Thursday, May 24, 2012

MSAIDIZI WA KAZI ZA NDANI ALIYETUHUMIWA KUUA MTOTO AKAMATWA

MSICHANA wa kazi za ndani anayetuhumiwa kumuua mtoto wa bosi wake, juzi usiku alinusurika kudhuriwa baada ya kukamatwa na bosi wake aliyejulikana kwa jina moja la Mama Angel.

Gazeti hili lilishuhudia msichana huyo mwenye umri wa miaka 17 (jina limehifadhiwa), akikamatwa juzi saa 6 usiku Sinza nyumbani kwa Mama Angel. Baada ya kukamatwa, majirani wa Mama Angel ambao walishiriki msiba wa mtoto huyo, walishirikiana kutaka kumchukulia sheria mkononi.

Inadaiwa kuwa msichana huyo alisababisha kifo cha mtoto huyo wa miezi saba wakati Mama Angel akiwa kazini Machi mwaka huu na kutoroka nyumbani hapo.

Kijana wa mwenye nyumba hiyo, Ally Hasan alidai alikuwa wa kwanza kugundua kuwa mtoto huyo amekufa baada ya Mama Angel kumpigia akimuomba kumuangalizia mtoto wake huyo aliyekuwa amemuacha amelala.

Hasan alidai alipoingia ndani ya chumba cha Mama Angel, alimkuta mtoto huyo akiwa amelala na hakugundua kuwa alikuwa ameshakufa.

Kwa mujibu wa madai ya Hasan, alitoa taarifa kwa Mama Angel kuwa mwanawe amelala na mama huyo alimuomba amuamshe ndipo alipogundua kuwa amekufa baada ya kuona haamki na kulazimika kutoa taarifa kwa mama mwenye mtoto alirudi nyumbani haraka.

Alidai kuwa mama wa mtoto huyo alipofika na kukuta mtoto ameshakufa kwa kushirikiana na majirani walitoa taarifa Polisi na kumzika.

Hasan alidai walianza harakati za kumtafuta msichana huyo wa kazi na kila walipompigia simu yake, inadaiwa alikuwa akiwajibu kimkato huku akikiri kuwa ameua mtoto huyo.

Naye Mama Angel akizungumza na gazeti hili juzi usiku, alidai alifunga kula na akaamua kufanya ibada kumuomba Mungu amuoneshe alipo msichana huyo, ndipo juzi alipokuwa akipita eneo la Mwananyamala akiwa na mumewe, wakamuona akiwa mtaani.

Alidai kuwa baada ya kumuona, walimkamata na wakampandisha katika teksi na kumpeleka nyumbani kwao Sinza ili kumhoji zaidi.

Mwandishi wa gazeti hili aliyekuwa eneo la tukio wakati dada huyo akishushwa, alimshuhudia mfanyakazi huyo akilumbana na Mama Angel ambapo alimng’ata mama huyo katika bega hali iliyozua tafrani baada ya majirani wa mama huyo kujitokeza kwa wingi kumsaidia.

Baada ya tafrani hiyo, msichana huyo wa kazi aliokolewa na wanaume waliokuwa eneo la jirani ambao walimkamata na kumpeleka nyuma ya nyumba wakamzunguka na kumlinda asidhurike na akinamama hao ambao wengi walikuwa wakidai kama msichana huyo amesababisha kifo, iweje yeye asiuawe.

Mama mzazi wa mtoto huyo akiwa mwenye uchungu, alisikika akieleza kuwa binti huyo anapaswa kuchukuliwa hatua kwa mauaji ya mwanawe, huku akitaka kumuadhibu. Hata hivyo, wanaume waliokuwapo walizuia msichana huyo wa kazi asidhuriwe.

Baadhi ya watu walipomhoji kuhusu kifo cha mtoto huyo, msichana huyo ambaye awali alionesha ujeuri kwa kusema watamfanya nini, baadaye alikuwa mpole na kudai mtoto huyo alimuacha ndani na hajui kilichomkuta.

Baada ya saa moja, waliwasili askari Polisi wa Kituo cha Polisi Mabatini eneo la Sinza waliomchukua na kuondoka naye huku wananchi waliokuwapo nje wakitaka kumdhuru.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alipoulizwa, alisema analifuatilia suala hilo na atatoa taarifa baadaye.