Wednesday, May 16, 2012

Nauli
NAULI ya Usafiri wa Daladala ya Cordial Transport Services P.L.C ya jijini Dar es Salaam, imeiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi Kavu na Majini (Sumatra) kupandisha nauli za usafiri huo kwa asilimia 150.

HAbari zinasema kuwa tayari Sumatra imepokea maombi hayo ambapo imeitisha mkutano wa wadau wa usafiri jijini humo ili kupata maoni yao kabla ya kubariki na kuidhinisha matumizi ya nauli hiyo mpya.

Taarifa iliyotolewa na Sumatra jana imeeleza kuwa kampuni hiyo imetoa sababu za kutaka nyongeza hiyo ya nauli kuwa ni ongezeko la mfumuko wa bei, kusababisha  ongezako  la gharama za maisha.

"Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imepokea maombi rasmi kutoka kwa Kampuni ya CORDIAL Transport Services P.L.C. ya usafiri wa Daladala Dar es Salaam ikipendekeza mapitio ya viwango vya nauli za mabasi yanayotoa huduma za usafiri mijini (Daladala)," ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Ofisa Uhusiano David Mziray na kuongeza:

"Sababu zilizotolewa na Kampuni hiyo ni pamoja na ongezeko mfumuko wa bei, hivyo kuongeza gharama za uendeshaji huduma. Mapendekezo ya viwango vipya ni ongezeko la karibĂș asilimia 150 ya nauli za sasa."

Mziray alisema kuwa kutokana na maombi hayo Sumatra imeandaa mkutano wa kukusanya maoni utakaowajumuisha wadau wa sekta ya usafirishaji abiria kwa barabara, wamiliki na watumiaji wa huduma za usafiri pamoja na wananchi kwa ujumla kujadili suala hilo.

"Mkutano huo wa wadau utakaofanyika tarehe 24 Mei, 2012 katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam kuanzia saa 3:30 asubuhi," alisema Mziray.

Alisema katika mkutano huo, uongozi wa hiyo ya usafiri utawasilisha mapendekezo yake ya kuangaliwa upya kwa viwango vya nauli, ambapo wadau watapata nafasi ya kuchangia kuhusiana na mapendekezo hayo.


Alisema mbali na mkutano huo wa wadau, Sumatra pia inapokea maoni kwa maandishi akiwashauri wanaohitaji kufanya hivyo kuwasilisha maoni hayo katika Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra iliyopo makutano ya Barabara za Ally Hassan Mwinyi na Mtaa wa Nkomo kabla ya Juni 6 mwaka huu.