Wednesday, May 16, 2012

NIDA WADAI KUNA VETI 700 AMBAVYO VINA MAJINA YANAYOFANANA

TAARIFA za kwamba Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), imebaini kuwa Jeshi la Polisi lina askari 700 wenye majina yanayofanana na waajiriwa wengine serikalini huku Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likiwa na askari 248 zimeshtua taifa.

Taarifa hizi za kutisha zilipatikana baada ya Nida kuanza utekelezaji wa kuwapatia wafanyakazi wa Serikali vitambulisho vya taifa katika Jiji la Dar es Salaam kabla ya kuwapatia watu wa kada nyingine nchini kote.
Kutokana na uchambuzi wa Nida, polisi na wanajeshi hao wamebainika kutumia cheti kimoja na wafanyakazi wengine wa Serikali kitendo ambacho ni kosa la kisheria.


Kutokana na jambo lenyewe kuwa nyeti na ambalo litakiwa kufanyiwa ufuatiliaji wa haraka, tayari Jeshi la Polisi limeunda tume ya kuchunguza kashfa hii ya vyeti ndani ya taasisi yake.

Hakika ni jambo lisiloweza kufikirika kwamba taasisi zetu muhimu za kulinda raia na mali zao, kulinda mipaka yetu zina wafanyakazi ambao hawana maadili kiasi cha kuthubutu kughusi vyeti kwa lengo la kupata ajira.

Tunaamini kwamba watumishi wa aina hii si hatari  ndani ya jeshi, lakini ni hatari kwa raia kwani wanaweza kufanya lolote hata kama linakiuka maadili ya kazi zao kwa kuwa wao wameweka  maslahi binafsi mbele, uadilifu wa kazi wameuweka kando.

Ndio maana leo katika majeshi yetuna idara kadhaa za Serikali kuna watumishi wengi wasio na maadili kazini kwa kuwa hawajasomea fani husika, bali wametumia njia za hila kupata ajira hizo kama Nida walivyobaini.

Ndio maana tunawapongeza Nida kwa kuweza kugundua kashfa ambayo huenda ikawakumba wengi zaidi hasa pale ambapo wataanza kutoa vitambulisho nchi nzima na hasa kwenye Halmashauri za Wilaya ambako tunaambiwa kuwa kuna idadi isiyo na kifani ya watu wanaotumia vyeti vya watu wengine, wakiwamo walio hai na waliokufa.

Idadio hii kubwa ya waajiriwa wa Serikali wamefanya udanganyifu mkubwa na wanachostahili baada ya uchunguzi kukamilika ni kufukuzwa kazi na kufunguliwa kesi za jinai kwa kughushi ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kufanya mchezo mchafu kama huo.

Kwa kuwa Nida wamefanya uandikishaji wa watumishi wa Serikali katika Jiji la Dar es Salaam pekee, tunaamini kwamba kashfa hii si  tu polisi na wanajeshi pekee bali itagusa maeneo yote.

Mbaya zaidi kashfa za kutumia vyeti bandia huenda vikaikumba sekta ya elimu ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikilalamikiwa kwamba elimu inayotelewa na baadhi ya walimu haikidhi viwango halisi.

Matokeo yake, wanafunzi wengi wanaomaliza elimu ya msingi nchini hawajui kusoma wala kuandika na kibaya zaidi kuna wengine wenye udhaifu huo wanachaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari.

Sote tumeshuhudia askari wengi wakifanya kazi chini ya kiwango kumbe kuna tatizo la msingi nalo ni kutokuwa na elimu inayoendana na kazi wanayoifanya.

 Lakini jambo muhimu la kujiuliza inakuwaje vyombo vya usalama ambavyo vina mkono mrefu vimeshindwa kufuatilia hawa watu kama kweli vyeti wanavyomiliki ni vyao? Je ndani ya vyombo vyetu vya usalama watumishi wote ni raia au kuna wageni? Yote haya ni majibu ambayo tume ya polisi inapaswa kuweka wazi kwa wananchi.


Tunadhani Serikali na vyombo vya dola vitachukulia sakata hili kwa umakini mkubwa ili wale wote wanaohusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.


Ni maoni yetu kwamba wafanyakazi wote ambao wamegushi vyetu vyao na kuajiriwa serikalini na katika sekata binafsi waachie ngazi mara moja na hatua za kisheria zianze dhidi yao kwa uvunjaji wa maadili ambao katu hauvumiliki.

source Mwananchi