Thursday, May 24, 2012

HATIMA YA MNYIKA LEO

HATIMA ya Mbunge wa Ubungo John Mnyika (Chadema) itajulikana leo wakati Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam itakapotoa hukumu ya kesi ya uchaguzi inayomkabili.

Kesi hiyo namba 107 ya mwaka juzi ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hawa Ng’humbi akipinga matokeo yaliyompa ushindi Mnyika katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 kwa madai taratibu na sheria ya uchaguzi zilikiukwa.

Jaji Upendo Msuya anatarajiwa ama kutengua ubunge wa Mnyika au kumtangaza kuwa mbunge halali wa jimbo hilo leo asubuhi mahakamani.

Katika kesi hiyo, Ng’humbi ana hoja tano za msingi ambazo ni kuwepo kwa tuhuma za kashfa kuwa aliuza jengo la Umoja wa Wanawake, kubadilishwa kimakosa kwa kura katika fomu za matokeo ya ubunge, kuwepo kwa watu kimakosa katika chumba cha majumuisho ya kura .

Hoja nyingine ni matumizi ya kompyuta za Mnyika wakati wa majumuisho ya kura na ukiukwaji wa taratibu za kisheria katika uchaguzi huo ambao ulisababisha kuwepo kwa kura hewa 14,854 .

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na upande wa mdai, katika fomu ya matokeo jumla ya kura halisi zilizoandikwa ni 119,823 lakini ukijumlisha kura za wagombea wote unapata kura 132,493 na ukitoa kura halisi na jumla ya kura za wagombea zinabaki kura 14,854.

Wakili wa Ng’humbi Issa Maige alidai kuwa licha ya upande wa wadaiwa kukiri kuwepo kwa kura hewa zaidi ya 14,000 ulishindwa kutoa maelezo ya kina na ufafanuzi kuhusu hizo kura zilitoka wapi na kuiomba Mahakama kubatilisha matokeo hayo.

Wakili wa Mnyika Edson Mbogoro na Wakili Mkuu wa Serikali Justus Mulokozi, waliiomba Mahakama itupilie mbali madai ya Ng’humbi wakidai kuwa ameshindwa kuthibitisha madai yake kwa kiwango kinachokidhi kisheria.

Walidai Ng’humbi alishindwa kuthibitisha hoja alizozitoa; ziliathiri vipi matokeo ya uchaguzi katika jimbo hilo na hata kama kura zilizozidi akipewa Ng’humbi haziwezi kumpa ushindi.

Wakili Mbogoro aliitumia hukumu ya kesi ya uchaguzi wa ubunge wa jimbo la Segerea iliyokuwa imefunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Fred Mpendazoe dhidi ya Mbunge wa jimbo hilo Dk. Makongoro Mahanga wa CCM.

Walalamikiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wasimamizi wasaidizi na Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi ambao wanatetewa na Wakili Mkuu wa Serikali Justus Mulokozi huku Mnyika akitetewa na Mbogoro.