainisha zaidi kwa kusema, ukaguzi wa kuviziana na kuumbuana umeshapitwa na wakati. “Ukaguzi wa  kuviziana ni wa kizamani hata nyumbani ( Tanzania)  hatufanyi  aina hiyo, tumeendelea, tunafanya ukaguzi wa viwango, tunajadiliana , kuelekezana na siyo kuviziana au kukomoana tunataka kujenga na si kubomoa” alisisitiza.

Katika mazungumzo hayo, Naibu Katibu Mkuu Asha- Rose Migiro alimpongeza   Utouh,  ofisi yake na Serikali kwa ujumla kwa kupata fursa hiyo ya kuingia kwenye Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa.
Akasema kuwa, Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa katika  Bara la Afrika katika eneo hilo la ukaguzi wa mahesabu kiasi cha kutambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Mwishoni mwa mwaka jana, Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa lilipitisha uteuzi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali  kuwa  mjumbe wa Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa.

Tanzania inachukua nafasi inayoachwa wazi na Afrika ya Kusini   Julai  mwaka huu na itafanya kazi na wajumbe wengine wawili wa  bodi hiyo  kutoka   Uingereza na China.